Habari za leo rafiki yangu?

Hongera kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo. Kila unapopata nafasi ya kuiona siku mpya, ni jambo kubwa la kushukuru na kutumia nafasi hiyo vizuri kwa sababu wapo wengi walipanga kuitumia lakini hawajaiona.

Karibu kwenye makala hii ya leo ambapo nakwenda kukukumbusha jambo moja muhimu sana kuhusu maisha yetu ya mafanikio.

Wapo watu ambao wamepitia magumu sana mpaka kuweza kufikia mafanikio. Na kwa hakika, kila mtu kuna ugumu lazima aupitie kabla hajafanikiwa. Mafanikio siyo rahisi, na huwa hayaji kwa wale walioridhika na maisha waliyonayo. Lazima ufike mahali useme imetosha na kuamua kuchukua hatua, ndipo unafanikiwa.

Katika kupitia changamoto hizi za mafanikio, wengi wamenyanyaswa sana. Wapo watu ambao wamepitia mateso na manyanyaso makubwa kutoka kwa watu ambao waliwategemea sana. Manyanyaso hayo yaliwapa hasira kubwa ya kuchukua hatua na kushika hatamu ya maisha yao. Wakapambana kweli mpaka wakafanikiwa.

Lakini sasa wanakuwa wanaendelea kufanya kosa moja kubwa sana kwenye maisha yao, ambalo linawazuia kufurahia mafanikio yao.

Kosa hilo ni kuendelea kuwa na vinyongo kwa wale ambao waliwanyanyasa na kuwatesa. Hivyo hufanya mambo kuwaonesha kwamba na wao sasa wana nafasi, au wakati mwingine hata kutaka kulipa kisasi. Pale inapotokea mtu aliyewanyanyasa anahitaji msaada, wanamkumbusha kwamba waliwanyanyasa na hivyo hawawapi msaada kwa moyo mmoja.

Usomaji

Hili ni kosa kubwa sana rafiki yangu, kama umewahi kulifanya basi leo ni siku ya kuachana nalo mara moja.

Mtu yeyote ambaye aliwahi kukunyanyasa au kukutesa huko nyuma, ukapata hasira na kuamua kupambana kwenye maisha yako ili ufanikiwe, ni mtu ambaye unapaswa kumshukuru sana. Tena kama yupo ambaye unamkumbuka chukua hata simu sasa na mpigie kumwambia asante.

Najua hili linaweza kuwa gumu kwako, hasa kama maumivu aliyokusababishia ni makubwa, lakini ni jambo jema sana kwako unaloweza kufanya kwenye maisha yako.

Huenda ni mzazi alikufukuza nyumbani na kukuambia hataki kukuona tena kwa sababu amekuvumilia na kashindwa. Ukalazimika kwenda kuomba kukaa kwa watu kwa muda na kuanza maisha yako mwenyewe.

Huenda ni mwajiri ambaye alikuwa anakunyanyasa kwenye kazi, au walikuwa hakulipi kwa muda na huenda alikufukuza kazi bila sababu, na hapo ukapata hasira na kuamua kwenda kujiajiri.

Au ni ndugu ambaye ulikuwa unamtegemea wakati huna kazi wala biashara, mwishowe akakuambia hawezi kukusaidia tena na utafute utaratibu mwingine. Huenda mtu alikufukuza kama mbwa na kukudhalilisha sana, hayo yote yakakupa hasira kubwa, huu ni wakati wa kuwashukuru wote hao.

SOMA; Huu Ndiyo Wakati Sahihi Wa Kutua Mizigo Tuliyobeba Kwenye Mioyo Yetu.

Kwa nini nakuambia hili?

Iko hivi rafiki, sisi binadamu ni viumbe wa tabia na mazoea, huwa tuna tabia ya kuzoea mambo haraka halafu kujenga tabia kwenye mazoea hayo. Baada ya kujenga tabia, huwa ni vigumu sana kubadilika kwa kuanzia ndani yetu wenyewe. Unaendelea kufanya kile ulichozoea, na ni vigumu kujaribu vitu vipya, kwa sababu huna uhakika wa matokeo, na kile ulichozoea kufanya tayari kinakupa matokeo fulani.

Hivyo ili kubadilika kutoka kwenye mazoea, kunahitajika nguvu kubwa mbili;

Nguvu ya kwanza ni kutoka ndani yako, kuwa na hamasa kubwa ya kutoka pale ulipo sasa na kufanya makubwa zaidi.

Nguvu ya pili ni kutoka nje, ambapo mazingira yanakulazimisha ubadilike.

Sasa nguvu ya ndani huwa siyo kubwa sana kwa wengi, na hivyo kitu pekee kinachoweza kuwasukuma watu kuchukua hatua ni nguvu ya nje, tena nguvu hiyo iwe kubwa sana, ambayo inaweza kuchochea nguvu ya ndani nayo kukazana kupata mabadiliko.

Na hapo ndipo manyanyaso na mateso yanapofanya kazi. Yanakusukuma kubadilika kwa nje, kufukuzwa nyumbani, kufukuzwa kazi, kunyimwa chakula, yote hayo yanakulazimisha uangalie njia mbadala. Lakini pia yanachochea nguvu ya ndani ya kutaka kubadilika, hapo unapata hasira, kudhalilika na kuamua kwamba umechoka na aina hiyo ya maisha ya mateso na manyanyaso.

Hali hii inakufanya uone huna namna nyingine zaidi ya kuchukua hatua, na unapochukua hatua, hutakuwa na hofu ya kushindwa, kwa sababu unajua ni bora ujaribu ushindwe kuliko usijaribu kabisa.

Unapokuwa huna pa kula wala kulala, ukiitiwa kazi yoyote utafanya, wala hutasema kwamba hiyo siyo hadhi yako. Lakini kama upo nyumbani, au kwa ndugu, ambapo unakula na kulala vizuri, iwe unafanya kazi au la, utakuwa mtu wa kuchagua sana kazi, kwa sababu huna cha kukusukuma kuchukua hatua. Sijui unaanza kuipata picha rafiki?

Hivyo kaa chini na tafakari kwa kina, angalia watu wote ambao wamewahi kukunyanyasa, kukutesa au hata kukunyima kitu ambacho ulikitaka sana. Angalia hamasa uliyoipata baada ya tukio lile, na hatua kubwa ulizoweza kuchukua kwenye maisha yako. Ona kama huna sababu ya kushukuru kwenye hilo.

Unaweza kufikiria lakini asingeninyanyasa au kunitesa, ningefanikiwa zaidi ya nilivyofanikiwa sasa. Huo ni uongo. Na ukitaka kudhibitisha mwenyewe, angalia wale waliokuwa kwenye hali kama zako lakini hawakunyanyaswa wala kuteswa.

Kama ulifukuzwa kazi kwa uonevu na kuamua kwenda kujiajiri, angalia wale wenzako ambao uliwaacha kazini, utashangaa wanaokuonea wivu kabisa. Yaani wewe unakuwa umepiga hatua kuliko wao.

Kama ulifukuzwa nyumbani, angalia wenzako ambao waliendelea kukaa nyumbani, utakuta wewe umepiga hatua kubwa kuliko wao. Tena wengine wanaweza kuwa wazembe zaidi kuliko wewe.

Hii ndiyo sababu nakutaka leo rafiki yangu, kama yupo yeyote ambaye amewahi kukunyanyasa au kukutesa kwenye maisha yako, mshukuru sana. Huyu amekusaidia wewe kuchukua hatua muhimu kwenye maisha yako, ambapo bila yeye huenda usingepata hamasa ya kutosha ya kuchukua hatua hizo.

Na kama una kinyongo chochote na watu wa aina hiyo, wasamehe mara moja.

Maisha yangu binafsi nimekuwa napiga hatua kutokana na manyanyaso na hata kukataliwa. Nimeweza kufanya mambo mengi makubwa baada ya kukosa namna au kukataliwa kitu ambacho nilikuwa nahitaji sana.

Kila jambo ambalo nimeweza kufanya kwenye maisha yangu, kuna mchango wa wengine katika kuninyima kitu au kuninyanyasa kwenye kitu fulani. Hivyo mara zote huwa nawashukuru sana watu hao.

Kama nisingefukuzwa chuo kikuu mwaka 2011, leo hii wewe usingenijua, ningekuwa ni daktari sehemu fulani huko ambaye anatibu wagonjwa wake na kusubiri mshahara uingie na maisha yaendelee. Lakini baada ya kufukuzwa, nililazimika kuchukua hatua ambazo huenda nisingekuja kuzichukua iwapo mambo yangeenda bila ya msukosuko. Na mara zote huwa nashukuru sana tukio lile la kufukuzwa, kwa sababu limeniwezesha kuingia ndani zaidi na kujua kumbe ndani yangu kuna mengi na makubwa kuliko niliyokuwa nimefundishwa miaka yote ambayo nimekuwa kwenye mfumo wa elimu.

Hivyo rafiki, shukuru kila mtu na kila tukio ambalo limewahi kutokea kwenye maisha yako. Lina mchango mkubwa kwa hapo ulipo sasa.

SOMA; Chanzo Kikuu Cha Maumivu Ya Ndani Tunayopitia Kwenye Maisha Yetu.

Kwa upande wa pili, kama baada ya kunyanyaswa au kuteswa ulikata tamaa na maisha yako yakawa mabovu zaidi, amka sasa na chukua hatua ya maisha yako. Usiendelee kuwalaumu na kulalamika kwamba wengine wamekuharibia maisha, hakuna wa kukuharibia maisha yako ila wewe mwenyewe.

Pia kama kuna mtu anakunyanyasa au kukutesa sasa, usikubali kuwa mwenye hatia, badala yake chagua kuchukua hatua, chagua kushika hatamu ya maisha yako, kutokuruhusu mtu aweze kukufanyia vile atakavyo. Fanya hivyo siyo kwa hasira juu yake au kutaka kumwonesha kwamba na wewe unaweza, bali kama njia ya kujenga maisha yako kuwa imara zaidi.

Mambo yakienda vizuri, sisi binadamu tuna tabia ya kuzoea na kujisahau, tunahitaji manyanyaso, mateso na kukataliwa mara kwa mara ili tukumbuke kuchukua hatua na kuwa huru zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog