Habari za leo rafiki,

Ni imani yangu kwamba unaendelea vyema kabisa. Hongera kwa nafasi hii nyingine nzuri sana ya leo, leo ni siku ya pili ya mwezi wa mwisho wa mwaka 2016. Yaani zimebaki siku 29 pekee tumalize mwaka huu 2016.

Ni hatua kubwa sana tumepiga mpaka sasa kwenye mwaka huu 2016, kuna mengi ambayo tulipanga kufanya mwaka huu, kuna ambayo tumefanya na yapo ambayo tumekwama. Hii ni hali ya kawaida kabisa kwa maisha ya binadamu. Lakini hatukubaliani nayo kirahisi, bali tunahitaji kuitumia kusonga mbele zaidi.

Rafiki yangu, leo nakuandikia ili uchukue nafasi ya kuutafakari mwaka 2016 umekwendaje kwako, yapi ambayo umeweza kufanikisha, na yapi ambayo umekwama kufanikisha. Ndiyo najua bado 2016 haijaisha, siku 29 zilizobaki unaweza kufanya makubwa, lakini tunahitaji muda wa kutafakari vyema kabla mwaka 2017 haujaanza.

Tahadhari ambayo nimekuwa nakupa tangu mwaka 2013 wewe rafiki yangu ni kutokujikuta kwenye ule mkumbo wa watu kusema mwaka mpya mambo mapya siku ya tarehe moja mwezi wa kwanza, lakini ikifika tarehe 10 umesharudi kwenye maisha yako ya kila siku.

Wewe rafiki yangu ni mtu makini, najua hilo na nataka utumie umakini wako kuweza kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako kwa mwaka unaokuja 2017. Hivyo basi, leo nataka utenge muda kidogo, angalau nusu saa, kaa na utafakari mwaka 2016, angalia yale uliyopanga kufanya mwaka huu 2016 na angalia mpaka sasa ni yapi ambayo umefanikisha kufanya.

Hili ni zoezi muhimu sana kwako kufanya rafiki, na nitahitaji unitumie jibu moja kati ya yale utakayotafakari.

Katika tafakari utakayofanya leo, ni vyema uwe na kalamu na karatasi ili uweze kuandika, unaoandika inakaa zaidi kwenye akili yako na unakuwa na msukumo wa kufanyia kazi.
Fanya yafuatayo;

1. Orodha ya kwanza; andika malengo yako uliyojiwekea kwa mwaka huu 2016, yaandike kama ulivyoyaandika mwanzoni mwa mwaka huu. Andika yote kabisa, iwe uliyafikia au hukuyafikia.

2. Orodha ya pili andika yale malengo ambayo umeweza kuyakamilisha ndani ya mwaka huu mpaka kufikia leo. Yaorodheshe malengo yote uliyokamilisha kwa mwaka huu 2016.

3. Orodha ya tatu, andika malengo ambayo umeanza kuyafanyia kazi lakini bado hujayakamilisha mpaka kufikia sasa. Yaorodheshe malengo yote hayo.

4. Orodha ya nne, andika yale malengo ambayo hukuyagusa kabisa. angalia katika ile orodha ya malengo uliyojiwekea kwa mwaka huu 2016 lakini hujaweza kuyagusa kabisa, yaani yapo vile vile kama ulivyopanga, hujachukua hatua yoyote.

5. Baada ya orodha hizi nne, angalia ni kwa kiwango gani malengo yako ya mwaka 2016 yametimia, kwa kiwango gani unafanyia kazi na kwa kiwango gani hujagusa kabisa.

6. Swali muhimu sana ambalo nitahitaji na mimi unishirikishe jibu ni hili; BI CHANGAMOTO IPI KUBWA UMEKUTANA NAYO MWAKA 2016 AMBAYO IMEKUZUIA KUFIKIA 
MALENGO YAKO YOTE? Angalia kwa yote ambayo umeyapitia mwaka huu 2016, angalia ni lipi kubwa kabisa lilikuwa kikwazo cha wewe kufikia mafanikio.

Nahitaji sana unishirikishe changamoto hiyo kubwa ambayo imekuwa kikwazo kwako kufikia malengo yako yote ya mwaka 2016.

Kwa nini nahitaji sana unishirikishe changamoto hii?

Kwa sababu sasa hivi naandaa semina ya mwaka 2017 ambayo itaanza tarehe za mwanzo kabisa za mwaka 2017. Katika semina hii nataka tufanye mapinduzi makubwa sana kwenye maisha yetu. Nataka tuuchukue mwaka 2017 tofauti kabisa na tulivyokuwa tunaichukua miaka mingine ya nyuma. Kuna kitu kikubwa sana nakiandaa kwa ajili ya mwaka huu 2017, mimi mwenyewe nakisubiri kwa hamu sana, kwa sababu sijawahi kukijaribu kwa muda mrefu, tutakianza wote mwaka huo 2017.

Hivyo nahitaji sana kupata changamoto yako ili niweze kuandaa mafunzo ya semina hii yakuwezeshe kutatua changamoto hiyo na nyingine kama hizo ili mwaka 2017 uwe mwaka wa kipekee kwako.

Hivyo rafiki, naomba ufanye zoezi hilo leo, fanyia kazi hayo halafu mimi nitumie jibu la ile changamoto kubwa iliyokuzuia kufikia malengo yako ya mwaka 2016. Nitashukuru sana rafiki iwapo nitapata majibu yako leo na kesho, ili niweze kujumuisha changamoto yako katika mafunzo ya semina ijayo.

Kuna kitu kikubwa sana kinakuja kwa mwaka 2017 rafiki yangu, endelea kuwa hapa, tutafanya makubwa mwaka 2017 kwa pamoja.

Nasubiri kusikia changamoto yako kubwa rafiki, tafadhali niandikie kwa kujibu swali hilo muhimu na kutuma kwenye email hii makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK