Sikiliza hapa;

Rafiki yangu Mpendwa,

Inapokuja kwenye mafanikio, nimekuwa nakusisitizia mambo mawili ya kujenga, tabia na nidhamu sahihi ya mafanikio. Huwa tunajenga tabia na kisha tabia zinatujenga, kwa sababu sehemu kubwa ya mambo tunayofanya kila siku tunaongozwa na tabia. Tukiweza kujenga tabia sahihi, sehemu kubwa ya safari ya mafanikio inakuwa imefanikiwa.

Ili kujenga tabia sahihi, nidhamu inahitajika sana. Na hapo ndipo mtego mkubwa ulipo, kwa sababu kujenga nidhamu kunatutaka kujisukuma zaidi ya tunavyotaka sisi wenyewe. Nidhamu ni kutekeleza yale uliyopanga, kama ulivyopanga, iwe unajisikia au hujisikii. Nidhamu ni kubaki kwenye mpango wako na kuachana na hisia zako.

Kwa sababu kwa asili sisi binadamu ni viumbe wa kihisia, tunaofanya mambo kwa kusukumwa na hisia, nidhamu imekuwa inaonekana ni kujitesa, kwa sababu inatutaka kwenda kinyume na hisia. Kwa kuona nidhamu ni mateso inakuwa kitu kigumu kujijengea.

Kwenye barua hii tunaenda kuangalia upande wa pili wa nidhamu binafsi, ambao una siri nzuri ambazo wengi hawazijui. Wakati tunaangalia nidhamu kama kujitesa, tunashindwa kuona upande mwingine wa nidhamu ambao ni kujitengenezea mazingira bora zaidi.

1. Nafsi Zako Tatu Na Jinsi Zinavyohujumiana

Hivi umewahi kujiuliza, iweje, wewe mwenyewe, ukae chini na kupanga kitu ambacho utafanya na muda wa kukifanya. Lakini muda huo wa kufanya ulichopanga unapofika, unaahirisha kukifanya?

Kama hiyo haitoshi, siku zinazokuja, unajilaumu kwa kutokufanya yale uliyokuwa umepanga. Sijui kama unanipata vizuri hapo, unapanga, hufanyi, halafu unajilaumu. Unaona kila kitu kipo sawa hapo?

Ukweli ni kila kitu hakipo sawa, na hiyo ni kwa sababu umekuwa unayaendesha maisha yako kwa kutumia nafsi moja, wakati ndani yako kuna nafsi tatu. Kwa kushindwa kuzitambua nafsi hizo tatu, umekuwa unajihujumu wewe mwenyewe.

Una nafsi tatu ndani yako, nafsi ya wakati uliopo (nafsi ya sasa), nafsi ya wakati uliopita (nafsi ya jana) na nafsi ya wakati ujao (nafsi ya kesho). Nafsi hizo zipo hai ndani yako na zinahusika kwenye maamuzi yote unayoyafanya. Tatizo kubwa ni umekuwa unaweka uzito kwenye nafsi moja pekee, na hilo ndiyo limekuwa linakukwamisha.

Unatumia nafsi ya sasa kufanya na kutekeleza maamuzi. Mipango na utekelezaji wa nafsi ya sasa ndiyo inaamua nafsi ya kesho inapata nini. Tatizo kubwa ni nafsi ya sasa huwa inapenda kujisikia vizuri, bila kujali madhara kwa nafsi ya kesho. Kwa kuizingatia nafsi ya sasa pekee, utajisikia vizuri, lakini madhara yatakuwa makubwa kwa nafsi ya kesho.

Nafsi ya kesho inapofikiwa, inaishia kulaumu nafsi ya jana kwa kushindwa kufanya yale yaliyopaswa kufanyika. Nafsi ya jana inayokuwa inalaumiwa ni nafsi ya sasa ambayo haikufanya maamuzi sahihi.

Sijui kama tuko pamoja au nimeshakuchanganya hapo. Labda twende taratibu kidogo, una nafsi ya sasa, ambayo kipaumbele chake ni kujisikia vizuri. Ukiitimizia hilo nafsi ya sasa, madhara yanaonekana kwenye nafsi ya kesho. Ambayo italaumu nafsi ya jana kwa kutokufanya maamuzi sahihi.

Kwa maana hiyo basi, ili uache kujihujumu wewe mwenyewe, unapaswa kuacha kufanya maamuzi kwa kuzingatia nafsi ya sasa pekee. Jikumbushe jinsi unavyotumia nafsi ya sasa kulaumu nafsi ya jana, kisha angalia nafsi ya kesho inadhurikaje na maamuzi yoyote unayofanya kwa nafsi ya sasa.

Kwa kila maamuzi unayoyafanya, fanya kikao na nafsi zako zote tatu kuhakikisha zimeshiriki kikamilifu. Iulize nafsi ya leo ni nini inalaumu kwa nafsi ya jana. Kisha uilize nafsi ya kesho nini ingepata kifanyike ili kusiwe na madhara. Hapo sasa unaweza kuitumia nafsi ya sasa kufanya maamuzi yaliyo sahihi.

Nidhamu binafsi ni kuhusisha nafsi zako zote tatu kwenye maamuzi na utekelezaji wa malengo na mipango yako. Kuhakikisha nafsi zote zimeridhika na maslahi yamezingatiwa.

2. Kumbuka Leo Ni Kesho Uliyoisema Jana.

Kitu kimoja kuhusu sisi binadamu ni jinsi tunavyosahau vitu haraka. Tumekuwa tunasahau vitu muhimu haraka sana, na hilo limekuwa linatukwamisha kupiga hatua kubwa kadiri ya tunavyotaka.

Unapanga vizuri nini utafanya na wakati wa kufanya. Ila wakati wa kutekeleza mipango unapofika, unaahirisha kwa kujiambia utafanya wakati mwingine. Ni kama unadhani wakati huo mwingine ni mbali sana. Ambacho hatujikumbushi ni kwamba muda tulionao sasa, ndiyo ambao tuliahirisha vitu huko nyuma.

Hapo ulipo sasa ni matokeo ya nidhamu binafsi ambayo umekuwa nayo huko nyuma. Kama upo kwenye changamoto za kifedha leo, ni kwa sababu ya nidhamu ya kifedha uliyokosa siku za nyuma. Kama afya yako ina changamoto leo, ni kwa sababu ya vitu ulivyofanya au kushindwa kufanya siku za nyuma.

Hii haimaanishi turudi huko nyuma tukabadilishe, bali tunapaswa kutambua sasa tuna nafasi ya kupunguza makosa ya siku zijazo. Kwa sababu, siku zijazo zitafika na yale tuliyopanga kufanya tutakuwa hatujayakamilisha na hivyo kuwa tumejikwamisha sisi wenyewe.

Kila unapotaka kubadili mipango uliyoweka, jiulize kama unaridhika na hapo ulipo sasa. Kama unaridhika, maana yake una historia ya kubadili maamuzi yako kwa mafanikio makubwa. Kama huridhiki, maana yake huna historia ya kubadili maamuzi yako kwa mafanikio. Wajibu wako ni kuhakikisha unatekeleza maamuzi ambayo yatakufikisha kwenye matokeo unayotaka.

Kwa kujikumbusha jinsi umekuwa unajikwamisha huko nyuma, utaweza kuondoka kwenye mtego wa kujidanganya kirahisi kwa nafsi yako ya sasa. Ipe nguvu nafsi yako ya kesho ihusike kwenye maamuzi ya sasa ili isihujumiwe kwa raha unazotaka kupata sasa.

Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK087; Siri Nzuri Usiyoijua Kuhusu Nidhamu Binafsi