Habari rafiki na msomaji wa uchambuzi wa vitabu. Ni matumaini yangu unaendelea salama na safari ya mafanikio. Wiki hii nakukaribisha kwenye uchambuzi wa Kitabu cha Millionaire Fastlane kilichoandikwa na mwandishi MJ DeMarco. Kitabu hiki kwa kweli ni moja ya vitabu vizuri sana. Kitabu hiki kinaongelea njia mbalimbali za kufikia Utajiri. Na Falsafa anayojaribu kufundisha, ni kwamba kuwa tajiri kwa haraka ni kitu kizuri kinachowezekana, na utajiri utaufurahia zaidi ukiupata ukiwa kijana, maana utakua na afya na nguvu kuliko kusubiri kuja kutajirika ukiwa na miaka zaidi ya 50. Katika kitabu hiki zipo njia kadhaa zinazotumiwa na matajiri kupata utajiri wa haraka, na jinsi wanavyozitumia kikamilifu. Hapa nimekuwekea mambo 20, ambayo ni machache sana ukilinganisha na mambo yaliyopo kwenye kitabu hiki.

 
Karibu tujifunze zaidi.
1. Kushindwa kwako kufikia mafanikio hakujasababishwa na vile ambavyo hujavifanya, bali ni vile ambavyo umekua unavifanya visivyo sahihi ndivyo vimekufikisha hapo ulipo. Kama mpaka sasa hujawa tajiri au hujafanikiwa kwenye jambo fulani, ACHA kufanya vitu unavyo fanya, na fanya vitu vingine. Acha kufuata mkumbo wa watu, Acha kutumia kanuni ambazo siyo sahihi, Acha kutumia njia ambazo zinakupelekea kua mtu wa kawaida kama wengine. Tafuta njia mpya, tafuta maarifa mapya. If you want to keep getting what you’re getting, keep doing what you’re doing.
2. Ule utamaduni wa kusoma kwa bidii ufaulu vizuri upate maksi nzuri halafu upate kazi nzuri haupo tena. Ukiwa na mawazo hayo utamaliza chuo na first class yako halafu utaingia mtaani unakutana na mambo tofauti kabisa. Halafu cha ajabu hakuna hata anayejali hiyo first class, unaenda kuomba kazi unakuta bosi pale ana diploma na anajua mambo sana. Ndio maana watu wanarudi shule kuongeza elimu wakiamini na kipato chao kitaongezeka, bila kufanya tathimini ya muda na gharama wanayoitumia ukilinganisha na ongezeko analoweza kulipata.
3. Kuna njia tatu kuu za mtu kufikia utajiri
· Njia ya pembezoni (sidewalk roadmap). Hii ndio njia ya uhakika kua maskini na ndio inayotumiwa na wengi
· Njia ya taratibu (slowlane roadmap). Hii njia inayotumiwa na baadhi, ambao huishia kua watu wa kawaida (mediocre) au watu wa kipato cha kati (middle class). Wapo wanaokua matajiri kwa njia hii ila inawachukua muda mrefu sana, na pengine kushindwa kufurahia utajiri wao maana wanaupata utajiri wakati umri umeshaenda.
· Njia ya haraka (Fastlane roadmap). Hii njia hutumiwa na wachache sana, na ndio wanaokua matajiri kwa haraka.
4. Katika njia ya Sidewalk, wafuasi wa njia hii kwanza hawana mpango wa kifedha (financial plan), kwa hiyo hatima yao ya kifedha haijulikani au kwa maneno mengine haipo. Kila kipato cha ziada wanachopata wanakitumia kununua vitu vya kuwapa furaha ya muda. Mfano mtu ananunua nguo, simu kali, gari jipya kwa sababu kipato kimeongezeka. Wanaotumia njia hii mara nyingi wanakua watumwa wa staili za maisha za sasa. Yaani wanataka waonekane ni watu wa kwenda na wakati, ukija mtindo mpya wa mavazi na yeye anataka ashone, likija toleo jipya la simu na yeye anataka awe anaimiliki. Mara nyingi huishia kwenye madeni, maana hutumia zaidi kuliko wanachoingiza. They spend more than what they earn
5. Kuwekeza kwenye vipande (mutual fund) au soko la hisa (stock market) ni moja ya njia za kutajirika kwa taratibu sana (slowlane). Yaani itakuchukua muda mpaka uwe tajiri kwa kujidundulizia kwenye mutual fund au hisa. Mfano hakuna mtu anayetajirika akiwa kijana chini ya miaka 30 kwa kupitia njia hiyo. Ni njia inayohitaji muda mrefu. Mfano mpaka ufike umri wa miaka zaidi ya 50, na uwe umeanza mapema.
SOMA; Sababu Kumi Kwa Nini Ni Muhimu Sana Wewe Kuwa Tajiri.
6. Matajiri hawatumii soko la hisa kujipatia utajiri, bali wao wanatumia uwekezaji huo kuendelea kuwa matajiri na kutengeneza kipato kikubwa. Mfano kama kwenye soko la hisa ukiwa na 100,000/= pakawepo na ongezeko la asilimia 10% utakua utatengeneza 10,000/=, lakini kwa tajiri mwenye bilioni kumi (10,000,000,000) kwenye soko la hisa, ikitokea tu hata ongezeko la 5% anakua ametengeneza milioni mia tano (500,000,000). Hapo yeye anaweza kuishi kwa hiyo faida tu. Lakini je kwa Yule anayetengeneza elfu 10 ataweza kuishi kwa kiwango hicho? Hiyo ndiyo tofauti ya matajiri wanaotumia soko la hisa kubakia matajiri, wakati watu wa chini wakitumia kudunduliza ili wapate utajiri.
7. Leo yako, ni matokeo ya jana yako. Yaani jana yako ndiyo iliyoweka msingi wa leo yako. Na hivyohivyo leo yako inaathiri kesho yako. Kama huna furaha ni wakati wakuacha kile unachofanya, kisha unatafakari njia iliyokufikisha hapo ulipo, na uliipitaje, kisha unabadilisha njia.
8. Safari ya maelfu ya kilometa lazima ianze na hatua moja. Hata uwe na ndoto kubwa kiasi gani, lazima kuna mahali utaanzia. Cha muhimu kujua hatua ya kwanza unayopiga ni ipi, na je hatua hiyo iko kwenye njia sahihi? Ukishapata uhakika, anza mara moja kupiga hatua ya kwanza.
9. Utajiri ni mchakato na sio tukio (Wealth is a process, not an event). Utajiri unatokana na mchakato wa kufuata fomula maalumu iliyohakikishwa kukufikisha huko kwenye utajiri. Unapoona kampuni Fulani imeibuka kidedea kua kampuni bora ya mwaka hilo ni tukio na sio mafanikio. Au mfano unaona mchezaji amepewa tuzo kwa kuwa mchezaji bora wa mwaka, lile nalo ni tukio la kutambua mafanikio, mafanikio halisi ni ule mchakato mchezaji huyo amekua akiufanya mpaka kufikia hapo. Wengi wetu tumekua tukivutiwa na matukio na kusahau mchakato hii husababisha kushindwa kuujua na kufuata ule mchakato uliomfikisha pale. Tukio ni kwa ajili ya kutambua (recognition) mchakato/mafanikio. Process makes millionaires, and the events you see and hear are the results of that process. Without process, there is no event.
10. Imani (beliefs) zetu zina athari sana katika mafanikio ya kifedha. Mfano kama unaamini kwamba matajiri wanapata utajiri kwa kuwekeza kwenye mutual fund (vipande) akili yako itakua inakuelekeza hukohuko. Hivyo basi kama unaamini utajiri unapatikana kwa muda mrefu, ndivyo hivyo matendo yako yataendana na imani yako, utaishia kutumia mbinu zenye kukuletea utajiri kwa muda mrefu kama unavyoamini. Maana ukipewa mbinu ya kuleta utajiri kwa haraka, imani yako itakataa utaona siyo sahihi.
11. Katika kuweka vipaumbele, watu wanagawanyika katika makundi mawili: Kundi la kwanza ni wale wanaotaka kuonekana matajiri na kundi la pili ni wale wanaotaka kua matajiri. Hilo la kwanza ni rahisi ila hilo la pili sio rahisi. Hii ina maana kwamba watu wengi wanatamani waonekane ni matajiri, hivyo hununua vitu vya gharama, na kufanya matumizi makubwa ya hela ili tu waonekane wanazo. Kwa kifupi wao ni watumiaji. Jinsi unavyojaribu kutaka unonekane tajiri, ndivyo umaskini nao unakung’angania. Wakati kundi la pili wao wanataka kuwa matajiri na si kuonekana matajiri, hivyo wanafuata kanuni za mafanikio, wao ni wazalishaji zaidi, wao ni wabunifu, wanabuni bidhaa au huduma ambazo zinakua ni suluhisho la changamoto zinazowakabili watu. Hawaishii hapo tu wanabuni au wanatumia mifumo mizuri ya kibiashara (business model) jinsi ya kumfikishia mteja bidhaa au huduma, na jinsi ya kupata malipo yake. Je wewe upo kundi lipi?
SOMA; FEDHA: Kama Una Mtazamo Huu Kuhusu Pesa, Tayari Wewe Ni Tajiri.
12. Utajiri ni mzuri sana kama ukiupata ungali kijana na sio ukiwa umri umeenda. Zipo njia kama za kuwekeza kwenye soko la hisa au kununua vipande ambapo uwekezaji unakua taratibu, ili uwe tajiri wa kweli inakuchukua hadi miaka 40. Sasa hebu ongeza umri wako na miaka 30 au 40. Ina maana utafurahia utajiri wako ukiwa na umri zaidi miaka 60. Kumbuka utajiri ni mahusiano mazuri na familia, afya pamoja na uhuru. Ukiwa na miaka 60 kuna uwezekano mkubwa ukawa hauko fiti kivile. Hivyo hutaweza kufurahia utajiri wako. Wealth is best experienced when you’re young, vibrant, and able, not in the twilight of your life.
13. Kuuza muda wako ni kuuza maisha yako. Muda sio pesa tu, bali muda ndio maisha yenyewe. Mfano unapokua umeajiriwa ukawa unafanya kazi masaa 8 kwa siku ili upate kipato, ina maana unauza sehemu ya maisha yako ili upate fedha za kuishi hayo masaa mengine. Kama ukifanya kazi unalipwa, usipofanya haulipwi, hii ina maana unaifanyia kazi fedha
14. Kuna tofauti kati ya kupata utajiri kwa haraka (get rich quick), na kupata utjiri kirahisi (get rich easy), japo wengi wamekua wakishindwa kutofautisha. Wengi wamekua wakiaminishwa na kuaminisha kwamba kua tajiri haraka haiwezekani au ni kitu kibaya. Wengi wanaamini ili kua tajri itakuchukua zaidi ya miaka 30 kufikia kwenye utajiri. Imani hii inawapelekea kuchagua njia au mifumo ya kuwapelekea kupata utajiri kwa muda mrefu kama wanavyoamini na hata hivyo wanaofanikiwa ni wachache sana, wengi wanakata tama mapema. Utajiri kwa muda mfupi ni kitu kizuri na kinawezekana. Teknolojia za siku za leo zimerahisisha sana mambo. Siku za leo Unaweza kuwafikia wateja wengi na kwa hara zaidi. Ukiwa na bidha au huduma nzuri na ukatumia business model nzuri unaweza kuwa bilionea kwa kipindi kisichozidi hata miaka kumi. Mfano Bilionea Mark Zuckerberg ambaye ni mmiliki wa Facebook ambayo ilianza 2004 hata miaka 10 haikuisha tayari akawa bilionea mkubwa duniani.
15. Utajiri haupimwi kwa fedha tu, bali utajiri unapimwa katika maeneo matatu makuu.
· Mahusiano mazuri na familia yako, ndugu na jamaa wanaokuzunguka. Kama fedha zinakufanya unafarakana na mke, watoto au ndugu, hutaweza kufurahia utajiri ulionao.
· Afya nzuri na nguvu. Kama afya yako ni mbaya hata uwe na pesa nyingi kiasi gani huwezi kufurahia.
· Uhuru. Kama huna uhuru wa kufanya uchaguzi wa vitu unavyotaka, au huna uhuru wa kuishi maisha unayohitaji, basi hujatajirika.
16. Kua mzalishaji zaidi na sio mtumiaji. Wazalishaji ndio wanaokua matajiri na sio watumiaji, ukiona wewe kila mara unataka kununua vitu, na huna mawazo ya kuzalisha kitu, basi ujue utaishia kuwa maskini au mtu wa maisha ya kati. Wazalishaji hutumia mbinu za kuwafanya wateja wao kuwa na kiu ya kununua hata kama hawana uhitaji. Kama unataka kua tajiri kweli lazima uondokane na fikra za kua mtumiaji zaidi, na badala yake uwe na fikra za kua mzaishaji. Kabla hujanunua kitu, hebu jaribu hata kujifunza ni jinsi gani kinazalishwa, na je wewe unaweza kua mzalishaji? Hata kama hutazalisha kwa kipindi hicho, lakini kujihoji huku kutaifanya akili yako iwe macho, na kuweza kukuzalishia mawazo yenye kuzalisha fedha. Mfano kama ni nguo, jaribu kudodosa imetengenezwa kwa malighafi gani, na kiwanda kipo nchi gani, na je kampuni hiyo inatumia mifumo gani kusambaza na kuwafikia wateja
SOMA; Kama Una Tabia Hii Moja Una Uhakika wa Zaidi ya 90% Wa Kufanikiwa Kwenye Chochote Unachofanya.
17. Waandishi wa vitabu vya mafanikio na fedha, mara nyingi njia wanazofundisha sio walizotumia wao kufikia mafanikio. Mfano mwandishi ameandika jinsi ya kua tajiri kwa kuwekeza kidogo kidogo kwenye soko la hisa ambapo njia hiyo mpaka uwe tajiri itachukua miaka zaidi ya 30. Huku yeye anakua tajiri haraka kwa kuuza hicho kitabu
18. Kanuni ya Effection (The law of effection). Kanuni hii inasema wa kadiri unavyoathiri maisha ya watu kuwa mazuri ndivyo na wewe unakua tajiri. Athiri mamilioni upate mamilioni. Je ni wangapi wanaonufaika na kazi yako, juhudi zako zinawasaidia watu wangapi. Umetatua changamoto gani? Idadi ya maisha ya watu unayoyagusa ndiyo itakayoamua kiwango cha kufanikiwa kwako. Gusa maisha ya mamilioni kwa huduma au bidhaa nawe utapata mamilioni. Kila unachofanya wewe cheza na namba, fikiria ni watu kiasi gani watanufaika na huduma au bidhaa yako.
19. Wewe ndiye gari la kukufikisha kwenye mafanikio. Hivyo wewe ndiye kiungo na rasilimali muhimu kuliko zote, na ndiye mwenye dhamana ya kuifanya safari ya mafanikio iwe halisi. Kufanikisha hilo lazima uwe unajimiliki. Kama umeajiriwa na chanzo chako kikuu cha kipato ni ajira basi ujue unamilikiwa na mtu, na kama unamilikiwa na mtu utakaua na maamuzi kidogo sana juu yako. You must own your vehicle (YOU).
20. Kujilipa mwenye kwanza (Pay yourself first) haiwezekani kama umeajiriwa. Falsafa ya kujilipa mwenye kwanza kila unapopata kipato ni falsafa inayotumiwa na wanaotajirika polepole, ikimaanisha kwamba kila kipato unachopata unatenga kwanza kiasi Fulani na kukidunduliza bila kukitumia kwa muda mrefu. Sehemu ya fedha hizo wengine huwekeza kwenye masoko ya hisa na vipande. Ila stori ni tofauti kama umeajiriwa, kwa waajiriwa kuna mshahara kabla ya makato (gross salary) na baada ya makato (takehome), hapo serikali inakua imechukua kodi yake tayari, na kama upo kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii kama NSSF unakatwa pia, au kama una na bima ya afya nayo inakatwa humohumo. Hivyo unachopokea wewe ndiye wa mwisho kulipwa. Mwajiri anajilipa kwanza ndio analipa kodi, wakati mwajiriwa kodi inalipwa kwanza yeye ndio analipwa mwishoni.
Asanteni sana
Tukutane wiki ijayo
Makala hii imeandikwa na Ndugu Daudi Mwakalinga mwandishi, mhamasishaji na mshauri katika masuala ya kilimo. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu 0763 071007 au barua pepe daudimwakalinga@yahoo.com au dd.mwakalinga@gmail.com