Rafiki yangu mpendwa,

Watu wengi hufikiri kwamba kitu kinachowazuia wasifanikiwe ni mambo yaliyo nje ya uwezo wao. Wengi wanalaumu mazingira, hali ya hewa, hali ya uchumi, serikali, wazazi, ndugu na hata jamaa na marafiki.

Lakini ukweli ni kwamba, sehemu kubwa ya kinachokuzuia wewe kufanikia kipo ndani yako na siyo nje yako. Tunaweza kusema wewe mwenyewe ndiye unayejizuia kufanikiwa. Kama utafanyia kazi maeneo muhimu yaliyopo ndani yako, hakuna kitu cha nje kitakachokuzuia wewe kufanikiwa.

Rafiki, pia nikukumbushe kwamba mafanikio ni kufanya na siyo kupanga. Chochote unachofanya, nje ya kufanya ni kupoteza muda, ni kukwepa kufanya. Kwa mfano kama unajiambia unajiandaa, kama unajiambia unasubiri uwe tayari, kama unajiambia kuna kitu unasubiri, jua ya kwamba unakwepa kufanya, na hilo litakuzuia au kukuchelewesha wewe kufanikiwa.

KURASA ZA MAISHA YA MAFANIKIO

Kanuni yetu ya mafanikio makubwa, ambayo ni MAARIFA SAHIHI + KUCHUKUA HATUA KUBWA = MAFANIKIO MAKUBWA, ni kanuni inayofanya kazi wakati wote, kama utaitumia kwa usahihi.

Kama utapata maarifa lakini usichukue hatua, unajidanganya tu, na maarifa hayo yanakuwa mzigo kwako. Na kama utachukua hatua bila ya kuwa na maarifa sahihi unapoteza nguvu zako.

Kwenye makala hii ya leo, nakwenda kukushirikisha kwenye kuchukua hatua, na kuna maeneo manne muhimu ya kufanyia kazi ili uweze kufikia ndoto zako kubwa na kufanikiwa sana. Bila ya kufanyia kazi maeneo haya manne, ambayo yote yapo ndani ya uwezo wako, hakuna chochote cha nje kitakachoweza kukusaidia.

ENEO LA KWANZA; PUNGUZA KUFANYA.

Eneo la kwanza unalopaswa kufanyia kazi kwenye maisha yako ni kupunguza kufanya baadhi ya vitu unavyofanya sasa. Katika vitu unavyofanya sasa, kuna ambavyo unavifanya kupitiliza, kiasi kwamba unakosa muda na nafasi ya kufanya vingine ambavyo ni muhimu pia.

Hivyo unahitaji kukaa chini na kuangalia kila unachofanya, kinachochagia kufanya na kujiuliza kipi unafanya sana, ambacho ukipunguza kufanya hakitakuwa na madhara, lakini pia utaweza kufanya vingine muhimu.

ENEO LA PILI; ONGEZA KUFANYA.

Eneo la pili la kufanyia kazi ni kuongeza kufanya baadhi ya vitu unavyofanya kwa uchache sana, lakini ambavyo ni muhimu sana kwa mafanikio yako. Hapa unaweka sawa vipaumbele vyako na hivyo kuweza kufanya zaidi yale ambayo ni muhimu zaidi.

Orodhesha yote unayofanya na kule unakokwenda, kisha angalia ni hatua zipi muhimu unazopaswa kuchukua lakini unachukua kwa kiwango kidogo. Ongeza kiwango cha hatua hizo na utaweza kupiga hatua sana kwenye maisha yako.

SOMA; Sababu Tatu Kwa Nini Mafanikio Madogo Yanakuwa Sumu Ya Wewe Kufikia Mafanikio Makubwa Zaidi Na Jinsi Ya Kuziepuka.

ENEO LA TATU; ACHA KUFANYA.

Eneo la tatu la kufanyia kazi ni kuacha kufanya baadhi ya vitu ambavyo haviendani na kule unakotaka kufika. Katika vitu unavyofanya sasa, kuna ambavyo vinapingana na kule unakokwenda, vitu hivyo vipo kinyume kabisa na ndoto zako. Hivi ni vitu ambavyo unapaswa kuacha kuvifanya mara moja ili uweze kufikia ndoto zako.

Orodhesha kila unachofanya, kisha jiulize kipi ambacho hakichangii wewe kufikia ndoto zako, na acha kukifanya.

ENEO LA NNE; ANZA KUFANYA.

Eneo la nne la kufanyia kazi ili kufikia ndoto zako ni kuanza kufanya baadhi ya vitu ambavyo mpaka sasa hujaanza kufanya. Ili kufikia ndoto zako, kuna vitu ambavyo lazima uvifanye, lakini huenda wewe hujaanza kuvifanya. Sasa usiendelee kujidanganya, badala yake anza kufanya, hata kama ni vigumu au unaona huwezi, wewe anza kufanya.

Jua kila kilicho muhimu kwako kufanya ili kuweza kufikia ndoto zako kubwa, na angalia nini ambacho hujaanza kufanya sasa na anza kukifanya.

Hayo ndiyo maeneo manne muhimu ya kufanyia kazi kwenye maisha yako ili kuweze kufikia ndoto kubwa za maisha yako.

Dhana hii pia unaweza kuitumia kwenye maeneo mengine ya maisha yako, kama watu unaochagua wakuzunguke, kuna watu inabidi upunguze muda unaokaa nao, wengine uongeze muda unaokaa nao, wengine uache kabisa kukaa nao na wengine uanze kukaa nao.

Kila siku angalia ni hatua zipi muhimu kwako kuchukua ili kusogea karibu na ndoto yako. Na zipo hatua nyingi nzuri za kuchukua iwapo utakuwa mfuatiliaji wa karibu na una kiu ya kufikia ndoto zako.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; http://eepurl.com/dDZHvL

Usomaji