KCM2324064; Ngazi.
Tumejipata, Tunaachilia Breki.
#JumatatuYaMalengo
Mwanamafanikio,
Mwaka wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kufanyia kazi kwa ukubwa kitu kimoja mpaka kitupe mafanikio makubwa tunayoyataka.
Tumeachilia breki kwa kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kujipa uhakika wa kufanya makubwa.

Neno la leo; Ngazi.
Leo ikiwa ni #JumatatuYaMalengo tunaona jinsi ambavyo kila hatua kwenye ngazi ni safari ya kwenda juu zaidi na siyo mahali pa kupumzika.
Unapoweka malengo kwenye maisha, huwa unayagawa kwenye vipande vidogo vidogo ambavyo unavifanyia kazi.
Ushindi unaoupata kwenye kila kipande ndiyo unapaswa kuwa msukumo wa kwenda kwenye hatua nyingine inayofuata.
Ni sawa na mtu unavyokuwa unapanda ngazi, kila hatua unayopiga ni safari ya kwenda hatua ya juu zaidi.
Hatua unazokuwa unapiga siyo mwisho wa safari au mahali la kupumzika, bali ni sehemu ya safari ambayo ni endelevu.
Unaweza kufurahia na kujipongeza kwa kila hatua unayokuwa unapiga, kwa sababu siyo rahisi.
Lakini ukidhani umeshamaliza na kuacha kuendelea, siyo tu kwamba utabaki pale unapokuwa umefika, bali utaanza kuanguka na kurudi chini.
Safari ya mafanikio ni sawa na kuendesha baiskeli, kadiri unavyochochea ndivyo unavyokaa kwenye mwendo. Ukiacha kuchochea, siyo tu baiskeli inakosa mwendo, bali pia inaanguka.
Kwenye mafanikio, kadiri unavyoendelea kuchukua hatua ndivyo unavyoendelea kufanikiwa.
Ukiacha tu kuchukua hatua, siyo tu unakwama kuendelea, bali pia unaanza kuanguka kwenye yale ambayo ulishayafanikisha.
Endelea kupiga hatua kwenye ngazi yako ya mafanikio.
Kwa kila hatua unayopiga, ndiyo unaona hatua nyingine ya juu zaidi kwako kuipiga.
Hupaswi kuchoka wala kuona umemaliza.
Bali unapaswa kuendelea kuzipiga hatua za mbele zaidi.
Hivyo ndivyo unavyojenga na kudumisha mafanikio makubwa kwenye maisha yako.
Kuwa na malengo unayoyafanyia kazi kwa uendelevu ni moja ya njia za kuachilia breki zinazowakwamisha wengi.
Zingatia hilo mara zote ili uweze kupata kila unachotaka kwenye maisha yako.
Hatua za kuchukua leo;
1. Andika ahadi yako ya mwaka wa mafanikio 2023-2024 kwa mtiririko wa NINI, LINI, WAPI, KWA NINI, NANI, VIPI na HISIA kisha weka kwenye kundi.
2. Soma kurasa 10 za kitabu cha MJASIRIAMALI MJANJA na shirikisha uliyojifunza kwenye kundi.
3. Chukua hatua kwenye yale ambayo umeshajifunza na shirikisha kwenye kundi.
4. Matokeo unayopata yashirikishe kwenye kundi.
5. Kaa kwenye mchakato sahihi wa kile unachotaka kufikia na epuka usumbufu unaokuwa kikwazo kwako.
Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu hatua unayochukua. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2024/01/01/3288
Ukawe na siku bora kabisa ya leo, siku ya kuendelea kupiga hatua kwenye ngazi yako ya mafanikio ili kufika juu zaidi ya pale unapokuwa.
Kocha.