Habari za leo msomaji wa AMKA MTANZANIA, naamini unaendelea vizuri na harakati za kuboresha maisha yako. Na hata kama kuna changamoto unazipitia usivunjike moyo kwani ndivyo maisha yalivyo na pia changamoto ndio njia ya kujifunza.

Karibu tena kwenye kipengele chetu cha ushauri kwa changamoto mbalimbali. Leo tutaangalia changamoto ya kushindwa kuanzisha biashara kutokana na kipato kidogo.

Watu wengi sana wanapenda siku moja wamiliki biashara zao kubwa ila changamoto kubwa inakuja wapate wapi mitaji? Kwa sababu wengi wao huenda hawana chanzo chochote cha fedha au wana kipato kidogo sana ambacho hakitoshelezi hata mahitaji yao.

Leo tutajadili wanaotaka kuanzisha biashara ila wana kipato kidogo, kwa ambao hawana kipato kabisa tutajadili siku nyingine kwa sababu hapo ni papana zaidi.

KUZA KIPATO

Kabla hatujajadili nini cha kufanya tuone ujumbe tulioandikiwa na m

wasomaji wenzetu walio omba ushauri;

Mimi ni fundi ujenzi changamoto yangu ni kwamba nashindwa kufikia malengo ya kuanzisha biashara kwa kuwa kazi nayoifanya hainilipi

KIPATO CHANGU NI KIDOGO NA NINA NIA YA KUFAIKIA MALENGO LAKINI INASHINDIKANA

Inawezekana na wewe ni mmoja wa watu ambao wanatamani sana kuanzisha biashara ila kipato chako ni kidogo. Leo tutajadili ni jinsi gani unaweza kukabiliana na changamoto hii.

Kuna mambo matatu muhimu ya kufanya kama unataka kuanzisha biashara ila kipato chako ni kidogo.

1. Jua ni biashara gani unataka kufanya na jua ni mtaji kiasi gani unahitaji.

Watu wengi wanaweza kukupa sababu kwamba kinachowazuia kuanzisha biashara ni mtaji. Cha kushangaza unapomuuliza ni mtaji kiasi gani anataka anaweza akakuambia hana uhakika au akakuambia ni kiasi fulani, ukimuuliza anaupangiliaje huo mtaji anabaki bila ya majibu. Ni muhimu sana kujua biashara ambayo wewe unataka kuifanya na ni vyema kama itakuwa kitu ambacho unapendelea kukifanya. Baada ya kuijua biashara hiyo vizuri jua utaifanyia wapi na utahitaji mtaji kiasi gani ili kuanza. Kujua gharama hizo ni lazima ufanye utafiti kidogo kwa kuuliza wengine wanaofanya biashara hiyo na kuulizia gharama za vitu unavyohitaji kwenye biashara hiyo.

Mpango huu mzima wa biashara yako unatakiwa kuwa kichwani kwako kila siku na kila mara hii itakusaidia kuweza kuona fursa zaidi za kuweza kuanzisha biashara hiyo. Ila kama mpango huo haupo kichwani kwako kila mara utaendelea kulalamika kila siku na hutaona mabadiliko yoyote.

2. Anza kuchambua mawazo yako kuhusu kuanza biashara hiyo.

Baada ya kujua ni biashara gani unafanya, unafanyia wapi na utahitaji kiasi gani cha fedha, anza kuwaza ni jinsi gani unaanza. Kwanza kabisa unapowaza ondoa mawazo hasi kwenye kichwa chako, usijiambie kwamba mtaji ndio kikwazo, waza kwamba unahitaji mtaji je utaupataje? Angalia ni jinsi gani unaweza kuanza kidogo na baadae ukakua kufikia malengo uliyojiwekea. Angalia ni vitu gani ulivyonavyo sasa ambavyo vinaweza kukusaidia kwenye biashara hiyo bila ya gharama kubwa. Inawezekana unajuana na watu wengine wanaofanya biashara kama hiyo kwa kiwango kikubwa, inawezekana kuna vipaji unavyo ambavyo unaweza kuvitumia kwenye biashara yako na ikaongeza kipato.

Katika wakati huu jipe muda wa kufikiria kwa kina kila sehemu ya biashara yako, lengo ikiwa kuondoa mawazo hasi kwamba haiwezekani na jinsi gani ya kuanza kidogo na baadae kukua.

3. Fanyia kazi kipato chako.

Unaposema kipato chako ni kidogo kuna mambo mengi ambayo bado hujayafanya.

Kwanza kuwa tu na kipato tayari inaonesha kuna kitu unaweza kukifanya na watu wakakulipa, kama ilivyo kwa mwenzetu ambaye ni fundi ujenzi. Hivyo cha kufanya hapo kwenye kipato chako ni kuangalia jinsi gani ya kuweza kukiongeza. Usiseme umeshindwa kukiongeza, unaweza sana kwa sababu tayari mpaka sasa una kipato. Hivyo anga;ia unawezaje kukiongeza, inawezekana kwa kufanya kazi muda mrefu zaidi, au kwa kufanya kazi nyingi zaidi au kwa kutafuta mbinu za watu wengi zaidi kujua kile unachofanya zaidi.

Baada ya kufikiria jinsi ya kuongeza kipato chako angalia ni jinsi gani unaweza kupunguza matumizi yako. Unaweza kuwa unalalamika kipato chako ni kidogo na wakati huo huo huwezi kulala bila ya kunywa hata bia moja, au kuna matumizi mengine ambayo siyo ya msingi ila yanaingia kwenye kipato chako.

Sikiliza, kuanza biashara sio kitu rahisi pale ambapo una kipato kidogo, kuna vitu vingi sana ambavyo utahitaji kutoa kafara ndio uweze kusonga mbele. Kwa wakati huu ambao unataka kuanza biashara kwenye kipato chako kidogo matumizi yoyote ambayo kama usipoyafanya huwezi kufa basi achana nayo. Hii ina maana matumizi yako ya fedha yaende kwenye maeneo muhimu tu yako na ya familia yako. Vitu kama nguo, vinywaji na starehe vinaweza kusubiri.

Kwa haya machache unaweza kuona itakuwa rahisi kidogo kuanza biashara kuliko unapokuwa hujui kabisa ni nini unataka na unapokuwa na mtazamo hasi kwamba wewe huwezi kwa sababu umekosa kitu fulani.

Kwa ushauri zaidi juu ya kutunza fedha na kuweza kuanzisha na kukuza biashara yako tembelea na jiunge na KISIMA CHA MAARIFA kwa kubonyeza hayo maneno.

Nakutakia kila la kheri katika harakati za kutafuta uhuru wa maisha yako.

TUKO PAMOJA.

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja makala zijazo kila siku ya jumatatu. Kama unahitaji ushauri wa haraka wasiliana na mimi kwa kwa email amakirita@gmail.com au simu 0717396253/0755953887.