Hiki Ndio Kikwazo Kikubwa Kinachokuzuia Wewe Kufikia Uhuru Wa Kifedha.

Linapokuja swala la fedha kila mtu anahusika. Yaani kwenye fedha ndio tunaweza kuzungumza lugha moja iwe mkubwa au mdogo, mwanaume au mwanamke. Fedha ina nafasi kubwa sana kwenye maisha yetu kwa sababu mahitaji yote muhimu kwenye maisha yetu tunayapata kwa gharama ya fedha.

100_7560 ED1

Pamoja na umuhimu huu mkubwa wa fedha bado kuna watu wengi kwa maneno wanabeza umuhimu huu wa fedha ila kwa matendo wanauonesha kwenye kila wanachofanya. Leo hatutazungumzia hilo, bali tutazungumzia kitu kimoja kinachokuzuia wewe kufikia uhuru wa kifedha.

Kwanza kabisa UHURU WA KIFEDHA ni nini?

Uhuru wa kifedha ni pale ambapo mtu anakuwa na fedha za kutosheleza mahitaji yake bila ya kufanya kazi kwa ajili ya mahitaji hayo. Yaani hata kama hutofanya kazi moja kwa moja una uwezo wa kuendesha maisha yako kwa kiwango ulichojipangia.

Hii ina maana vyanzo vyako vya mapato vinatokana na mali zinazozalisha fedha bila ya wewe kufanya kazi moja kwa moja.

Kama bado unafanya kazi ili upate fedha ya matumizi bado hujapata uhuru wa kifedha. Bado unaendelea kuzikimbiza fedha ili uweze kuendelea kuishi. Hivyo endelea kusoma hapa ujue ni kitu gani kinaendelea kukufanya ushindwe kufikia uhuru wa kifedha.

Sababu moja kubwa sana inayokufanya mpaka sasa na huenda miaka mingi ijayo hutafikia uhuru wa kifedha ni kutokuwa na imani. Yaani huamini kama unaweza kufikia uhuru wa kifedha.

Kila unapovuta picha kwamba unaweza kuwa umetengeneza fedha na mali za kuzalisha fedha kiasi kwamba huna haja ya kufanya tena kazi ndio uendelee kuishi, huamini kabisa kama inawezekana. Unaamini kazi uliyonayo ndio uliyopangiwa na hivyo utaifanya kwa miaka ishirini ijayo kwa shida shida ili baadae upate mafao ambayo nayo hayatakupatia uhuru wa kifedha. Unaamini biashara ndogo unayofanya haiwezi kuwa kubwa kiasi cha wewe kuwa msimamizi tu wa juu na hivyo kuendelea hivyo hivyo kwa miaka mingi sasa.

Ni madhara gani yanatokana na wewe kutoamini unaweza kupata uhuru wa kifedha?

Kuna madhara mengi sana yanayotokea pale unapoamini huwezi kufikia uhuru wa kifedha. Na haya ndio yanasababisha uendelee kuwa hivyo ulivyo.

Kwa kuamini kwamba huwezi kufikia uhuru wa kifedha;

Huchukui hatua yoyote ya kusoma vitabu vinavyoelezea kuhusu matumizi na usimamizi wa fedha binafsi.

Huchukui mafunzo yoyote yanayotolewa ili kujiendeleza kitaaluma au kibiashara na uweze kuwa bora zaidi.

Huhudhurii semina mbalimbali zinazotolewa juu ya mafanikio na maendeleo binafsi.

Hivyo umeendelea kuwa kwenye shimo hilo la kukimbiza fedha ndio uweze kuishi na huenda ukikutana na kitabu, semina au mafunzo yanayoweza kukutoa kwenye shimo hilo unabeza kwa kusema hayana msaada wowote kwako.

Unaendelea na maisha yako magumu huku ukiendelea kulalamika kila siku na kuona wenye uhuru wa kifedha kama wana bahati sana au wamefanya hila kufikia walipofikia.

Hata wewe unaweza kufikia uhuru wa kifedha. Ila ni muhimu kuondoa imani hiyo kwanza ndio uweze kufikia uhuru huu. Vinginevyo utafanya kazi sana, utahangaika na biashara sana lakini kila siku fedha itakuwa msamiati mgumu kwako.

Soma vitabu vinavyoelezea kuhusu mambo ya fedha na maendeleo, tembelea mitandao inayozungumzia mambo haya(kama AMKA MTANZANIA), hudhuria semina zinazofundisha mambo haya na kama ikiwezekana hudhuria mafunzo ya kuboresha taaluma yako au biashara zako.

Kwa wale ambao bado hawajapata vitabu vitatu ninavyotuma(think and grow rich, the richest man in babylon na rich dad poor dad) nitumie email kwenye amakirita@gmail.com Ukivipata vitabu hivi visome na utumie yale unayojifunza kwenye maisha yako.

Pia kwa wale wanaopenda kujifunza zaidi kuhusu kujenga tabia nzuri za kifedha ingia KISIMA CHA MAARIFA na ujiunge ili uweze kujifunza zaidi na ufikie uhuru wa kifedha. Kwenye kisima cha maarifa utapata mafunzo yatakayokuwezesha kufikia uhuru wa kifedha kama utayatumia kwenye maisha yako.

Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya kufikia uhuru wa kifedha.

TUKO PAMOJA.

 

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: