💯KCM2324013; Maisha.
Tumejipata, Tunaachilia Breki.
#JumamosiYaUtulivu
Mwanamafanikio,
Mwaka huu wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kuweka umakini wetu wote kwenye kitu kimoja mpaka kitupe matokeo makubwa.
Na tunaachilia breki kupitia kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kuweza kupiga hatua kubwa.

💯 Neno la leo; Maisha.
Leo ikiwa ni #JumamosiYaUtulivu tunaangalia jinsi ambavyo utulivu ndiyo maisha yenyewe.
Tumezoea mahangaiko kwenye maisha kiasi cha kuyachukulia maisha kama ni mahangaiko.
Watu wengi wamekuwa wanahangaika kwenye maisha yao yote, kiasi cha kuondoka hapa duniani wakiwa hawajayaishi maisha kabisa.
Kila wakati wanakuwa kwenye hali ya msongo ambao unawapelekea kuwa kwenye hali ya wasiwasi na mahangaiko makubwa.
Maisha ya aina hiyo, yamekuwa hayana utulivu na hivyo kukosa ubora.
Maisha yasiyo bora huwa hayana furaha hata kama mtu amepata mafanikio makubwa.
Pamoja na juhudi kubwa unazoweka kwenye yale unayofanya, pamoja na msongo ambao unakutana nao mara kwa mara, usiache kutafuta utulivu wa maisha.
Kila mara rudisha akili yako na roho yako kwenye hali ya utulivu ili upate fursa ya kuyaishi maisha.
Pamoja na mengi unayoyapitia kwenye siku yako, usiache kutenga muda wa kwa ajili yako.
Tumia muda huo kuyatafakari maisha yako kwa kina na kufanya tahajudi.
Muda huu unakurudisha kwenye kusudi kuu la maisha yako.
Kukosa utulivu kwenye maisha ni sawa na mtu ambaye anakimbia kwa kasi wakati amepotea njia.
Kadiri anavyoongeza kasi, ndivyo anavyozidi kupotea.
Wewe nenda kasi, lakini mara kwa mara tulia na utafakari kama bado upo kwenye njia sahihi au umeshapotea.
Hilo ni zoezi la kufanya kila siku, la sivyo ni rahisi sana kupotea.
Safari ya maisha haina tofauti na safari ya ndege angani.
Kazi kubwa ya rubani wa ndege ni kuirudisha ndege kwenye njia yake kutokana na kusogezwa pembeni na vitu mbalimbali, kama upepo na mawingu.
Kadhalika kwenye maisha yako, kila msongo unaokutana nao unakuondoa kwenye njia yako kuu.
Kama utaendelea kwenda bila ya kupata utulivu wa kutafakari kwa kina, utajikuta umepotea kabisa.
Lakini kwa kupata muda tulivu kila siku na kujitafakari, utaweza kurudi kwenye njia yako kuu na kufanya makubwa.
💯Hatua za kuchukua leo;
- Andika ahadi yako ya mwaka wa mafanikio 2023-2024 kwa mtiririko wa NINI, LINI, WAPI, KWA NINI, NANI, VIPI na HISIA kisha weka kwenye kundi.
- Soma kurasa 10 za kitabu cha MTAALA WA UTAJIRI na shirikisha uliyojifunza kwenye kundi.
- Chukua hatua kwenye yale ambayo umeshajifunza na shirikisha kwenye kundi.
- Matokeo unayopata yashirikishe kwenye kundi.
- Kaa kwenye mchakato sahihi wa kile unachotaka kufikia na epuka usumbufu unaokuwa kikwazo kwako.
Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu mchezo unaocheza. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2023/11/11/3237
Ukawe na siku bora kabisa ya leo, siku unayokwenda kushika hatamu ya maisha yako na kuifanya kuwa ya kipekee kabisa kwako.
Kocha.
💯