Rafiki yangu mpendwa,

Karibu tena kwenye makala yetu ya ushauri wa changamoto ambapo tunapeana hatua za kuchukua kulingana na changamoto mbalimbali ambazo tunapitia kwenye maisha yetu.

Changamoto ni sehemu ya maisha, na hivyo dawa yake ni kuzitatua na siyo kukubali zituzuie au kuzitumia kama sababu ya kutokupiga hatua zaidi. Ukikubali changamoto ikuzuie maana yake unakuwa hujajitoa kweli kufanikiwa. Kwa sababu hutaweza kuziondoa kabisa changamoto kwenye safari yako ya mafanikio.

Leo tunakwenda kuangalia changamoto mbili kubwa ambazo zinawasumbua wengi. Changamoto hizo ni pale mtu anaposhindwa kutekeleza mipango yake kutokana na changamoto za kifedha na pia kushindwa kuwekeza kwa sababu ya kuwa mbali na nyumbani.

NUFAIKA NA MABADILIKO

Karibu kwenye makala hii tujifunze hatua sahihi za kuchukua ili kuweze kufikia mipango yetu. Kabla hatujaendelea tupate kwanza maoni ya msomaji mwenzetu aliyetuandikia kuomba ushauri kwenye hili;

‘Changamoto yangu ni kuwa, (1) nafanya kazi Serikalini na nikipata mshahara huku nikiwa nimepangilia mipango yangu ya matumizi ili kutimiza malengo yangu, lazima itokee tukio katikati ambalo linahitaji fedha na hivyo husababisha mimi kutoa kiasi cha fedha kwa ajili ya tukio hilo jambo ambalo hunifanya kushindwa kufanya lile nililolikusudia. (2) Sipati kabisa hata muda kufanya mambo muhimu ya uwekezaji maana nipo mbali na nyumbani na nikituma hela wafanye shughuli ambayo naikusudia nakuta haijafanyika kama nilivyokusudia.’ – Ormaoi L. M.

Changamoto ya fedha.

Wanasema kwamba fedha huwa haikosi matumizi, kwamba kila unapokuwa na fedha, matumizi yatakuwa yanajitokeza, hata ambayo utakuwa hujapangilia. Na hii ndiyo inapelekea hiyo hali ya kuwa na mipango mizuri ya kifedha, lakini unapozipata unashangaa zinatokea changamoto zinazohitaji fedha, unatumia fedha hiyo kwa changamoto na mipango yako inasimama.

Usipokuwa makini na kustuka haraka, utajikuta unahangaika na kila changamoto inayojitokeza, lakini hupigi hatua kwenye mipango yako. Kwa sababu changamoto za fedha hazitaisha, kila unapopata fedha kuna changamoto mpya zitakazoibuka.

Njia pekee ya kuzuia changamoto hizi za kifedha zisiharibu mipango yako ni kutengeneza gereza la fedha zako.

Iko hivi rafiki, unazitumia fedha ka changamoto mbalimbali kwa sababu unazo. Iwapo changamoto itatokea ukiwa huna fedha kabisa, haimaanishi kwamba utakufa, bali maisha yataendelea. Sasa hii ndiyo dhana unayohitaji kuitumia ili kuepuka changamoto zinazotokea zisizuie mipango yako.

Unachohitaji kufanya ni kuwa na akaunti maalumu ambayo unaweza tu kuweka fedha lakini huwezi kuzitoa kwa kipindi fulani. Benki nyingi zina akaunti za aina hii. Hivyo mshahara unapoingia kwenye akaunti yako, unahamisha sehemu ya mshahara huo uliyoitenga kama akiba na kuweka kwenye akaunti hiyo maalumu.

Ukishahamisha fedha hizo, unakuwa umeziweka kwenye gereza, hivyo huwezi kuzipata hata kama ni nini kitatokea. Utatumia ile iliyobaki kwa matumizi yako na changamoto zitakazojitokeza, ikiisha basi itabidi uendeshe maisha yako kwa namna nyingine unayoweza. Lakini ile fedha yako ya akiba inakuwa ipo salama kwenye gereza ulilotengeneza.

Ukifanyia kazi hili, utashangaa changamoto nyingi zilizokuwa zinahitaji fedha zako huzioni tena, kwa sababu unakuwa huna fedha na hivyo hujisumbui na vitu ambavyo huwezi kuviathiri.

Chukua hatua leo ya kutengeneza gereza la fedha zako na utapunguza changamoto zinazokufanya utumie fedha unazokuwa umeziwekea mipango mizuri ya baadaye. Fungua akaunti maalumu kwenye benki ile ile unayopokelea mshahara na unaweza kuwaambia wakafanya zoezi hili wao wenyewe pale mshahara unapoingia wanakata kiasi fulani na kuweka kwenye akaunti hiyo maalumu.

Bila ya kuwa na gereza la fedha zako, itakuwa vigumu sana kwako kupiga hatua kubwa, kwa sababu wengi hawana nidhamu ya kuweza kukaa na fedha na wakawa na utulivu. Wengi wanapokuwa na fedha akili haiwezi kutulia mpaka wahakikishe wamemaliza kutumia fedha hiyo.

SOMA; Vitu Hivi Vitatu Usivyovijua Kuhusu Fedha Ndiyo Vinakuzuia Wewe Kufika Kwenye Utajiri Na Uhuru Wa Kifedha.

Changamoto ya uwekezaji ukiwa mbali.

Ni kweli kabisa kwamba kuna changamoto kubwa kufanya uwekezaji pale unapokuwa mbali na nyumbani. Hasa kama utatumia utaratibu wa kutuma fedha ili watu wafanye vitu fulani, siku unafika unakuta hakuna kilichofanyika na utapewa sababu ya kila aina.

Hivyo kujaribu kuwekeza ukiwa mbali na nyumbani, huku ukiwatumia ndugu, utakuwa unatafuta ugomvi na ndugu zako hao. Maana nao wana changamoto ya kukaa na fedha, wakiwa nazo na wakapata changamoto watajikita wanazitumia tofauti na mipango uliyoweka.

Njia ya kutatua hili ni kutumia gereza kama nilivyoshauri hapo juu, unaweza kuweka fedha zako kwenye gereza hilo na kuzikusanya kwa ajili ya uwekezaji pia. Hivyo unapopata muda wa kwenda nyumbani, unakwenda kusimamia mwenyewe ule uwekezaji ambao unaufanya huko nyumbani.

Kitu kingine unachoweza kufanya ni kuwekeza kwenye masoko ya kifedha, ambayo hayajali upo wapi. Unaweza kuwekeza kwa kununua hisa, kununua vipande na fedha zako zikaweza kukua kadiri muda unavyokwenda. Kujifunza zaidi kuhusu uwekezaji kwenye masoko ya kifedha soma hapa; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kutajirika Kwa Kuanza Na Shilingi Elfu Moja.

Pia unaweza kuwekeza kwenye vitu ambavyo ni rahisi kuvifuatilia kama kununua mashamba na viwanja. Hii itakuwezesha kuweka fedha zako na kuepuka kuzitumia vibaya.

Kitu muhimu kabisa cha kufanya kuhusu kuwekeza fedha zako ni kuhakikisha una biashara inayotumia fedha zako kuzalisha faida zaidi. Na biashara hiyo iwe pale ulipo na siyo mbali. Kazana kwa namna unavyoweza uhakikishe unakuwa na biashara unayoiendesha kwa pale ulipo. Hii itakuwezesha kutumia vizuri fedha zako na kuzizalisha zaidi.

Kwa vyovyote unavyochagua kuiwekeza fedha yako, hakikisha inakuwa salama na pia inaongezeka thamani. Ondoa vishawishi vya wewe au wengine kutumia fedha uliyopanga kwa ajili ya uwekezaji.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Usomaji