Rafiki yangu mpendwa,
Mwandishi na mshauri wa mambo ya kifedha, Robert Kiyosaki amewahi kuandika kwamba kuna matatizo mawili kwenye fedha. Tatizo la kwanza ni kutokuwa na fedha, na tatizo la pili ni kuwa na fedha. Wengi hufikiri tatizo lao kwenye fedha ni la kwanza, yaani hawana, lakini subiri mpaka wanapopata fedha ndiyo wanagundua hawakuwa na maandalizi ya kutosha, kwa sababu wanazipoteza zote na wasione nini wamefanya.
Karibu kwenye makala ya ushauri wa changamoto mbalimbali ambazo zinatuzuia kufikia mafanikio makubwa. Kwenye makala ya leo tunakwenda kuangalia jinsi ya kuituliza kila fedha inayopita kwenye mikono yako ili uweze kujijengea utajiri na uhuru wa kifedha.
Msomaji mwenzetu ametuandikia hili katika kuomba ushauri;
Kiukweli Mimi napata sana shida nikiwa na hela nakosa pa kupeleka na pia nakosa matumizi natamani nitunze lakini nashindwa. Kwa hiyo nilikuwa naomba ushauri naweza kuwekeza wapi huku naendelea kusoma kwa sababu Niko kidato cha 6. Nitashukuru kama utanisaidia. Mura K. N.
Kama alivyotuandikia Mura, wapo watu wengi ambao wanakuwa na mipango mizuri sana kabla hawajawa na fedha, wanajua kabisa wakipata fedha watafanya nini na nini. Na tena watawashangaa sana wale wanaopata fedha na kuzitumia vibaya. Lakini subiri watu hao hao wazipate fedha, mipango yote inayeyuka, fedha zinatumika hovyo na mpaka zinapoisha ndiyo akili zinawarudia.
Kitu kimoja ambacho nataka kushauri leo kwa wale wote wenye shida ya kukaa na fedha, ni hiki; ACHA KUWA KARANI WA FEDHA ZAKO.
Watu wengi linapokuja swala la fedha, hawana tofauti na makarani, ambao wanapokea fedha na kuzipelekeka zinapopaswa kwenda. Ukienda benki kuweka fedha na ukamkabidhi karani wa benki fedha zako, utaona kama anashika fedha nyingi, lakini mwisho wa siku fedha hizo habaki nazo yeye, bali anakabidhi zinapohusika.
Sasa watu wengi wamekuwa wanayaishi maisha yao kama makarani wa fedha zao. Kinachotokea ni hiki, mtu anafanya kazi au biashara na analipwa mshahara au kupata faida kama kipato chake. Anachukua kipato hicho na kwenda kulipia vitu na kununua vitu mbalimbali. Mwisho anabaki hana fedha kabisa.
Alichokifanya mtu huyu ni kuchukua fedha kwenye kazi au biashara na kwenda kuitoa kwa wale wanaomdai au wanaouza vitu mbalimbali. Mwisho wa siku anabaki hana hata senti moja.
SOMA; Sheria Tano Za Fedha Unazopaswa Kuzijua Na Kuzisimamia Kama Unataka Kuondoka Kwenye Umasikini.
Acha mara moja kuwa karani wa fedha zako, kwa kuzihamisha kutoka unakozipata na kuzipeleka kwenye matumizi na wewe kubaki huna kitu.
Na ipo njia moja rahisi kwako kuacha kuwa karani wa fedha zako, njia hiyo ni KUJILIPA WEWE MWENYEWE KWANZA.
Kwa kila kipato unachoingiza kwenye maisha yako, kabla hujapeleka kwenye matumizi yoyote, toa sehemu ya kipato hicho na iweke pembeni. Sehemu hiyo ya kipato uliyoitoa ndiyo malipo yako kwako na hupaswi kuitumia kwa shughuli nyingine yoyote ya matumizi. Hichi ni kipato ambacho utakiwekeza zaidi ili uweze kufanikiwa zaidi.
Sasa najua ni vigumu kukaa na fedha, kwa sababu kama wanavyosema watu, fedha huwa hazikosi matumizi. Ukishakua na fedha, dunia itahakikisha unazitumia kwa namna yoyote ile. Hivyo vitu vitaharibika, watu wataumwa utashangaa unapokuwa na fedha ndiyo unapokea simu nyingi zikitaka utoe msaada fulani.
Hivyo kuna njia nyingine bora kabisa ya kuhakikisha kile unachojilipa hakipati matumizi na ukakipoteza. Njia hiyo ni KUJENGA GEREZA LA AKIBA YAKO. Kile kiasi ambacho unajilipa wewe mwenyewe, kitengenezee gereza, ambapo ukishaingiza, huwezi kutoa tena, hata itokee nini. Hata uwe na dharura kiasi gani, gereza hilo halikuruhusu uondoe fedha ulizoweka.
Gereza la fedha zako ni mfumo wowote unaokuruhusu kuweka fedha lakini kutoa inakuwa siyo rahisi. Na unaweza kufanya hivyo kwa kuwa na akaunti maalumu ya benki ambayo inakuruhusu kuweka lakini siyo kutoa. Unaweza pia kufanya uwekezaji wa moja kwa moja ambao utafanya kupata fedha yako kuchukue muda. Lakini pia unaweza kuweka mpango na mtu au watu wengine, na mkawa mnaweka fedha lakini hamtoi.
Angalia njia inayokufaa wewe, ambapo ukiweka fedha, inakuwa vigumu sana kwako kuitoa, na hilo litakusaidia kujiwekea fedha zako kulingana na mipango uliyonayo.
Hivyo nimalize kwa kukumbusha mambo muhimu sana tuliyojadili hapa;
ACHA KUWA KARANI WA FEDHA ZAKO.
JILIPE WEWE MWENYEWE KWANZA.
TENGENEZA GEREZA LA FEDHA ZAKO.
Fanya hayo matatu na fedha yako itaweza kutulia, na utaweza kufanya makubwa. Ukishaweza kuituliza fedha yako, utaweza kuiwekeza na kupitia uwekezaji ndiyo utaweza kufikia utajiri na uhuru wa kifedha.
Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog