Habari mpendwa rafiki na msomaji wa amka Mtanzania? Ni matumaini yangu kuwa hujambo na unaendelea vizuri katika shughuli zako za kila siku. Pole pia rafiki kwa changamoto unazokutana nazo katika maisha yako. Je huwa unazichukuliaje hizo changamoto unazokutana nazo? 

Umezichukulia kama ni laana au fursa? Kwa kila changamoto unayokumbana nayo hakikisha unajifunza kitu usipofanya hivyo utakua unaona mambo ni magumu.

Rafiki, kama ukizichukulia changamoto katika hali ya mtazamo chanya basi utakua uko sehemu sahihi lakini kama unachukulia changamoto unazokutana nazo kama vile ni mkosi au laana uko sehemu mbaya yakupasa ubadilishe mtazamo wako kwanza.

Mpendwa msomaji napenda kutumia nafasi hii kukualika tena katika makala yetu ya leo ili tuweze kujifunza wote kwa pamoja yale niliyoweza kukuandalia siku hii ya leo. Kwa hiyo nakusihi sana rafiki karibu tuweze kusafiri pamoja mpaka mwisho wa somo letu la leo.

SOMA; Huyu Ndiye Adui Namba Moja Kwenye Malezi Ya Watoto.

Katika makala yetu ya leo tutakwenda kujifunza wote kwa pamoja imani chanya unayopaswa kumjengea mtoto katika malezi. Karibu tujifunze ndugu msomaji. Ili tuweze kuwa na watoto bora katika jamii yetu yatupaswa kwanza tuweze kuwapatia malezi bora katika familia. Katika familia ndio msingi wa malezi ya mtoto unapoanzia hivyo kama mtoto amekosa kupewa malezi bora katika familia naye atakwenda kujenga jamii iliyo mbovu.

Wazazi ndio walimu wa kwanza katika malezi ya watu lakini siku hizi wasaidizi ndio wanageuka kuwa walimu wa kwanza katika malezi ya mtoto. Wazazi wanajisahau kwa kisingizio cha kuwa bize katika kutafuta mafanikio. Mafanikio yako unayoyatafuta yanaleta maana gani kama familia yako ni mbovu? Tunapaswa kurudi katika njia sahihi na kukumbuka wa wajibu mzazi ni upi. 

Kama mzazi ukishatambua kuwa wewe ndio mwalimu wa kwanza katika malezi ya watoto huwezi kujisahau kabisa na hata kukosa muda wa kuwaangalia watoto wako.

SOMA; Hii Ndio Faida Ya Kutumia Falsafa Ya Imani Ya Kidini Kwenye Malezi Bora Ya Watoto

Mpendwa msomaji, malengo mahususi ya somo letu la leo ni kufahamu imani chanya unayopaswa kumjengea mtoto katika malezi. Imani chanya unayopaswa kumjengea mtoto ni uwezo wa kujiamini na kumwambia kuwa anaweza kufanya kitu Fulani. Kuna baadhi ya wazazi wanakuwa wanawajengea watoto wao imani hasi ya kwamba wao hawawezi kufanya kitu Fulani. Imani hasi ya kumwambia mtoto kuwa huwezi kufanya kitu Fulani huwa inawaathiri sana kisaikolojia. Kama mzazi unatakiwa kumjengea mtoto imani chanya kuwa anaweza na siyo hawezi.

Rafiki, kuna watoto wengine wanaambiwa na wazazi wao, walimu au walezi wao kuwa hawana akili hivyo dhana hii inakuwa inajijenga kwa mtoto kuwa yeye hana akili na wenye akili ni watu wengine. hata mtoto kama anataka kuthubutu kufanya kitu Fulani anaogopa kufanya kulingana ana imani hasi aliyojengewa kuwa yeye hana akili na hawezi kufanya kitu. Tunaliona hili katika familia zetu ni jinsi gani watoto wanajengewa mitazamo hasi katika maisha yao.

Kuna wazazi, au walezi ambao wanakuwa wanawatishia watoto wao pale wanapokuwa wanajaribu kufanya jambo Fulani hivyo hii hali huwa inaua kipaji cha mtoto lakini pia hata ubunifu wa kufanya mambo mbalimbali katika maisha yake. Tunapaswa kuwajengea imani chanya kwa watoto kama vile wewe unaweza na siyo wewe huwezi badala ya kumwambia hawezi mwache ajaribu na mpongeze kwa kumpa moyo hata kama amekosea. Mtoto anapokuwa anajaribu jambo na mzazi unakosa kumpatia au kumjengea imani chanya juu ya kile anachofanya huwa inammaliza kabisa.

SOMA; Adhabu Saba (7) Zisizostahili Katika Malezi Ya Watoto.

Mpendwa mzazi na mlezi, unatakiwa kuchunga sana maneno unayomwambia mtoto wako kwani maneno hasi huwa yanaharibu watoto na kuwajengea imani hasi katika akili yao. Kuna siku moja nilishuhudia mtoto mmoja aliyesifiwa na mtu wa pembeni kuwa wewe ni mzuri lakini mtoto Yule aliweza kumjibu mtu Yule wa pembeni kuwa yeye si mzuri ni mbaya. Na mtu wa pembeni akamuuliza kwa nini unasema wewe ni mbaya? Mtoto akajibu kuwa mama yake huwa anamwambia kuwa yeye ni mbaya, yuko kama nyani.

Kwa kweli, mtoto Yule alikataa kabisa kuambiwa kuwa yeye ni mzuri na akaendelea kushikilia imani hasi aliyoambiwa na mama yake kuwa yeye yuko kama nyani hivyo ni mbaya. Watoto wanapata mateso makubwa ya akili ambayo athari yake ni kubwa kupita maelezo katika jamii yetu. Kama wazazi muda wa kuamka na kubadilika katika malezi ya watoto.

Hatua ya kuchukua leo, epuka kumjengea mtoto au watoto wako imani hasi inayompelekea kutokujiamini katika maisha yake. Anza leo kumwambia mtoto maneno chanya ya kumtia moyo na kumhamasisha katika kile anachofanya. Epuka maneno hasi yanayomharibu mtoto na kumjengea imani hasi na hatimaye kutokujiamini.

Mwisho, watoto wanahitaji malezi ya baba na mama kuliko malezi ya wasaidizi wa ndani. Hivyo basi, hatuwezi kuwajengea watoto msingi imara wa malezi kama mzazi unakosa muda wa kukaa na mtoto wako kumuuliza siku yake ilikwendaje ili kama kuna mambo ambayo haya kwenda vizuri akuelezee na wewe kama mzazi uweze kumtatulia mtoto wako. Kama mtoto anakosa mtu wa karibu wa kumwelezea matatizo yake, ambaye mtu sahihi ni wazazi ambao ni baba na mama au walezi. Kila mzazi awajibike katika kuhakikisha mtoto anapata malezi bora.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505/0767101504 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com, kessydeo@mtaalamu.net au unaweza kutembelea tovuti yake, www.mtaalamu.net/kessydeo ,www.actualizeyourdream.blogspot.com