Watu wengi waliiona mbali waliwatahadharisha watu kuhusu usalama wa ajira lakini watu kutokana na kulewa ama kuwa watumwa wa ajira hawakuelewa kabisa. Hivi sasa kila mtu anajionea mwenyewe ni jinsi gani ajira zimekuwa sio salama. Ajira zimekuwa chache na ngumu kupatikana na pia zimekuwa rahisi sana kupotea. Ni jambo la kawaida sana kusikia kampuni ama shirika linapunguza wafanyakazi.

acha kazi3

  Pamoja na usalama wa ajira kuwa mdogo, ajira pia zimewasababishia watu wengi sana msongo wa mawazo. Inasemekana chanzo kikubwa cha msongo wa mawazo kinaanza na matatizo yanayotokana na kazi mtu anayofanya. Sehemu za kazi zimekuwa sio za kufurahia sana kama ilivyokuwa zamani. Na wafanyakazi hawana morali kubwa ya kufanya kazi.

  Kutokana na matatizo mengi yatokanayo na ajira watu wengi wanaona ni bora kujiajiri ama kufanya biashara. Karibu kila mfanyakazi wa ngazi ya chini kwenye kampuni ama shirika lolote ana mawazo hayo, hata wewe una mawazo hayo mazuri.

acha kazi

  Ila pamoja na kuwa na mawazo haya mazuri bado ni wachache sana wanaoweza kuondoka kwenye ajira na kuthubutu kujiajiri ama kufanya biashara. Wengi wameishia kupanga mipango ya kuondoka kwenye ajira kila mwaka ila unapofika wakati wa kutekeleza inawawia vigumu kufanya hivyo.

  Kuna uwezekano mkubwa wewe ni mmoja wa wanaosema kila siku “naachana na kazi na kufanya mambo yangu” ila mpaka sasa ni zaidi ya miaka mitano hujafanya hivyo. Unaweza kujipa sababu nyingi za kushindwa kuondoka kwenye ajira ila sababu hizo sio za msingi.

   Sababu kuu inayokufanya kila unapotaka kuondoka kwenye ajira unashindwa ni kutokuwa na uhakika wa kipato.

  Unapokuwa umeajiriwa una uhakika kila mwisho wa mwezi utalipwa mshahara wako. Hata kama utachelewa ila bado uhakika wa kuupata ni mkubwa. Japo mshahara huo unaweza kuwa kidogo na haukutoshi ule uhakika tu kwamba lazima utakuwepo unakupa amani ya kuendelea na ajira.

  Unapokuwa umejiajiri ama unafanya biashara na hasa wakati wa mwanzoni huna uhakika wowote wa kupata kiasi fulani cha fedha kila mwisho wa mwezi au angalau kila siku. Kuna kipindi unaweza kupata fedha nyingi na kuna kipindi hupati hata shilingi.

  Kwa kuwa nidhamu yetu ya matumizi ya hela iko chini sana tunajikuta katika hali mgumu sana nyakati kama hizo.(soma; tatizo sio fedha, tatizo ni wewe)

  Unapowaangalia waliojiajiri wanapopitia nyakati hizo unaogopa sana kuingia kwenye mrengo huo na kujipa moyo kwamba hata kama unapata kidogo una afadhali kwa sababu una uhakika wa kukipata.

  Ili kweli uweze kuondoka kwenye ajira na ufanikiwe kwenye ulimwengu wa kujiajiri na biashara unahitaji maandalizi mazuri ya kimwili, kifedha na kiakili.(soma; kama una tabia hii zibadili kabla hujajiajiri) Jua kwamba kutakuwa na nyakati ngumu sana, ila hautakuwa mwisho wa dunia. Kama kweli utakuwa umedhamiria na umejipanga vizuri kuhusu kujiajiri ama kufanya biashara hakuna linaloweza kukuzuia kupata mafanikio.