Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Huwa ni rahisi kwetu kuwalaumu watu ambao wanashindwa kutimiza majukumu yao na kuishia kutukwamisha kwenye mambo yetu. Tunaona wao wakiwa sababu ya sisi kushindwa yale tunayoona tunastahili kuyapata.
Lakini, sisi wenyewe, ndiyo watu wa kwanza kujikwamisha, kwa kushindwa kutimiza wajibu wetu mkuu tulionao kwenye maisha. Ni wajibu mmoja mkubwa sana, ambao tukiweza kuutimiza kikamilifu, mambo mengine yote yanawezekana.
Kwa bahati mbaya sana, hakuna mahali ambapo tunafundishwa kuhusu wajibu huo na jinsi ya kuutimiza. Tunatumia muda mwingi wa maisha kujiandaa kutimiza wajibu huo, mpaka tunaishia kuondoka kwenye maisha tukiwa hatujautimiza.
Kwenye barua hii tunaenda kuangalia wajibu huo na jinsi tunavyopaswa kuutimiza ili kuweza kuwa na maisha ya mafanikio kama tunavyotaka.

1. Wajibu Wako Mkubwa Maishani.
Ni kuishi. Huu ndiyo wajibu namba moja, ni wajibu ambao ukiweza kuutimiza, mambo mengine yote yanakwenda vizuri kama unavyotaka.
Unaweza kujiuliza kwani huishi? Na hilo ni swali ambalo hata mimi nitakuuliza, ili ujitafakari na kuchukua hatua sahihi.
Kuna kuishi na kusukuma tu maisha. Watu wengi hawaishi, badala yake wanasukuma maisha, wanasogeza siku.
Hilo linadhihirika kwa jinsi mtu anavyokuwa anajiandaa kuishi badala ya kuishi. Akiwa mtoto anakuwa anajiandaa kuwa mtu mzima ili aishi. Akiwa mtu mzima anajiandaa kupata kazi au biashara ndiyo aishi. Baadaye anajiandaa kuwa na familia, anajiandaa kulea watoto. Mchezo unaenda hivyo mpaka maisha yanafika ukingoni bila ya kuyaishi.
Na kama bado unajiuliza mtu anapaswa awe na maisha ya aina gani ndiyo awe anaishi, sehemu inayofuata inaeleza hilo.
2. Kuishi Ni Kutengeneza Ulimwengu Wako.
Unazaliwa na kujikuta kwenye ulimwengu ambao tayari upo na utaishi kwenye ulimwengu huo. Mwanzo utapaswa kuishi kwenye ulimwengu huo kikamilifu, kama sehemu ya kujifunza na kujenga maisha yako.
Ili kuishi maisha yako, ni lazima uende zaidi ya ulimwengu ambao umejikuta. Ni lazima utengeneze ulimwengu wako mwenyewe, ambao unaendana na vile ulivyo wewe, ambapo ni wa kipekee.
Huwa tunadhani ulimwengu tuliojikuta ndani yake ndiyo ulimwengu pekee uliopo na ndiyo ulio sahihi kwa watu wote. Ambacho hatujui ni kwamba ulimwengu ambao tumejikuta, umetengenezwa na watu kama sisi, ambao hata hawakuwa na kikubwa cha kutuzidi.
Waliotengeneza ulimwengu ambapo tumejikuta walikuwa na ujasiri wa kuchagua kuyaishi maisha kwa namna yanaendana na wao. Badala ya kuiga na kufuata mkumbo, walichagua kuleta maono na ndoto zao kwenye uhalisia.
Hujaishi kama kila unachofanya ni kile kinachofanywa na watu wengine. Maisha yanaanza pale unapogeuza maono na ndoto zako kuwa uhalisia. Hapo ndiyo unakuwa na fursa ya kuipa dunia zawadi iliyo ndani yako. Na hiyo ndiyo nafasi ya kuacha alama ya kipekee hapa duniani, ambayo itaonyesha kweli uliishi.
Unapoishi maisha ya kuiga na kufuata mkumbo ni kama unatupa jiwe gizani, huwezi kujua kama limempata mtu kama hutasikia milio. Kama leo utaondoka hapa duniani na hakuna kikubwa ambacho watu watakumbuka kuhusu wewe, maana yake hukuishi.
Huenda unadhani ili uishi inabidi ufanye mambo ya kimuujiza sana, hilo siyo sahihi, kila mtu ana fursa ya kuishi, kwa chochote anachochagua kufanya, kama utakavyoona kwenye sehemu inayofuata.
Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; 081; Una Huu Wajibu Mkuu Mmoja Kwenye Maisha, Utimize Kwa Ukamilifu