Je, umeshawahi kujiuliza unacheka vipi na kwa nini? Kila mmoja wetu ameshawahi kucheka au kulia, labda tu kama ana tatizo. Kucheka na kulia inatazamwa kama vitu muhimu sana katika jamii yoyote kwa kucheka au kulia, mwili hufanya mabadiliko ambayo ni muhimu sana kwetu binadamu. Kucheka na kulia ni kama sifa za lazima kwetu katika kutufanya tuishi tukiwa na afya pamoja na maisha marefu.
Kulia ni mchakato wenye utata mwingi sana kuliko watu wengi wanavyofikiria. Kuna aina tatu za  machozi, ambazo nina uhakika wengi wetu hatuzijui au tulikuwa hatujui kwamba, machozi yamegawanyika.
Kuna machozi yanayofahamika kama Basal, ambayo haya ni yale yenye kufanya macho kutokuwa makavu, yaani yanakuwa na maji muda wote.
Halafu kuna machozi yanayofahamika kama Reflex, haya ni yale ambayo yanatoka pale macho yanapochokozeka, kama vile yanapoingiwa na moshi au maji ya vitungu na vitu vingine vya aina hiyo.
Machozi ya aina  tatu ni yale yanayofahamika kama Psychic. Haya ni machozi yanayotoka wakati unapochokozeka kihisia, iwe kwa huzuni, huruma, furaha au shukrani.
Machozi ya kihisia yana kemikali na homoni, ambazo zinapopunguzwa mwilini humfanya mliaji kujihisi vizuri. Ndiyo maana inashauriwa kwamba, mtu anapokuwa kwenye uchungu fulani, akilia, aachwe alie tu. Baada ya kulia, mtu hujisikia kufarijika kiasi.
Kuna mambo ambayo yanakubalika katika jamii au jamii zote kwamba, mtu anapolia hakuna wa kumshangaa. Mambo kama misiba, simanzi na mengine ya aina hiyo. Iliaminika na inaaminikia kwamba, mtu asipolia wakati akiwa kwenye maumivu hujiumiza. Ni kweli kujiumimza kwa sababu anashindwa kupunguza hisia hizo za maumivu. Huu ni ukweli wa kisayansi na ndiyo maana katika jamii nyingi, kulia sana baada yakufia kwa mfano kama ni lazima.
Uzoefu wa maisha na mapenzi ni sababu nyingine ambazo zinaruhusiwa na jamii kumfanya mtu kulia. Wanawake wameruhusiwa au kufanywa na jamii kulia zaidi. Lakini faida za kulia zinashauri kwamba, mwanamume ndiye ambaye angetakiwa kulia zaidi kuliko mwanamke.
Kila jamii kwa mila na desturi zake, au mazoea yake, zimeruhusu kulazimika mtu kulia kwa simanzi au maumivu. Lakini pia jamii hizo zimeweka mipaka au masharti ya wapi na wakati gani mtu alie. Kwa baadhi ya jamii, umewekwa muda maalum wakulia kwenye misiba. Kwa mfano, baadhi ya jamii, kulia kwa sababu ya kifo cha mtu huruhusiwa hadi saa nne na baada ya hapo mkuu wa jamii hiyo hutangaza kwamba, msiba huo ulitokea miaka minne iliyopita na haruhusiwi mtu tena kulia tena.

Kama ilivyo kulia, kucheka pia kumewekewa vigezo na mipaka na jamii. Kitu ambacho kinaonekana ni cha kuchekesha Tanzania kwa mfano, kinaweza kisiwe cha kuchekesha huko au mahali pengine Duniani. Jamii pia hupanga ni mahali na kitu gani ambacho kwacho, mtu anaruhusiwa kucheka.
Kama ambavyo wanasayansi wengi wamekuwa wakisema kucheka ni tiba, huu ndiyo ukweli. Kwa kucheka mwili hupata ahueni na kumpumzika. Wakati wakucheka maeneo mengi ya mwili hupata faida. Maeneo kama kongosho, tumbo, mfumo wa kupumua, uso, miguu na misuli ya migongo.
Wanasayansi hivi sasa wamethibitisha kwamba, kucheka mara mia ni sawa na kufanya mazoezi kwenye mashine ya kukimbilia kwa dakika kumi au dakika kumi na tano kwenye baiskeli ya mazoezi. Kucheka husaidia kutibu mwili kwa kushusha shinikizo la damu na kuongeza msukumo wa kawaida wa damu. Watu waliopaata kiarusi wanatakiwa kucheka sana ili kuisaidia miili yao kujitibu.
Tunapocheka, uzalishaji wa T- Cell, ambazo ndizo zinaharibu uvimbe wa mwili kukabiliana na virusi mbalimbali, huongezeka na protini inayokabiliana na maradhi mwilini, Gamma interferon huzalishwa zaidi. Kucheka, imebainika kwamba, husaidia kupunguza kiwango cha homoni ya sonono mwilini na kumwezesha binadamu kukabiliana na misukumo ya kimaisha.
Kuna watu ambao wanapokuwa kwenye sononi au huzuni kali, hupenda kuchukua mikanda ya video ya kuchekesha au kusoma vitabu au magazeti yenye habari za kuchekesha zaidi. Njia hii imethibitishwa kuwasaidia sana watu hao.
Ukweli ni kwamba, tunahitaji machozi na vicheko ili tuweze kuendelea kuwepo na kutenda katika dunia hii. Kama tulivyoona, kuna faida za kulia na kucheka na hizo zote ni njia za kupunguza maumivu ya kihisia.
Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikiona endelea kutembelea AMKA MTANZANIA kujifunza na kuhamasika.
Karibu pia kwenye DIRA YA MAFANIKIOkujifunza na kuboresha maisha yako.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
IMANI NGWANGWALU,
0713048035,