Daima namshukuru Mungu kwa namna ambavyo amekuwa akinipa pumzi pasipo malipo, asante Mungu uliye msanifu wa maumbile yetu, mambo yote yatapita lakini ufalme wako utadumu milele. Lengo la makala hii ni kukuwezesha kutambua makosa ambayo watu wengi wameyafanya na wengine wanaendelea kufanya kwa kujua au kwa kutokujua, hali hii huwafanya washindwe kufurahia maisha kama wengine.



Kuamini Kuwa Haupo tayari kuwekeza Kwa Sasa
Wakati wa kufanya maamuzi na kutenda ni sasa, baadae tutarajie matokeo ya tulichowekeza, uwekezaji wa majengo hauna tofauti sana na uwekezaji wa aina nyingine katika uchumi, kwa sasa zimejitokeza fursa nyingi sana za watu kuwekeza kwenye majengo lakini ni watu wachache sana wanaozitumia fursa hizo huku wengine wakiamini kuwa hadi watakapopata fedha nyingi kwa wakati mmoja ndipo watakapofanya maamuzi ya kujenga, Anza safari kwa kiasi ulichonacho kwa kuwa kitakusogeza hatua Fulani na utakuwa umepunguza gharama kwa kiasi Fulani, Nimekutana na watanzania wengi ambao hutamani kuwa watu wenye mafanikio ya aina Fulani lakini unapowaambia ili ufanikiwe lazima ujitoe kwa jambo Fulani, hutafuta sababu nyingi za kushindwa na hatimaye huishia kusema nitakapokuwa tayari nitafanya hivyo. Hali hii ni hatari sana na kamwe tusi iruhusu itawale nafsi na akili zetu.
SOMA; AUDIO BOOKS; Vitabu Kumi Na Mbili(12) Vitakavyobadili Maisha Yako Kabisa Na Kukuletea Mafanikio Na Furaha.
Kuamini Kuwa Utafanikiwa Pasipo Kutumia Wataalamu
Kwenye maisha ya mafanikio nimejifunza kuwa huwezi kufanikiwa ukiwa wewe kama wewe. Ni lazima upate ushirika kutoka kwa watu wengine. Hii ni kutokana na wewe kutojua kila kitu. Ulimwengu wa sasa ili ufanikiwe unahitaji taarifa sahihi za jambo husika ili uweze kufahamu vema kama litakuletea manufaa au la. Pia taarifa sahihi zitakuwezesha kufanya jambo kwa ufanisi zaidi na kuweza kufikia lengo kwa uhakika zaidi. Taarifa sahihi hupatikana kwa watu sahihi, watu sahihi ni watu wenye uelewa wa juu na uzoefu wa jambo au fani Fulani. Ili ufanikiwe hakikisha unatengeneza mtandao wa watu sahihi watakao kusaidia kufikia lengo. Mfano, ofisi yetu inahusika na utoaji ushauri na usimamizi majenzi nchi nzima lakini tumezungukwa na kila aina ya wahandisi, madaktari, wahasibu, wachumi na wanasayansi wa fani mbalimbali ambao hutushauri mambo mbalimbali ili kufikia malengo. Watanzania wanapaswa kufahamu kuwa uwekezaji wa majengo huhitaji wataalamu wa fani mbalimbali ili wakusaidie kukupa ushauri. Lazima ujue unawekeza kiasi gani cha fedha na baada ya muda gani fedha hizo zitarejea na baada ya muda gani faida itaanza kupatikana. Je kwa hali ya kipato chako unaweza kuhimili uwekezaji wa kiasi gani na wa aina gani. Hayo yote utayapata endapo utawatumia wataalamu.
Kuamini Kuwa Huwezi
Hakuna aliyezaliwa na pesa, sote tumezaliwa tukiwa watupu, hivyo sote tuna fursa sawa za kuwa tajiri au maskini, chaguo ni lako. Mazingira yaliyokuzunguka na majukumu makubwa uliyonayo yasikufanye uwe mnyonge na kisingizio cha wewe kushindwa kufikia lengo la kumiliki nyumba ya makazi au biashara. Ikatae akili ya kushindwa, kwa nini wengine waweze na wengine washindwe kwenye jambo moja linalofanana, utagundua kuwa tofauti ipo kwenye namna ya kufikiri na utayari wa kufanya maamuzi.
Kuna faida kubwa na nyingi kwenye uwekezaji wa majengo, ni rahisi wakati wa ujenzi pia ni rahisi wakati wa usimamizi na umiliki. Fikiria hasara na kadhia utakazopata endapo hutamiliki nyumba yako na faida endapo utamiliki nyumba yako ya biashara na makazi. Anza safari yako sasa kwa kiasi ulichonacho na amini kuwa utaweza.
Kuamini Kuwa Benki Ni Rafiki
Nimeshuhudia majengo mengi yakipigwa mnada na mawakala wa benki mbalimbali hapa nchini. Nimeshuhudia familia zikisambaratika, wamiliki wa nyumba wakipoteza fahamu na hata kupata maradhi sugu yanayohusiana na mfumo wa fahamu. Sababu kuu utaambiwa ameshindwa kuilipa benki Fulani kutokana na mkopo aliochukua na kununua gari anayotembelea kwa sasa au biashara aliyoianzisha hivi karibuni. Hii ni hatari sana, hali hii ikikukuta lazima upoteze “network za kichwa” lazima upoteze mwelekeo wa maisha ikiwa hiyo ndiyo nyumba pekee inayokustiri na kukuwezesha kupata chochote kwenye maisha yako. Lazima utambue kuwa benki zipo kibiashara zaidi na si kirafiki kama wengi wanavyofikiri, wanapokuwezesha jambo Fulani lazima na wewe uwape sehemu ya faida hiyo tena kwa wakati maalumu. Pata ushauri kabla hujaweka nyumba yako rehani ili uepukane na kadhia hii, pia si vema ukanunua nyumba ya kwanza kwa kutumia mkopo wa benki za biashara pasipo kupata ushauri, utaumia na utabeba mzigo utakaokushinda siku za usoni. Zipo njia nyingi za kukuwezesha kumiliki nyumba yako pasipo kuwa na msongo wa mawazo au kukosa usingizi. Muhimu ni kupangilia kipato chako na kuweka kipaumbele kwenye kujilipa wewe mwenyewe na ndipo utakapoweza kuwekeza kwa kile unachokihitaji.
SOMA; USHAURI; Mambo Ya Kuzingatia Pale Biashara Yako Inapokutana Na Ushindani Mkali.
Kununua Na Kujenga Mahali Pasipo Sahihi
Tumechoka kuona na kusikia nyumba zilizojengwa kwa gharama kubwa zikibomolewa kwa sababu yoyote ile isiyo na mashiko masikioni mwa watu. Kuna kesi nyingi sana zipo mahakamani kuhusiana na ujenzi holela wa majengo mbalimbali hapa nchini. Jitahidi sana kuepukana na hali hii isikufike kwenye uwekezaji wako kwa kufanya tafiti kabla hujanunua na kujenga nyumba yako. Epuka hifadhi za barabara, hifadhi za misitu na wanyamapori, pia epuka hifadhi mbalimbali za miundombinu. Zingatia sana ili kuepukana na migogoro isiyo na ulazima na yenye uwezekano wa kukwepa endapo utakuwa makini. Pia kwenye viwanja kuna utaratibu wa ujenzi na zingatia matumizi sahihi ya viwanja, fikiri kwanza kabla ya kununua kiwanja, unanunua kwa lengo gani, usijenge kiwanda kwenye eneo la makazi au makazi kwenye eneo la biashara. Kama huna ufahamu wa maeneo haya tafadhali pata ushauri kwanza.
Kufanya Makadirio Ya Chini Kwenye Uwekezaji
Kuweka Malengo ni jambo muhimu na lenye maana sana kwenye maisha yetu. Malengo hutuwezesha kutathmini mwelekeo wa mambo yote tunayoyasumbukia. Pasipo malengo ni vigumu sana kutathmini jitihada ya mambo tuyafanyayo hatimaye hukata tamaa kirahisi na kutofikia lengo kwa wakati. Hata kwenye uwekezaji wa majengo huhitaji kufanyika mahesabu ya kina juu ya gharama halisi za uwekezaji. Tumia wataalam wakuandalie mchanganuo wa bajeti halisi itakayo kuwezesha kufikia lengo lako kulingana na uwezo wa kipato chako. Watu wengi wamejikuta wakifanya uwekezaji ulio juu ya uwezo wao na hatimaye kuacha majengo kuwa magofu na maficho ya wezi na wakabaji. Usifanye makosa haya, mtafute mtaalamu akushauri ni namna gani utafanikiwa kuwekeza kulingana na kipato chako. Huna sababu ya kuwa na msongo wa mawazo au kukosa usingizi kwa sababu zinazoweza kuzuilika.
Tuendelee kuwa pamoja kupitia AMKA MTANZANIA tufike kwenye kilele cha mafanikio, pia endelea kufuatilia makala zijazo ili ujifunze zaidi.
Mwandishi wa makala hii ni mwanataaluma na mshauri wa ujenzi.
Anapatikana kwa: Simu: +255 685 729 888,
Email: kimbenickas@yahoo.com