Kila mtu ana ukuu ndani yake, ila ni wachache sana ambao wameweza kuishi ukuu huu. Wale wanaotambua na kuishi ukuu wao, wanafanya makubwa sana kwenye maisha yao. Ila wale ambao hawautambui na kuishi ukuu wao, wanabaki na maisha ya kawaida.

 

Changamoto kubwa ni kwamba, hakuna shule yoyote itakayokufundisha kuhusu ukuu wako. Shuleni utafundishwa vitu vikubwa sana, historia za miaka elfu 2 iliyopita, mzunguko wa damu wa kila mnyama, miamba mikubwa ambayo huenda hutaiona mpaka unapokufa, bila kusahau hesabu ngumu ambazo unaweza usizitumie tena mpaka unakufa. Lakini hatupati nafasi ya kufundishwa kuhusu ukuu wetu, hatupati njia ya kuweza kuujua na kuweza kuutumia kufanya makubwa.

Hapa ndipo mwandishi Lewis Howes, alipoamua kutafuta elimu hii ya ukuu kutoka kwa watu ambao wamefanya makubwa, watu walioweza kufika mbali kuliko walivyotegemewa. 

Akazungumza nao, akawahoji, akadadisi na kugundua mambo muhimu ambayo kila mtu akiyafanya, ataweza kuujua ukuu wake na kuutumia kufanya makubwa kwenye maisha yake. 

Lewis ameita kitabu chake THE SCHOOL OF GREATNESS, kwa sababu kupitia kitabu hichi utajifunza kwa kina namna ya kufikia ukuu wako na wewe kuwa mkuu sana.
Karibu sana tujifunze kwa pamoja kupitia uchambuzi huu wa kitabu.

1. Ukuu siyo tu kufanya mambo ya kishujaa, kwamba umeshinda medali kwenye mbio, au kushinda vita, au kuwa kiongozi mkubwa wa nchi unayefanya makubwa. Unaweza kuwa mkuu kwenye kila kitu unachofanya kwenye maisha yako. Unaweza kuwa na ukuu kama mzazi, msanii, mjasiriamali, na vingine vingi unavyofanya kila siku.

Zipo hatua kuu nane za kutengeneza na kufikia ukuu wako kwenye maisha. Hatua hizo ni kama ifuatavyo;

2. Hatua ya kwanza; TENGENEZA MAONO MAKUBWA YA MAISHA YAKO.
Huwezi kufikia ukuu kama huna maono makubwa ya maisha yako, kama hujui wapi unakwenda, huwezi kufika kwenye ukuu. Unahitaji kuwa na maono makubwa ya maisha yako, uyaone kabisa kwenye taswira yako, wapi unakwenda na utafikaje pale. Kila siku unapoamka unajiona pale unapotaka kufika. Maono yatakusukuma uweze kufikia ukuu wako.

SOMA; Tumia Muda Huu Mchache Kufanya Mabadiliko Makubwa Na Endelevu Katika Maisha Yako.

3. Hatua ya pili; GEUZA MATATIZO KUWA FAIDA KWAKO.
Hakuna mtu yeyote aliyefikia ukuu ambaye hakukutana na matatizo, changamoto na vikwazo vikubwa. Watu wa kawaida wanapokutana na hali hizi, wanakubaliana nazo na kuona hawana namna tena. Wanaofikia ukuu, wanapokutana na hali hizi, wanaangalia wanawezaje kutumia matatizo waliyonayo kuweza kufikia maono yao.
Hivyo usikimbie matatizo au changamoto zozote unazokutana nazo, hapo ndipo penye ukuu wako, tatua matatizo hayo au yavuke na utafika mbali.

4. Hatua ya tatu; TENGENEZA MTAZAMO WA USHINDI.
Moja ya vitu vinavyowatofautisha wakuu na wale wanaoishia kuwa kawaida, ni mtazamo. Wale ambao wanafikia ukuu, wana mtazamo wa ushindi, mara zote wanaangalia mambo kwa mtazamo chanya, kama yanawezekana, na kuweka juhudi zaidi ili kufika kule wanataka kufika. Lakini wale wanaoshindwa, kila wanachokiangalia wanaona sababu ya kushindwa. Ondoka kwenye hali hizo.

5. Hatua ya nne; JIANDAE KUWEKA KAZI.
Ukuu ungekuwa rahisi, kila mtu angekuwa mkuu. Kila mtu angekuwa na mafanikio na angekuwa mbali. Lakini siyo rahisi, inahitaji kuweka kazi, na siyo kazi tu, bali kazi kubwa na inayochosha. Utahitajika kufanya kazi zaidi ya kawaida, kuwa kwenye kazi zako kwa muda mrefu zaidi ya wengine. Kuna wakati utahitajika kusahau mapumziko ya mwisho wa wiki, hiyo yote katika kutengeneza ukuu.

Kuwa tayari kujitoa kuweka kazi, kama kweli unautaka ukuu.

6. Hatua ya tano; UTAWALE MWILI WAKO.
Mwili wako ni moja ya vitu muhimu unavyohitaji ili kufikia ukuu. Unahitaji kutawala mwili wako, unahitaji kutengeneza mwili ambao utakuwezesha kufanya makubwa. Na hapa tunaangalia afya ya mwili na akili. Kama afya yako ni mbovu, huwezi kufikia ukuu, hakuna watu wanaofikia ukuu wakiwa wamelazwa kwenye vitanda vya hospitali kila siku.
Angalia sana vitu unaruhusu viingie kwenye mwili na akili yako. Usiruhusu sumu iingie, kula vizuri, fanya mazoezi, na pata muda wa kupumzika.

SOMA; Kama Unataka Mafanikio Makubwa Katika Maisha Yako, Acha Kuogopa Kufanya Mambo Haya.

7. Hatua ya sita; TENGENEZA TABIA CHANYA.
Tunafanya kile tunachofanya sasa, kutokana na tabia ambazo tumejijengea. Ulijenga tabia huko nyuma, na sasa tabia zinakujenga wewe. Kama haupo kwenye ukuu, hatua ya kwanza unayohitaji kuchukua ili ufike kwenye ukuu, ni kuanza kutengeneza tabia chanya. Kuwa mtu wa kuwa na vipaumbele, vifanyie kazi kila siku, jua yapi muhimu kwako na yafanye hayo. Linda sana muda wako.

8. Hatua ya saba; TENGENEZA TIMU YA USHINDI.
Huwezi kufikia ukuu wewe peke yako. Kufikia ukuu siyo vita ya mtu mmoja, siyo jeshi la mtu mmoja, bali ni matokeo ya timu imara inayofanya kazi kwa ushirikiano kufikia ushindi.
Ili kufikia ukuu unahitaji watu wengi sana kwenye maisha yako.

Kwanza unahitaji watu wa kukuongoza, hawa wanaitwa MENTORS, hawa wanakuonesha wapi pa kupita ili uweze kufikia ukuu.

Pia unahitaji watu wa kukushauri na kukusimamia, hawa ni COACHES. Hawa wanazijua mbinu bora kwako kutumia ili kufikia ukuu.

Unahitaji watu watakaokusaidia pia kwenye yale unayofanya, huwezi kufanya kila kitu wewe mwenyewe, hivyo jenga wasaidizi wenye uwezo wa kufanya makubwa.
Tengeneza timu yako sasa, kama upo mwenyewe mwenyewe, unajidanganya.

9. Hatua ya nane; KUWA WA HUDUMA KWA WENGINE.
Kwa lugha nyingine, ongeza thamani kwenye maisha ya wengine. Ukuu siyo tu kuwa na maisha mazuri, kuwa na fedha nyingi au kushinda medali nyingi. Ukuu ni jinsi gani umegusa maisha ya wengine, ni kwa namna gani umeongeza thamani kwenye maisha ya wengine. Uwepo wako umekuwa na mchango gani kwa wengine kuwa na maisha bora na hata kufikia ukuu?
Chochote unachofanya kwenye maisha yako, hakikisha kinaongeza thamani kwenye maisha ya wengine. Kwa sababu hii ndiyo itakuwezesha wewe kuacha ina, na kuwa na ukuu unaodumu.

10. Kuona vizuri, geuza darubini yako ya maisha.
Darubini huwa zina pande mbili, ukiangalia upande mmoja, unaona vitu vya karibu kuwa mbali. Lakini ukigeuza na kuangalia kwa upande wa pili utaona vilivyopo mbali kwa ukaribu zaidi. Hivyo kama unaona mambo hayawezekani, huenda unaangalia kwa upande ambao siyo. Geuza darubini yako na utaona vitu vizuri zaidi. Hii ina maana ya kubadili mtazamo wako, na utaona vitu vinawezekana.

11. Unapokutana na ugumu, vikwazo au changamoto kwenye maisha yako, una mambo mawili unaweza kufanya;
Moja; unaweza usifanye chochote, ukaacha matatizo yale yakuelemee na kubaki kulalamika kwamba una bahati mbaya na kisirani.
Mbili; kupokea changamoto hiyo, kufanyia kazi ugumu uliokutana nao na kuufanya kuwa sehemu ya hadithi yako ya mafanikio.
Uamuzi ni wako kati ya hayo mawili, lakini kama unataka kuwa mkuu, basi huna budi kuchukua hatua ya pili.

12. Unapochagua kuwa mkuu, unapoanza safari ya ukuu, dunia haitakuacha kirahisi. Vitaibuka kila aina ya vikwazo kukuzuia, utaona kama dunia inapambana na wewe ili usiwe mkuu. Na hili linaweza kuwa kweli, kwa sababu dunia haitaki vinyonge viwe vikuu, hivyo inahakikisha anayefikia ukuu, amepambana hasa. Hivyo jiandae kama unaelekea kwenye ukuu.

SOMA; Tumia Siri Hii Moja Kupata Chochote Unachotaka Kwenye Maisha Yako.

13. Wakuu wote hufikia hatua ya kufanya kazi kama sehemu ya maisha yao, na siyo tu kukamilisha jukumu fulani. Wanapokuwa wanafanya kazi zao, akili na mawazo yao yote yanakuwa kwenye kazi ile, mpaka wanasahau kama kuna vitu vingine. Mtu anaweza kuwa kwenye kazi hiyo kwa masaa matano lakini yeye anaona ni kama nusu saa tu imepita. Hali hii inaitwa FLOW, kazana uweze kuifikia, utakuwa kitu kimoja na kazi unayofanya, na ukuu unakuwa wako.

14. Kitu ambacho kinaathiri kila unachofanya ni wewe mwenyewe. Kwa sababu wewe ndiyo upo kila mahali unapokuwepo. Iwe kwenye kazi, biashara, mahusiano, na hata maisha kwa ujumla. Hivyo bila ya wewe binafsi kuwa bora, huwezi kuwa bora kwenye chochote unachofanya. Bila ya wewe binafsi kuwa mkuu, huwezi kufikia ukuu kwenye jambo lolote. Hivyo anza na ukuu wako binafsi, hakikisha unajijenga kuwa bora, unajenga tabia nzuri kwako, unakuwa na afya bora ya akili na mwili.

15. Kujiamini wewe mwenyewe ni moja ya mahitaji muhimu ya kufikia ukuu. Kama hujiamini, kama huamini unaweza, hutaweza kufanya makubwa. Lakini pia kufikia ukuu, hupaswi kuwa na majivuno, kujiona wewe ndiyo wewe, unapaswa kuwa na unyenyekevu, jiamini lakini usiwe na dharau kwa wengine.

16. Huwezi kufikia ukuu, kama hupo tayari kufanya vile ambavyo wengine hawapo tayari kufanya. Kama huna mkuu yeyote wa kujifunza kwake, basi angalia ambao siyo wakuu wanakwepa kufanya nini, na wewe fanya hayo wanayokwepa wao. Ukuu siyo rahisi, na watu wengi hawapendi mambo magumu, fanya hayo magumu wewe na utaondoka kwenye kundi la wengi, na kufika kwenye kundi la wachache ambao ni wakuu.

17. Kuna watu watakuambia usifanye kazi kwa nguvu, bali fanya kazi kwa maarifa (don’t work hard, work smart), usiwasikilize wanakudanganya. Hakuna ukuu unaofikiwa bila kufanya kazi kwa nguvu, na maarifa ni muhimu mno katika kufikia ukuu. Hivyo ili kufikia ukuu, fanya kazi kwa nguvu na maarifa (WORK HARD AND SMART). Hakuna mkuu mvivu, usiwasikilize wavivu, weka kazi.

18. Kipaji pekee hakikutoshi wewe kuwa mkuu, wapo wengi wenye vipaji, lakini hakuna makubwa waliyofanya. Pamoja na kuwa na kipaji, lazima uweke kazi, tena kazi kubwa. Huwezi kutenganisha ukuu na kazi, lazima ufanye kazi sana, tena mara nyingi kazi ambayo haitaonekana. Baadaye unapofikia ukuu, wapo watakaosema una bahati, usiwasilize.

19. Uweke mwili wako kwenye kitu ambacho hautaki, hii inakusaidia kutengeneza nidhamu. Fanya kitu ambacho mwili wako unakataa au haupendi kufanya, uumize kwa kiasi, ili uweze kufungua ukuu uliopo ndani yako. Kama unafanya mazoezi, fanya mpaka mwili uanze kuuma, hapo unakuwa umeongeza wigo wako wa kufanya mazoezi. Hata kazi pia fanya hivyo.
Ukweli ni kwamba, huwezi kujua unaweza kwenda umbali kiasi gani, kama hutaenda mbali zaidi ya ulivyozoea. Hivyo huwezi kujua mwili wako una uvumilivu kiasi gani, kama hutauweka kwenye hali ngumu ambayo haijazoea. Huwezi kujua unaweza kufanya kazi kubwa kiasi gani, kama utaendelea kufanya kazi kama ulivyozoea.

20. Ili uweze kufikia ukuu, unahitaji kujijali wewe mwenyewe kwanza, unahitaji kujali afya yako, unahitaji kujipa kipaumbele kwanza. Huwezi kuwasaidia wengine wakati wewe mwenyewe upo kwenye matatizo. Hivyo jipe kipaumbele ili uwe kwenye nafasi nzuri ya kuwasaidia wengine.

Unaweza kuwa mkuu kama utachagua kuwa mkuu na kuweka kazi kubwa ili kuwa mkuu kweli. 

Fanyia kazi haya uliyojifunza, hasa zile hatua nane za kufikia ukuu, na utakuwa mkuu sana kwenye maisha yako.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea MOBILE UNIVERSITY (www.mobileuniversity.ac.tz)

Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita