3288; Hatua unayochukua.

Rafiki yangu mpendwa,

Kila mtu kuna vitu anavyokuwa anavitaka kwenye maisha yake.
Na anaweza kujiwekea malengo na mipango mbalimbali juu ya vitu anavyotaka.

Lakini ili mtu aweze kupata kile anachotaka, anapaswa kuchukua hatua kwenye yale anayopanga.
Hilo ni la msingi kabisa, lakini limekuwa linapuuzwa na wengi.
Wengi wanadhani kupanga na kusema inatosha kuwaletea yale wanayoyataka.

Kuna ambao wanaanza kuchukua hatua, lakini wanapokutana na magumu au changamoto mbalimbali wanaacha kwa kuona haiwezekani.
Hawa nao hawapati wanachotaka, siyo kwa sababu haiwezekani, bali kwa sababu hawajafanya kadiri ya inavyohitajika.

Kuna wanaofanya, lakini matokeo yanapochelewa wanaacha kufanya. Wanaona kuchelewa kwa matokeo ni kutokuwezekana kwa kitu.

Halafu sasa, kuna ambao wanafanya, wanapata matokeo makubwa, halafu wanaacha kufanya kwa kuona wameshamaliza kila kitu.
Hawa nao huwa wanapata anguko kubwa baadaye.

Mafanikio na kufanya ni vitu ambavyo vinakwenda pamoja na haviwezi kutenganishwa.
Tangu mtu anapoanza mpaka anafanikiwa, lazima awe anaendelea kufanya bila ya ukomo.
Ni kupitia kufanya ndiyo mtu anaweza kujifunza na kuwa bora zaidi.

Kwa kufanya, mtu anapiga hatua kubwa sana kuliko kupanga na kusema pekee.
Unachotaka na unachofanya vinapaswa kwenda pamoja ili uweze kupiga hatua kubwa kwenye maisha yako.

Usiwapigie watu kelele sana juu ya nini unachotaka.
Bali waonyeshe kwa yale unayofanya.
Fanya wakati wote, bila kuchoka wala kuacha na utaweza kuzalisha matokeo makubwa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe