Najua unajua kwamba utandawazi umeifanya dunia kuwa kijiji. Kila siku dunia inazidi kuwa ndogo zaidi na zaidi. Na hili limekuwa na madhara makubwa sana kwenye biashara.

Kwa mfano, siku za nyuma watu walifikiri ukishakuwa na biashara yako eneo fulani na ukaweza kuikuza pale, basi hakuna kinachoweza kukuhatarisha kama utakuwa mwangalifu kwa eneo ulipo. Hivyo wengi walikazana kuangalia pale walipo na kuhakikisha hakuna ushindani ambao ni hatari kwao.

IMG-20170611-WA0003

Lakini siku hizi, ushindani hauanzii hapo ulipo, unaanzia mbali kabisa, unaanzia huko duniani. Mtandao wa intaneti umerahisisha sana biashara. Mtu anaweza kununua kitu chochote, kutoka popote na kufikishiwa pale alipo.

Hata vitu ambavyo mtu hukuwa unategemea watu wanaweza kununua kwa njia ya mtandao, wananunua bila ya shida yoyote. Watu wana nafasi ya kuchagua kununua ndani ya nchi kwa njia ya mtandao na hata kununua nje ya nchi kwa njia hiyo ya mtandao.

Ndiyo maana nikasema kwamba chochote unachofanya, unashindana na watu bilioni saba duniani, na siyo wale wanaokuzunguka tu.

Sasa unapokuwa unashindana na watu bilioni saa, utakubaliana na mimi kwamba siyo zoezi rahisi hilo. Ukitaka kuhakikisha unawaweka chini watu wote hao na wewe kuwa juu, haitakuwa kitu rahisi kwako.

SOMA; BIASHARA LEO; Ingia Kwenye Biashara Yenye Ushindani Lakini Usishindane.

Hivyo badala ya kukazana kuwashinda wengine, nenda kinyume, kazana kuweka kitu zaidi kwenye kile unachofanya. Kazana kuweka roho yako na damu yako kwenye kile unachofanya. Kazana sana mteja akija kwenye biashara yako asikie mguso wa utu, wa kuthaminiwa na kujaliwa. Kwa njia hii mtu anafurahia na kuwa tayari kuja tena na tena na tena.

Kwenye fujo hizi za dunia ya sasa, anayeshinda siyo yule anayefanya tu kwa sababu anafanya, bali yule anayefanya kwa ajili ya kuyafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi. Na wewe unaweza kuwa mmoja wa watu hao, iwapo utaweka maslahi ya wengine mbele.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog