Yapo mambo ambayo kwa kawaida tunataka kutenda kila wakati, inaweza ikawa kwetu sisi au kwa wengine. Mambo hayo ambayo tunakuwa tunayapangilia yapo ambayo yanakuwa yanatuumiza sisi au wengine na yapo ambayo yanatoa msaada.

Siku zote katika maisha yako kabla hujatenda kitu chochote, kabla hujasema kitu chochote, jiulize kitu unachotaka kutenda au kitu unachotaka kusema je, kitaleta matokeo chanya kwako au hata kwa wengine?

Sio kwa sababu unayo nafasi nzuri ya kutenda au kusema hiyo ikawa na maana kwako ufanye au useme tu hata mambo yanayoumiza wengine. Unatakiwa kuwa makini na kuzingatia ni nini matokea ya kile ambacho unakwenda kutenda au kukizungumza.

Ni dhahiri wapo watu ambao moja kwa moja utawaumiza, kama utatenda au kusema maneno ya hasi, hata kama hujui jinsi unavyowaumiza. Pia uelewe wapo watu utakaowaponya kama utaamua kusema au kutenda matendo chanya ambayo yana msaada mkubwa katika maisha yao kwa ujumla.

095a5b996f7db11bfe3b1d93a17b444b.0Kila wakati, unayo nafasi nzuri sana ya kutoa mazuri katika dunia, ingawa uamuzi ni wako. Acha kutenda au kusema mara moja kile kinachokujia kichwani mwako, Jipe muda wa kukifikiri kitu hicho na kujua ni nini matokeo yake katika maisha yako na ya wengine.

Kama wewe ni kiongozi unatakiwa kujua, hatua unazo chukua au hatuautakazochukua zitasaidia vipi kuweza kuwajenga wale unawaongoza na badala ya kuwabomoa. Kile unachokitenda kina umuhimu mkubwa sana kwako.

Kama wewe ni mwandishi, andika si kwa sababu unaweza kuandika, jiulize kile unachokiandika kina msaada vipi kwa watu, kitu hicho kinajenga vipi maisha ya watu wanaokuzunguka na kuyafanya yawe bora kabisa.

Kama wewe ni mwimbaji, usiimbe tu kwa sababu una mdomo, kumbuka kazi zako zitadumu siku hadi siku, sasa kwa nini uharibu kizazi chako cha leo na kesho kwa sababu ya maamuzi uliyachukua leo?

Hapo ulipo uwe mzazi, uwe daktari au uwe mtu yeyote mwenye wadhifa wowote hapa duniani kuna kitu ambacho unakitenda iwe kwa maneno au kwa njia yoyote ile. Jiulize kitu hicho unakitenda kwa chanya kiasi gani?

Lengo lako ambalo unapswa kulitambua na kulijua ni kuhakikisha kila kitu ukitendacho kiwe chanya, yaani kiwe msaada mkubwa kwa wengine na si kuvuruga wengine. Kuharibu maisha yaw engine ni kitu mbaya sana na haikubaliki kwa vyovyote vile.

Kuwa tabibu wa maisha ya wengine kwa kutenda mambo chanya. Ukiwasadia watu wengine, na wakaona maisha yao yanakuwa mazuri, basi elewa wewe utakuwa nawe ni moja ya watu wenye mafanikio mkubwa sana duniani.

Kuanzia leo jifunze kutoa yale mazuri katika hii dunia, jenga utamaduni wa kutoa yale matendo au maneno mazuri iwe sehemu ya utamaduni wako. Ukifanya hivyo dunia itakupa mazuri pia na utafurahia  maisha yako kutokana na mazuri unayoyatoa.

Simama imara katika kuhakikisha hili unalitenda. Kumbuka sana toa yale mazuri katika maisha yako,  give goodness to life, ukifanikisha hili furaha na mafanikio vitakuwa upande wako.

Fanyia kazi haya na pia nakutakia 2018 yenye mafanikio makubwa katika maisha yako.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,

Ni wako rafiki katika mafanikio,

Imani Ngwangwalu,

Mshauri wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali,

Tovuti; www.amkamtanzania.com

Mawasiliano; +255 767 048 035, +255 713 048 035,

Email; dirayamafanikio@gmail.com