Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Kuna kauli ukizisikia, unaweza kupata wasiwasi mkubwa, na kuona labda ni mtego, au wewe umekosa umakini wa kutosha.
Moja ya kauli hizo ni kwamba kuna jawabu moja la matatizo yote uliyonayo. Ni kauli nzito, kwamba lipo jawabu la matatizo yote uliyonayo? Na tena mpaka sasa hujalijua jawabu hilo? Ina maana umekuwa unateseka kwa maisha yako yote bila sababu?
Majibu ni ndiyo, lipo jawabu moja la matatizo yako yote, lakini siyo jawabu ambalo hujui. Ukweli ni jawabu hilo unalijua kabisa, lakini umekuwa unachagua kulikwepa na kuhangaika na mengine mengi ambayo hayajaweza kuwa na msaada kwako.
Kama umeshahangaika na mambo mengi ili utatue matatizo uliyonayo na kupata mafanikio makubwa lakini huoni matokeo, ni wakati sasa wa kurudi kwenye jawabu sahihi. Japo ni jawabu ambalo umekuwa unalipuuza, kama umeshahangaika bila matokeo, huna budi bali kurudi kwenye jawabu hilo.
Kwenye hii #BaruaYaKocha unaenda kujikumbusha jawabu hilo na jinsi ya kulitumia kutatua matatizo yote uliyonayo na kupata mafanikio makubwa unayoyataka.

1. Jawabu La Matatizo Yote Uliyonayo.
Rafiki, jawabu la matatizo yako yote ni hili;
‘Fanya kile kinachopaswa kufanywa, wakati kinapopaswa kufanywa, na kifanye kwa namna hiyo kila wakati.’
Rahisi eh? Hukutegemea kwamba matatizo makubwa uliyonayo yanaweza kuwa na jawabu rahisi kama hilo! Nakuelewa kabisa kwenye hilo. Na ndiyo maana nataka tukumbushane hapa ubora wa jawabu hili na jinsi ya kulitumia kutatua matatizo yako na kupata unachotaka.
Kabla hatujaingia kuchambua jawabu hilo kwa kina, lazima tukubaliane kwamba kutatua matatizo uliyonayo na kupata unachotaka, kunaanzia kwenye kufanya. Kikwazo kikubwa kwa watu kimekuwa ni kutokufanya.
Yaani watu wana matatizo, lakini hakuna chochote wanachofanya kuyatatua matatizo hayo. Ambacho wanaweza kufanya ni kulalamika na kulaumu juu ya matatizo hayo wanayokuwa nayo.
Na bado wanashangaa pale matatizo yao yanaendelea kuwepo, licha ya lawama na malalamiko mengi wanayokuwa nayo.
Kadhalika kwenye kutaka mafanikio, wengi wamekuwa wanayataka sana. Wamekuwa wanaeleza jinsi ambavyo wanataka mafanikio makubwa. Wamekuwa wanaweka mipango na malengo ya kupata mafanikio hayo. Lakini, cha kushangaza, hakuna wanachofanya ili kupata wanachotaka.
Kitendo tu cha kuwa tayari kuchukua hatua ya kufanya, kinakuweka tofauti na wengi ambao wamekwama kwenye matatizo waliyonayo au hawapati kile wanachotaka.
2. Fanya Kinachopaswa Kufanyika.
Jawabu la matatizo yote ya maisha yako linaanza na wewe kufanya kinachopaswa kufanyika. Kwa chochote unachopitia kwenye maisha yako, kuna kitu ambacho kinapaswa kufanyika. Kitu hicho unakuwa unakijua kabisa, lakini tatizo limekuwa ni kutokukifanya.
Unazijua tabia ulizonazo ambazo zimekuwa zinakukwamisha kupata mafanikio unayoyataka. Na unajua kabisa kwamba unapaswa kuachana na tabia hizo na kujenga tabia nyingine zilizo bora zaidi.
Matatizo yote ya kifedha uliyonayo unajua nini kinapaswa kufanyika. Unapaswa kuongeza kipato, kudhibiti matumizi na kuweka akiba na kuwekeza. Kwa kufanya hayo, unayatatua matatizo hayo ya kifedha uliyonayo.
Kujenga biashara yenye mafanikio, na inayojiendesha bila kukutegemea unajua kinachopaswa kufanyika. Lazima uwe na thamani ambayo unatoa kwa wengine, upate wateja wanaotaka thamani hiyo, uwashawishi kununua, uwape thamani wanaponunua, ulipwe pesa na uwe na watu wa kufanya hayo yote.
Tunaweza kuona matatizo tuliyonayo ni makubwa na yaliyoshindikana, lakini hakuna tatizo ambalo halina hatua inayopaswa kuchukuliwa. Hata kama hatua hiyo hailitatui tatizo hilo kabisa, bado inakuwa ni bora kuliko mtu kubaki pale ambapo amekuwepo kwa muda mrefu.
Kila unapojikuta kwenye matatizo, changamoto au kutaka kupiga hatua zaidi ya pale unapokuwa, swali la kwanza kujibu ni nini kinachopaswa kufanyika kwenye hali hiyo unayokuwepo. Jua hatua sahihi inayofuata kwenye kuchukua hatua ili kubadili hali uliyonayo sasa na kupata matokeo unayoyataka.
Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK124; Hili Ndiyo Jawabu La Matatizo Yote Uliyonayo