Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Mtoto anapozaliwa, anakuwa hajui vitu vingi kuhusu maisha. Lakini anazaliwa akiwa anajua kufanya vitu vinavyohitajika ili aweze kuwa hai. Hivyo mtoto anazaliwa akiwa anajua kunyonya na kulia pale ambapo kuna kitu hakipo sawa kwake.
Ndiyo maana uwezo wa kunyonya na kulia ndiyo vitu vya kwanza vinavyopimwa kwa kila mtoto anayezaliwa. Hivyo vikiwepo, mtoto anaweza kuishi, na kama vitakosekana, mtoto atakuwa na changamoto kubwa.
Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye mafanikio yoyote tunayotaka kuyapata kwenye maisha yetu. Tayari tunajua nini hasa tunapaswa kufanya ili kupata mafanikio hayo. Haiwezekani uwe unataka kitu, halafu usijue jinsi ya kupata kitu hicho.
Na jinsi ya kupata tunachotaka, huwa inaanzia ndani yetu wenyewe, kwa sababu tunachokuwa tunataka huwa ni tofauti kabisa na vitu wanavyotaka watu wengine. Lakini pia tumekuwa tunajifunza kwa wengine yale yanayopaswa kufanyika ili kupata mafanikio tunayokuwa tunayataka.
Kitu ambacho kimekuwa kinashangaza, na ambacho kimewakwamisha wengi kupata mafanikio ni kutokufanya yale ambayo yanapaswa kufanyika. Licha ya kujua nini cha kufanya, bado wengi wamekuwa hawafanyi.
Pamoja na kutokufanya, bado wamekuwa ndiyo watu wa kulalamika sana kuhusu kukosa matokeo wanayokuwa wanayataka. Ni jambo linaloshangaza sana, mtu anajua anachopaswa kufanya, hakifanyi na bado analalamika kutokupata matokeo anayoyataka.
Ili tuweze kutatua tatizo hili la kujua cha kufanya na kutokukifanya, lazima tujue nini kinachosababisha. Kwenye hii #BaruaYaKocha tunaenda kuangalia kinachosababisha tushindwe kufanya yale tunayojua yanapaswa kufanyika. Tutaona jinsi ya kuvuka hayo yanayotukwamisha ili tuweze kupiga hatua kubwa tunazotaka kupiga.

1. Unadhani Kuna Njia Nyingine Tofauti.
Watu ambao hawajafanikiwa huwa wanashangaza sana. Wanapowaangalia watu waliofanikiwa kuliko wao, wanaona kuna kitu watu hao wanakuwa wanajua ila wao hawajui. Kinachoshangaza ni pale wale waliofanikiwa wanapoeleza siri zao za mafanikio, wasiofanikiwa huwa wanakataa kwamba vile wanavyoeleza ndiyo vimewapa watu hao mafanikio. Wanakuwa wanaamini kwamba kuna siri nyingine kubwa zaidi wamezificha na hawawezi kuzisema.
Tunapojua yale tunayopaswa kufanya ili tufanikiwe, huwa hatuamini kama ndiyo hayo tu yanahitajika. Tunadhani kuna njia nyingine tofauti, ambayo inaweza kuwa ya siri zaidi, rahisi zaidi au ambayo ni bora zaidi. Huwa tuna picha zetu wenyewe za namna ya kupata mafanikio bila kutumia njia zilizoainishwa wazi.
Ni hali hiyo ya kudhani kuna njia ya tofauti ndiyo imepelekea watu wengi kuhangaika na fursa mpya kila wakati bila kupiga hatua. Ukishajikuta umefanya kazi au biashara nyingi na hakuna matokeo makubwa uliyopata, tatizo ni wewe kufikiri kuna njia ya tofauti ambayo bado hujaijua.
Kinachokufanya kila wakati utafute kazi au biashara mpya ya kufanya, ambayo unaona ndiyo itakupa mafanikio unayotaka kwa haraka zaidi ni kudhani kuna njia ya tofautia mbayo bado hujaijua.
Kuondokana na mkwamo huu, acha kutafuta njia ya tofauti. Tambua kwamba njia iliyo mbele yako sasa ndiyo njia inayoweza kukupa mafanikio makubwa unayoyataka. Tambua kwamba kitakachokupa mafanikio siyo kile unachofanya, bali jinsi wewe unavyokifanya.
Kazi au biashara yoyote ile ina uwezo wa kukupa mafanikio makubwa unayoyataka. Kinachohitajika ni wewe ujue nini unapaswa kufanya, ufanye hicho unachopaswa kufanya na uende hivyo kwa msimamo bila kuacha. Hata ukutane na magumu na changamoto kiasi gani, wewe endelea kufanya na utapata matokeo mazuri.
2. Unaona Bado Hujawa Tayari.
Kitu kikubwa ambacho kimewazuia watu wengi kufanikiwa ni kunasa utotoni. Kunasa utotoni ni kuishi maisha ya kujiandaa kila wakati. Tunapokuwa watoto, tunakuwa tunajiandaa kuwa watu wazima. Tunaenda shule kama sehemu ya kujiandaa kuja kufanya kazi na/au biashara ili kuishi maisha yetu.
Lakini kwa bahati mbaya sana, hayo maandalizi yamekuwa hayana mwisho. Kwani hata baada ya kumaliza elimu, bado watu wanakuwa kwenye maandalizi ya kupata kazi au biashara. Wakipata kazi au biashara, wanaingia kwenye maandalizi ya kuwa na familia. Wakipata familia wanakuwa kwenye maandalizi ya malezi. Mtu anaenda hivyo mpaka anazeeka na kujikuta hajawahi kuyaishi maisha yake, badala yake alikuwa kwenye maandalizi tu.
Unajua kabisa ni nini unapaswa kufanya ili ufanikiwe, ila unaona bado hujawa tayari kufanya kitu hicho. Unaona unahitaji maandalizi zaidi ndiyo uweze kufanya hicho unachopaswa kufanya. Hilo limekuwa linakukwamisha kuchukua hatua ambazo unajua kabisa kwamba unapaswa kuzichukua.
Kuondokana na kikwazo hiki, unapaswa kujua kila wakati upo tayari kufanya kile kinachopaswa kufanyika. Ondoka kwenye akili ya utotoni ya kusubiri mpaka uwe tayari. Upo tayari kwa vile ulivyo sasa. Kila ulichonacho sasa kinakutosha kutumia kupata matokeo unayoyataka.
Na hata kwa vitu ambavyo unaona unavikosa, wewe anza kufanya na utaona vitu hivyo vikipatikana. Kuna milango ukiiangalia unaona imefungwa, ila unapoifungua, unakuta ni rahisi kabisa kuifungua. Umekuwa unajizuia kupata mafanikio unayotaka kwa kusubiri uwe tayari wakati ulivyo umekamilika kabisa kuanza.
Umeshajua unachopaswa kufanya ili kupata matokeo unayotaka, wewe anza kufanya. Hata kama unajiona hujawa tayari, wewe anza kufanya. Vitu vingine utaweza kuvifanya baada ya kuanza kufanya. Kabla ya kuanza kila kitu huwa ni kigumu, ni mpaka unapoanza na ukawa kwenye mwendo ndiyo unaona jinsi vitu vinawezekana.
Vitu unavyoona ni kikwazo kwako kupata unachotaka siyo kikwazo kikubwa kama unavyodhani. Unaona ukubwa wa kikwazo kabla hujaanza kufanya. Ukianza kufanya, hata kama jambo ni gumu, kulifanya kunafungua njia za kulirahisisha na kuwezekana kufanyika.
Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK125; Unajua Cha Kufanya Ili Ufanikiwe, Lakini Umekuwa Unajikwamisha Kwa Sababu Hizi