Tunaendelea na uchambuzi wa kitabu RICH DAD POOR DAD.
Leo tutajifunza hatua kumi za kufuata ili kuanza safari yako ya kufikia uhuru wa kifedha.
1. Hatua ya kwanza; Sababu kubwa kuliko uhalisia.
Watu wengi wanapenda kufikia uhuru wa kifedha, ila uhalisia unawazuia kufikia malengo hayo. Hii inatokana na kwamba safari hiyo ni ndefu na ngumu. Kutokana na ugumu huu watu wengi wanaona ni vyema kuajiriwa na kupata fedha ambayo ni ya uhakika. Robert anasema ni lazima uwe na sababu ambayo ni kubwa kuliko uhalisia. Na sababu hii itatokana na vitu ambavyo unavitaka na vile ambavyo huvitaki. Kwa mfano Robert anasema hataki kufanya kazi maisha yake yote, hataki yale wazazi wake wamemdanganya kuwa apate kazi nzuri na pia hataki kuwa muwajiriwa. Pia Robert anasema anataka kuwa huru kusafiri duniani na kufanya yale anayofurahia, anapenda kufanya hayo akiwa bado kijana, anataka kuwa huru, anataka kuwa na uhuru juu ya muda wake na amaisha yake na anataka fedha imfanyie yeye kazi. Robert anakuuliza ni vipi ambavyo hutaki na vipi ambavyo unavitaka?
2. Hatua ya pili; Nguvu ya kuchagua.
Robert anasema hatua ya pili ya kufikia uhuru wa kifedha ni kuwa na nguvu ya kuchagua. Anasema kila fedha inayoingia kwenye mkono wako unaweza kuchagua kuwa tajiri au kuwa masikini. Anasema kwa kuwa safari ya utajiri ni ngumu watu wengi huchagua kutumia fedha zao vibaya na hivyo kushindwa kufikia uhuru wa kifedha. Robert anasema pia lazima mtu uwe na nguvu ya kuchagua ni jinsi gani unatumia muda wako. Anashauri hata kama huna fedha basi chagua kutumia muda wako kujifunza zaidi. Hakikisha kila unalochagua linakusogeza kwenye uhuru wa kifedha.
3. Hatua ya tatu; Chagua marafiki kwa umakini.
Robert anasema hachagua marafiki kwa kuwa ni matajiri au masikini, ana marafiki wengi na wenye hali tofauti za kiuchumi. Anasema anajifunza kutoka kwa kila rafiki yake. Anasema marafiki zake wenye fedha wanazungumzia kuhusu fedha na anajifunza mengi kutoka kwao. Na marafiki zake ambao hawana fedha hawapendi kuzungumzia fedha ua biashara na hivyo anajifunza ni mambo gani asifanye kupitia wao.
4. Hatua ya nne; Ijue kanuni na jifunze nyingine.
Ili kutengeneza mkate kila mpishi anafuata kanuni, ndivyo ilivyo kwenye fedha. Robert anasema linapokuja swala la fedha, watu wana kanuni moja waliyofundishwa shuleni; FANYA KAZI NDIO ULIPWE FEDHA. Robert anasema kanuni moja anayoiona kwa watu wengi ni kuamka asubuhi, kwenda kazini, kupata mshahara, kulipa madeni na kurudia tena hivyo mpaka wanapostaafu. Robert anasema kama umechoka kanuni hii kikubwa cha kufanya ni wewe kubadili kanuni yako ya kutengeneza fedha. Robert anasema akiwa na miaka 26 alijiunga na darasa la kujifunza jinsi ya kununua nyumba za biashara, na ilimsaidia sana. Baada ya kuijua hiyo vizuri alitafuta kanuni nyingine ya kujifunza.
5. Hatua ya tano; Jilipe wewe kwanza, nguvu ya nidhamu binafsi.
Kama huwezi kujidhibiti mwenyewe, usijaribu kuwa tajiri. Ukosefu wa nidhamu binafsi ndio unaowafanya watu wengi wanaoshinda bahati na sibu kuishiwa baada ya muda mfupi. Ni ukosefu wa nidhamu binafsi unaowafanya watu wanaoongezewa mshahara kuongeza matumizi zaidi na hivyo kuendelea kuwa na maisha magumu.
Robert anasema katika hatua zote kumi hii ndio hatua ngumu sana kwa watu wengi kuweza kuifuata. Robert anasema kinachowatofautisha matajiri na masikini ni nidhamu bianfsi. Robert anasema anasisitiza sana kwamba ni muhimu kujilipa wewe kwanza. Anasema alijifunza hili kwenye kitabu cha THE RICHEST MAN IN BABYLON. Anasema wengi wamekisoma kitabu hiki ila hawatimizi usemi huo.
Robert anasema ni muhimu kujilipa wewe kwanza na ndio uendelee kulipa madeni na bili zako. Na ili kujilipa mwenyewe punguza matumizi yasiyo ya msingi na wekeza kwenye mali zinazozalisha. Kama una kipato kidogo ambacho hakikuwezeshi kujilipa kwanza fikiria mbinu za kutengeneza kipato zaidi kupitia uwekezaji wako.
6. Hatua ya sita; Walipe madalali vizuri.
Robert anasema ni vyema kumlipa kila mtu mwenye taaluma yake vizuri. Anasema madalali mbalimbali anaofanya nao biashara ni muhimu sana kwani wanamwezesha kupata taarifa sahihi za biashara na uwekezaji.
7. Hatua ya saba; Kuwa mtoaji wa kihindi.
Robert anasema hii ni njia ya kupata kitu bila ya kuwa na kitu. Anatoa mfano wa walowezi walioenda marekani kipindi cha ukoloni na kukutana na wahindi wa marekani. Anasema wakati wa baridi wahindi waliwapa walowezi wale mablanketi, ila walipotaka kurudishiwa walowezi wale walikataa kuwarudishia. Kwenye ulimwengu wa kuwekeza kwenye ASSETS, Robert anasema ni lazima uweze kutoa fedha kwenye uwekezaji ambao hauna uhakika sana ili baadae uweze kupata faida. Anasema unaweza kukuta kampuni ni ndogo na hivyo hisa zake sio ghali sana, kama kampuni ni nzuri, unaweza kuwekeza mwanzoni kwa urahisi na baadae ukawa kwenye nafasi nzuri ya kutengeneza faida kubwa.
Tutaendelea na hatua zilizobakia kwenye makala ya kesho.
Kumbuka keshi ndio tunafikia mwisho wa kitabu hiki, na baada ya hapo tutaanza ushambuzi wa kitabu THE RICHEST MAN IN BABYLON.
Nakutakia kila la kheri katika kufikia mafanikio makubwa.
TUKO PAMOJA.
Ahsante Ubarikiwe
LikeLike
Asante na karibu sana,
TUKO PAMOJA.
LikeLike