Rafiki yangu mpendwa,

Juma jingine la mwaka huu 2018 linakwenda chini leo, na juma jingine linakwenda kuibuka.

Majuma yataendelea kukatika hivi kila siku, na wewe ni labda utakuwa unaenda mbele au unarudi nyuma.

Kumbuka kwenye maisha hakuna kusimama, hata kama unajiona umesimama, jua ya kwamba unarudi nyuma. Kama huendi mbele basi unarudi nyuma. Kwa sababu unapokuwa umesimama, dunia inaendelea kwenda.

Nikupe mfano labda unafanya kazi ambayo umezoea kuifanya, kwa viwango ulivyozoea kufanya na unatengeneza kipato kidogo. Unaweza kuendelea kwa kazi hiyo kwa mazoea, ukiona upo pale pale, lakini napenda kukuambia ya kwamba unachofanya ni kurudi nyuma.

Kwa sababu muda unakwenda na nguvu zako zinapungua. Mwaka mmoja ujao kutoka leo umri wako utakuwa umeongezeka zaidi na nguvu zako kupungua zaidi. Hivyo yale unayoweza kuyafanya leo kwa ubora, hutaweza kuyafanya hivyo miaka ijayo.

Hivyo rafiki, kilio changu kwako mara zote ni hichi, weka juhudi zaidi, jitume zaidi, nenda hatua ya ziada, fanya zaidi kwa sababu dunia inakwenda kwa kasi sana, usipokuwa kasi, unaachwa nyuma na ukiachwa nyuma, maisha yako yanakuwa magumu zaidi ya yanavyopaswa kuwa.

MASAA MAWILI YA ZIADA

Rafiki, karibu kwenye TANO ZA JUMA, makala ambayo nakukusanyia mambo matano muhimu sana ya juma zima, ambayo kuna mengi ya kujifunza na hatua za kuchukua ili uweze kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi.

Jipe muda wa kusoma tano hizi za juma, tafakari namna kila kimoja unaweza kukitumia kwenye maisha yako, kisha chukua hatua.

#1 KITABU NILICHOSOMA; MISINGI MIKUU MINNE YA UWEKEZAJI.

Rafiki, moja kati ya vitabu nilivyosoma juma hili, ni kitabu kinachoitwa CHARLIE MUNGER; THE COMPLETE INVESTOR, ambacho kimeandikwa na Tren Griffin.

Tukianza na utangulizi mfupi, Charlie Munger ni mmoja wa wawekezaji wenye mafanikio makubwa sana duniani. Ni mshirika wa karibu wa Warren Buffett, mwekezaji namba moja duniani, na wamekuwa wanafanya kazi pamoja kwa zaidi ya miaka 50 sasa.

Warren Buffett anasema kama siyo Charlie Munger, huenda asingeweza kupata mafanikio makubwa aliyoyapata kwenye uwekezaji. Kwa sababu Charlie amekuwa ni mtu mwenye kudadisi sana uwekezaji kabla ya kuchukua hatua. Warren anakiri kuna uwekezaji aliwahi kufanya kabla ya kujadiliana na Munger na alipata hasara kubwa sana.

Munger ni mmoja wa watu ambao wamejenga msingi wao wameujenga kwenye maarifa na hekima. Munger anaamini sana katika kujifunza, siyo tu kwenye lile eneo ambalo mtu unafanyia kazi, bali kwenye maeneo mengine pia.

Munger ana mfumo wake anaouita MENTAL MODELS, ambapo anasema ili kuweza kufanya maamuzi sahihi, lazima uweze kufikiri kwa mifumo mbalimbali. Lazima uweze kutumia mifumo tofauti na kile unachofanyia kazi. Kwa mfano kwenye uwekezaji, lazima uweze kufikiria kama mwanahisabati, mwanafizikia, mwanasaikolojia, mwanahistoria, mwanabaiolojia na mwanafalsafa.

Kama kuna kitu kikubwa ambacho jamii yetu ya sasa imebarikiwa kuwa nacho, basi ni kuwa na watu kama kina Munger, ambao wanatumia kujifunza kama njia ya kuweza kufanya maamuzi sahihi na kufanikiwa pia. Munger na Buffett wanasema kazi yao kubwa kwenye siku ni kusoma na kujifunza. Watoto wa Munger wanasema baba yao ni kitabu kinachotembea, maana anatumia muda mwingi kwenye kusoma na kujifunza kuliko kwenye jambo jingine lolote.

Mwandishi Tren Griffin ametuchambulia kwa kina falsafa ya maisha na uwekezaji ya Munger, ambapo yapo mengi sana ya kujifunza. Kitabu hiki kimeeleza mfumo wa uwekezaji na ufanyaji maamuzi anaotumia Munger pamoja na Buffett. Pia ametuonesha jinsi ambavyo wamekutana na changamoto mbalimbali na jinsi walivyojifunza na kuweza kuzivuka.

Kwenye makala hii, nakwenda kukushirikisha maeneo matatu muhimu sana ya kufanyia kazi ili kufanikiwa kwenye biashara, uwekezaji na hata maisha kwa ujumla. Maeneo hayo ni; MISINGI MIKUU MINNE YA UWEKEZAJI, MAKOSA 25 YA KISAIKOLOJIA TUNAYOFANYA NA YANATUGHARIMU na MAMBO NANE YA KUZINGATIA ILI KUFANIKIWA KWENYE UWEKEZAJI.

MOJA; MISINGI MIKUU MINNE YA UWEKEZAJI.

Charlie Munger na Warren Buffett wanatumia mfumo wa uwekezaji ulioasisiwa na Ben Braham ambaye alikuwa mwekezaji na mwalimu wa Warren Buffett. Graham pia ndiye aliyeandika kitabu cha THE INTELIGENT INVESTOR, kitabu cha msingi na muhimu sana kwenye uwekezaji.

Kupitia mfumo wa uwekezaji wa Braham, ipo misingi mikuu minne, ambayo Munger anasema kamwe haiwezi kupitwa na wakati. Mwekezaji anayezingatia misingi hii anafanikiwa, wakati anayeipuuza anashindwa.

Msingi wa kwanza; chukulia hisa unayonunua kama umiliki wa biashara.

Graham anasema unapowekeza kwa kununua hisa, kitu cha kwanza kabisa unachopaswa kukijua ni kuelewa biashara ambayo kampuni unayonunua hisa zake inafanya. Kama huwezi kuelewa biashara inayofanyika, usinunue hisa za kampuni hiyo.

Munger anaamini sehemu ya kuanzia kwenye uwekezaji ni kuelewa misingi ya biashara husika. Biashara hiyo inauza nini, wateja wake ni watu gani na washindani wake ni wapi? Baada ya hapo anahitaji kujua jinsi ambavyo biashara inaendeshwa na faida inayoingiza.

Mfumo huu wa Graham unahitaji muda na kazi, na ndiyo maana wachache sana wanafanikiwa kupitia mfumo huu. Wengi wamekuwa wanawekeza kwa kufuata mkumbo na siyo kuelewa biashara inayofanyika.

Mfumo wa Graham unaepuka sana kutabiri mwenendo wa biashara wa siku za baadaye. Kwa sababu hakuna utabiri ulio sahihi.

Msingi wa pili; nunua kwa bei ya chini ukilinganisha na thamani halisi ili kuwa na wigo wa usalama.

Msingi wa pili wa Graham ni kutengeneza wigo wa usalama wakati wa kununua. Unapokuwa unanunua hisa au kuwekeza popote, unapaswa kununua kwa bei ya chini kuliko thamani halisi. Hii inakupa wigo mpaka wa kutokupata hasara.

Kwa mfumo wa Graham, faida unaipata wakati wa kununua na siyo wakati wa kuuza.

Munger anaamini kwamba ili kufanikiwa kwenye uwekezaji, lazima ununue hisa au uwekezaji kwa bei ya chini sana kiasi kwamba huwezi kupata hasara.

Hivyo Munger pamoja na Buffett wamekuwa wakijisifu kwa kitu kimoja, siyo wanunuaji wa kila aina ya hisa au kampuni. Huwa wanatafiti kila aina ya hisa na kampuni, na kupiga hesabu ya thamani halisi ya kampuni na thamani ya kununua. Kama bei ya kununua iko chini ya thamani halisi, basi wananunua kwa wingi. Kama bei ni juu wanaachana nayo, hawanunui.

Munger anasema kinachowafanya wao kufanikiwa kwenye msingi huu wakati wengine wanashindwa, ni kuwa na subira. Anasema wawekezaji wengi hawana subira kwenye kutafuta uwekezaji bora, hivyo wanajikuta wananunua uwekezaji ambao bei ya kununua ni kubwa kuliko thamani yake halisi.

Msingi wa tatu; lifanye soko kuwa mtumwa wako na siyo wewe kuwa mtumwa wa soko.

Mfumo wa Graham unaelea kwamba soko huwa halitulii, huwa linapanda na kushika, mara kwa mara. Wawekezaji wengi huwa wanakuwa watumwa wa soko. Pale soko linapopanda wengi wanakimbilia kununua, hivyo wananunua kwa bei juu, na pale soko linaposhuka wengi wanakimbilia kuuza, na hivyo wanauza kwa bei ya chini. Hivyo kinachotokea ni hasara, unanunua bei juu na kuuza kwa bei ya chini.

Ili kufanikiwa kwenye uwekezaji, lazima ulifanye soko kuwa mtumwa wako, na kuacha kuendeshwa na kupanda au kushuka kwa soko.

Munger na Buffett wamekuwa wanaenda kinyume na soko na wawekezaji wengine, pale soko linaposhuka na watu wanakimbilia kuuza, bei zinashuka sana, na hapo wao ndiyo wananunua, hivyo wananunua kwa bei ndogo mno. Soko linapopanga na bei zinakuwa juu, wanaacha kununua na wanaamua kuuza au kutulia na uwekezaji waliofanya. Kwa njia hii wanapata faida kubwa.

Munger anasema huu ni mfumo rahisi sana kueleweka na yeyote anaweza kufanya, ila anasema wengi hawawezi kutulia pale soko linapoanguka, hasa kwa kasi, wanakimbilia kuuza ili wasipate hasara kabisa. Munger anatoa mifano mingi ya jinsi walivyonufaika kwenye vipindi vya anguko la soko la hisa kama mwaka 2000 na mwaka 2009, wakati kila mtu alikuwa ametaharuki na kukimbilia kuuza, wao walikuwa wananunua. Hivyo waliweza kununua hisa nyingi mno kwa bei sawa na bure.

Ili uweze kutumia msingi huu, lazima ujue na kuamini kwamba kwa muda mrefu, thamani ya soko la hisa inakwenda juu. Ndani ya muda mfupi soko linaweza kupanda na kushuka, lakini kwa muda mrefu, mfano ukichukua miaka kumi, thamani kwa ujumla inakuwa imepanda.

Msingi wa nne; tumia mantiki, kuwa na malengo na usiendeshwe kwa hisia.

Mfumo wa uwekezaji wa Graham unatambua udhaifu mmoja ambao unawazuia watu kufanikiwa kwenye uwekezaji. Udhaifu huo ni kufanya maamuzi kwa kusukumwa na hisia na siyo kufikiri kwa kina.

Munger anasema unapaswa kuweza kufikiri kwa kina na kufanya maamuzi sahihi na siyo kuendeshwa na hisia zako mwenyewe au za wengine.

Kitu cha kwanza ambacho unapaswa kukifanya ili kufanikiwa kama mwekezaji ni kujifunza kufikiri kwa akili yako mwenyewe. Usikubali kushikiwa akili, usifanye maamuzi kwa sababu kila mtu anafanya. Fikiri kwa kina, na jua nini unataka ndipo uweze kufanya maamuzi sahihi kwako. Na hata kama maamuzi yako yanakwenda kinyume na wengine usiogope. Kwenye mambo mengi katika maisha, kuwa kwenye kundi kubwa ni kupotea.

MBILI; MAKOSA 25 YA KISAIKOLOJIA TUNAYOFANYA NA YANATUGHARIMU.

Kama wanadamu huwa tunatengeneza sheria za kufanya maamuzi ambazo zinatusaidia kuvuka changamoto mbalimbali na kupata tunachotaka. Lakini sheria hizi hizo tunazojitengenezea, huwa zina madhaifu ambayo yanatupelekea kufanya makosa kwenye maamuzi mbalimbali.

Munger amekuwa anachambua makosa 25 ya kisaikolojia ambayo binadamu huwa tunafanya na yanatugharimu. Anasema tukiyajua haya na kuyaepuka, tutaweza kufanya maamuzi bora sana kwenye maisha yetu na kupunguza kukosea.

Yafuatayo ni makosa 25 ya kisaikolojia ya kuyaepuka ili kuepuka kufanya makosa kwenye maamuzi yetu;

  1. Zawadi na adhabu, huwa tunapenda kufanya kile ambacho tunazawadiwa kufanya na kuepuka kile tunachoadhibiwa. Unapoomba ushauri kuhusu fedha na uwekezaji kwa mtu, jiulize je jibu analokupa linampa yeye zawadi gani. Kama jibu analokupa linamfanya yeye apate zawadi, jua siyo jibu sahihi kwako, bali ni sahihi kwake ili apate zawadi.
  2. Makosa ya kupenda, wengi tunapopenda kitu au mtu huwa hatuoni mapungufu yake, hili ni kosa kubwa kwenye uwekezaji. Weka mapenzi pembeni na ona uhalisia ulivyo.
  3. Makosa ya kutokupenda, ni tabia ya binadamu kupuuza kile ambacho hatukipendi, wakati mwingine unakosa fursa nzuri kwa kupuuza kitu kwa sababu tu hukipendi.
  4. Kosa la kuepuka mashaka, mara nyingi watu wamekuwa wanaamini kitu kama kilivyo ili tu kuepuka kuwa na mashaka juu ya kitu hicho. Na hili limekuwa linawafanya watu wasihoji kitu kinachopelekea kufanya makosa kwenye maamuzi.
  5. Kosa la kuepuka kutokuwa na msimamo. Watu wanapenda kuwa na msimamo, hawapendi kubadilika mara kwa mara. Epuka kuendelea na kitu kwa sababu umeshakifanya, kuwa tayari kubadilika wakati wowote unapopata taarifa sahihi zaidi ya ulizokuwa nazo mwanzo.
  6. Kosa la udadisi. Watu wengi huwa wanakuwa na udadisi, lakini udadisi huu unaweza kuwaondoa kwenye yale muhimu kwao. Hivyo unapaswa kuwa makini udadisi wako usikutoe kwenye yale muhimu kwao.
  7. Kosa la kutaka usawa. Huwa tunapenda sana kuwepo kwa usawa, lakini siyo mara zote usawa una manufaa. Kuna wakati utahitajika kunufaika zaidi au kuumia zaidi ya wengine.
  8. Kosa la wivu, binadamu huwa tunasukumwa sana na hisia za wivu, hasa pale tunapoona wengine wananufaika kuliko sisi. Munger anasema hii ndiyo sababu kuu masoko ya hisa huwa yanaanguka, pale mtu mmoja anapopata faida, wengine nao wanataka wapate faida pia hata kama alichofanya aliyepata faida siyo sahihi.
  9. Kosa la kulipa fadhila. Kama binadamu, huwa tunapenda kulipa fadhila, mtu akitufanyia kitu kizuri, tunakuwa na deni la kumfanyia kitu kizuri pia. Kuna watu wanatumia kosa hili kunufaika kupitia wewe, mtu anakupa kitu kidogo, halafu baadaye anakuomba kikubwa, kwa kuwa umeshapokea kidogo unaona una deni, hivyo unatoa kikubwa na unapoteza zaidi.
  10. Kosa la kuamini kwa kujua au kupenda. Huwa tunawaamini sana wale watu ambao tunawajua au tunawapenda. Ndiyo maana matangazo mengi huwa yanatumia watu maarufu, kwa sababu watu wanawapenda watu maarufu. Sasa kuonekana kwa mtu maarufu kwenye tangazo la kitu fulani, haimaanishi anakitumia, hivyo usinunue kwa sababu mtu maarufu ameonekana kwenye tangazo.
  11. Kosa la kukataa ukweli unaoumiza. Watu huwa hawapendi ukweli unaoumiza, hivyo wanachofanya ni kukataa kwamba ukweli huo haupo. Kuwa tayari kupokea ukweli hata kama unaumiza, itakusaidia kuepuka kufanya makosa zaidi.
  12. Kosa la kujiamini kupitiliza. Watu wengi wanapofanikiwa kidogo, huwa wanashindwa sana baadaye, kwa sababu mafanikio kidogo wanayopata yanawafanya wajiamini kupitiliza. Wanajaribu vitu ambavyo vipo nje ya uwezo wao na kushindwa vibaya. Usijiamini kupita uwezo wako, jua uwezo wako uko wapi na kazana na maeneo unayoyaweza, mengine achana nayo.
  13. Kosa la matumaini yaliyopitiliza. Kuwa na matumaini ni kuzuri, lakini kuwa na matumaini yaliyopitiliza ni hatari kubwa kwenye maisha na hata uwekezaji. Kwa sababu mambo yanaweza kuwa mabaya na yameshapitiliza hivyo unapaswa kukubali hasara na usonge mbele, lakini kwa kuwa na matumaini yaliyopitiliza unaendelea kukomaa ukiamini mambo yatakuwa mazuri tu, kitu ambacho hakipo.
  14. Kosa la kuogopa kupoteza. Binadamu tunaongozwa na tamaa mbili, kutaka kupata na kuogopa kupoteza. Hisia za kuogopa kupoteza huwa ni kubwa sana, kwa mfano ukipewa fursa ambayo unaweza kupata laki moja, lakini pia unaweza kupoteza laki moja, utaikataa. Kwenye uwekezaji, hofu ya kupoteza ndiyo imekuwa unawafanya watu kununua hisa kwa bei juu na kuuza kwa bei chini.
  15. Kosa la kufuata wengine. Sisi kama binadamu huwa tunapenda kuwa ndani ya kundi hivyo kama kitu kinafanywa na wengi, huwa tunaona ni salama kufanya, kwa sababu tunaamini wengi hawawezi kukosea. Ukweli ni wengi wanakosea na wanakosea sana, hivyo epuka kufanya kitu kwa sababu tu wengine wanafanya.
  16. Kosa la kulinganisha vitu. Huwa tuna tabia ya kulinganisha vitu, kisha kuchagua kile ambacho ni afadhali. Hili linaweza kutuletea hasara kubwa. Mfano kama unataka kununua kitu, mtu anaanza kukuonesha kitu ambacho siyo kizuri sana lakini cha bei kubwa, kisha anakuonesha kitu kingine cha bei nafuu, utanunua hicho ulichoambiwa ni cha bei nafuu kwa kulinganisha na cha bei ghali, wakati huenda hiyo unayoambiwa ni bei nafuu, kwingine ni chini zaidi ya hapo.
  17. Kosa la kusukumwa na msongo, unapokuwa na msongo, uwezo wako wa kufanya maamuzi sahihi unakuwa mdogo. Hivyo unaposukumwa na msongo kufanya maamuzi, jua kabisa unafanya maamuzi ambayo yatakuumiza baadaye.
  18. Kosa la kutumia kumbukumbu za karibuni. Maamuzi yetu huwa yanashawishiwa sana na kumbukumbu za karibuni. Kama ulifanikiwa kwenye kitu fulani siku za karibuni, utakuwa tayari kukifanya tena, na kama ulishindwa utakiepuka. Ili kuweza kuziona fursa kwa usahihi, lazima uache kutumia kumbukumbu za karibu na kufikiri kwa kina.
  19. Dhana ya kutumia au kupoteza. Chochote unachojifunza, kama hutakitumia, basi jua utakipoteza. Kwenye uwekezaji, siyo kitu cha kufanya mara moja halafu unasahau. Lazima utenge muda wa kufuatilia uwekezaji kwa kina ili kuwa mwekezaji mzuri.
  20. Kosa la kusukumwa na ulevi. Ulevi wa aina yoyote ile, unaharibu uwezo wako wa kufikiri kwa kina na kufanya maamuzi sahihi. Epuka sana ulevi kwenye maisha yako, una hasara kubwa na faida ni kidogo mno.
  21. Kosa la kusingizia umri. Watu wengi umri unavyokwenda, ndivyo wanavyozidi kuzorota na kila kitu wanasingizia umri. Ingawa ni kweli mwili unachoka kadiri umri unavyokwenda, lakini bado unaweza kukazana na kufanya vizuri kama utaacha kusingizia umri.
  22. Kosa la kuamini mamlaka bila kuhoji. Watu wengi huwa wanaamini watu wenye mamlaka bila ya kuhoji, hivyo kuwa tayari kufanya kile wanachoambiwa na wenye mamlaka bila ya kuhoji. Wengi wamekuwa wanajipa mamlaka fulani ili kupata kile wanachotaka kutoka kwa wengine.
  23. Kosa la kuonekana unafanya kitu. Binadamu huwa hatupendi kuonekana tumekaa tu na hatuna tunachofanya. Hivyo watu wamekuwa wanafanya vitu ambavyo havina hata maana ili tu waonekane nao wanafanya. Hili limepelekea wengi kupata hasara, hasa kwenye uwekezaji, kwa kushindwa kukaa na kutulia na uwekezaji ambao wameshafanya.
  24. Kosa la kuamini sababu. Watu wengi huwa wanaamini sababu wanazopewa, hata kama siyo sababu sahihi. Mtu anaweza kuombwa kitu, kwa kupewa sababu ambayo haihusiki na bado wakaiamini. Mfano kwenye uwekezaji watu wengi wamekuwa wanatumia sababu ambazo hazina uhusiano wowote na uwekezaji, na bado wengi wanaziamini. Usiamini haraka kila sababu unayopewa, dadisi na chimba ndani, utagundua siyo sababu zote ni sahihi.
  25. Dhana ya muunganiko wa sababu mbalimbali. Matokeo ambayo wengi wanayapata kwenye maisha, hayatokani na kitu kimoja, bali muunganiko wa vitu mbalimbali. Mtu anayefanikiwa siyo kwa sababu tu anaweka juhudi, zipo sababu nyingine nyingi. Kadhalika kwa anayeshindwa. Kwenye dhana na makosa haya ya kisaikolojia, mengi yanaweza kuungana kwa pamoja na kusababisha kushindwa sana.

TATU; MAMBO NANE YA KUZINGATIA ILI KUFANIKIWA KWENYE UWEKEZAJI.

Ili uweze kufanikiwa kwenye uwekezaji, yapo mambo nane muhimu sana unayopaswa kuyazingatia.

Moja; jua thamani halisi ya biashara au hisa kabla ya kununua. Na nunua kwa bei ambayo ipo chini ya thamani halisi.

Mbili; jua wigo wa usalama ulionao kabla ya kununua. Unahitaji kununua kwa bei ambayo itakuwa vigumu kwako kupata hasara, hata kama bei haitapanda.

Tatu; jua wigo wako wa umahiri na ujuzi, huwezi kujua kila kitu, hivyo kazana na yale maeneo unayojua na achana na mengine.

Nne; jua kiwango sahihi kwako kununua, wengi hupenda kununua hisa chache za makampuni mengi, wengine wanapenda kununua hisa nyingi za makampuni machache. Kama utatumia namba tatu hapo juu, kwa kujua umahiri wako, nunua hisa nyingi za makampuni machache unayoyajua kwa undani.

Tano; jua ni wakati gani sahihi kwako kuuza. Wapo wanaouza pale bei inapopanda, wengine hawauzi kabisa.

Sita; jua kiasi cha hatari ambacho upo tayari kuchukua. Kila uwekezaji una hatari yake, hivyo kuna nafasi ya kupoteza kwenye kila uwekezaji, jua kiwango ambacho wewe upo tayari kupoteza ili uweze kuwekeza vizuri.

Saba; amua kama utazingatia ubora wa biashara, wapo wawekezaji ambao wanaangalia faida tu, hawaangalii ubora wa biashara. Wapo ambao wanaangalia ubora wa biashara, jua kipi unajali zaidi, ubora au faida.

Nane; amua ni aina gani ya biashara unataka kumiliki, aina ya biashara unayochagua kuingia ina mchango mkubwa kwenye mafanikio yako kama mwekezaji. Kuna biashara ambazo ni rahisi na zina ushindani mkubwa, na zipo biashara ngumu zenye ushindani mdogo.

Rafiki, haya ni machache sana kati ya mengi ya kujifunza kuhusu maisha na uwekezaji kutoka kwa mwekezaji Charlie Munger, jifunze haya kwa kina na fanyia kazi kwenye maisha yako ili kuweza kufanya maamuzi sahihi kwenye kazi, biashara, uwekezaji na hata maisha kwa ujumla.

#2 MAKALA YA JUMA; NJIA YA UHAKIKA YA KUWASHAWISHI WATEJA KUNUNUA.

Rafiki yangu, juma hili nilikushirikisha makala ya njia moja ya uhakika ya kumshawishi mteja kununua chochote unachouza. Watu wengi wana bidhaa na huduma nzuri, lakini wanakosa ushawishi na hivyo kushindwa kuuza.

Kama hukupata nafasi ya kusoma makala hiyo, unaweza kuisoma hapa; Hii Ndiyo Njia Moja Ya Uhakika Ya Kuwashawishi Wateja Kununua Chochote Unachouza.

Pia nimetoa nafasi za kipekee sana za kufanya kazi kwa ukaribu na watu 12 kwa kipindi cha mwaka mmoja ili kuweza kukuza zaidi biashara zao. Kama hujaona nafasi hizi, soma hapa; Ama Kweli Watu Wana Kiu Kubwa Ya Mafanikio, Soma Hapa Uone Jinsi Nafasi Hizi Nzuri Zilivyoisha Haraka.

#3 TUONGEE PESA; KANUNI YA MUNGER YA KUFIKIA UTAJIRI.

Charlie Munger, mwekezaji mwenye mafanikio makubwa sana ambaye nimekushirikisha falsafa zake kupitia kitabu nilichosoma, anasema kanuni ya kufikia utajiri ni rahisi sana, ila wengi wanashindwa kwa sababu hawaamini kwenye urahisi huo, na hawana subira, wanataka vitu vya haraka na vitu vinavyoenda na wakati. Anasema kanuni yake ni ya kizamani na imepitwa na wakati, lakini inaleta matokeo sahihi, yaani mtu anapata utajiri kweli.

Munger anasema; kama unataka kuwa tajiri, unahitaji kuwa na mawazo mazuri machache ambapo unajua kwa hakika ni nini unafanya. Kisha unapaswa kuwa na uthubutu wa kukomaa na mawazo hayo, wakati wa kupanda na kushuka bila ya kukata tamaa. Siyo kanuni ngumu, na pia siyo ya kisasa.

Rafiki, Munger amemaliza kila kitu hapo, sasa kazi ni kwako kama upo tayari kukomaa na kile unachofanya mpaka ufanikiwe, au unataka kuendelea kukimbizana na kila aina ya fursa mpya inayokuja mbele yako.

Ninachoweza kukuambia rafiki yangu ni hichi, ukichagua kitu kimoja au vichache ambavyo utavifanya kwa maisha yako yote, ukawa unajifunza kila siku na kuchukua hatua, halafu ukaachana na mengine yote wanayofanya wengine, una uhakika wa kufanikiwa. Lakini sasa wengi hawana uthubutu na nguvu ya kuepuka tamaa zinazopamba njia ya kuelekea kwenye mafanikio.

#4 HUDUMA NINAZOTOA; TUMEKARIBIA KABISA TUKIO KUBWA LA MAFANIKIO KWA MWAKA 2018/2019.

Rafiki yangu pendwa, zimebaki siku tano tu kuelekea kwenye tukio kubwa la mafanikio kwa mwaka huu 2018, tukio hilo ni SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018, ambayo itafanyika tarehe 03/11/2018, jijini Dar es salaam. Lakini zimebaki siku tatu pekee kupata nafasi ya kushiriki semina hii, ambapo mwisho wa kulipia ili kushiriki ni tarehe 31/10/2018.

Nafasi za kushiriki semina hii ni 100 pekee, waliodhibitisha kushiriki ni zaidi ya 100. Hivyo nafasi zitafungwa pale ambapo idadi ya waliolipia itatimia 100. Hivyo kama hupendi kukosa nafasi hii ya kipekee kwako kwa mwaka huu 2018 na hata 2019, fanya malipo mapema.

Ada ya kushiriki SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018 ni tsh 100,000/= (laki moja) ambayo inajumuisha huduma zote za siku ya semina, kuanzia chai, chakula vinjwaji, vijitabu vya kuandikia, kalamu na kadhalika.

Namba za kufanya malipo ni 0755 953 887 au 0717 396 253 majina ya namba hizo ni AMANI MAKIRITA.

Karibu sana kwenye semina ya KISIMA CHA MAARIFA 2018, tujifunze na kupata hamasa ya kuchukua hatua kwa mwaka mzima bila ya kuchoka.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; KINACHOKUZUIA NI KILE UNACHOKIKIMBIA.

“It’s not who you are that holds you back, it’s who you think you’re not.” – Unknown

Watu wengi wamekuwa wanafikiri kwamba kinachowazuia kufanikiwa ni vile walivyo, ukweli ni kwamba kinachowazuia wengi kufanikiwa ni kile ambacho wanajaribu kukikimbia. Kile ambacho unajifikiria siyo, ndiyo kinachochukua muda na nguvu zako nyingi na kukuzuia kufanikiwa.

Rafiki kama utachukua hatua leo ya kujijua wewe ni nani na unataka nini, kisha ukafanya maamuzi ya kuendesha maisha yako kwa kufanyia kazi wewe na kile unachotaka, utapunguza sana ugumu wa safari yako ya mafanikio.

Lakini unapoteza muda na nguvu nyingi kwenye mambo ambayo hayaendani na wewe, pale unapojilinganisha na wengine, unapojaribu kuwaiga wengine, au kufanya mambo kwa sababu wengine wanafanya, hata kama hayana maana kwako.

Chagua kuwa wewe, na chagua kufanya yale ambayo ni muhimu kwako tu, na utaweza kupiga hatua kubwa sana kwenye maisha yako.

Rafiki, nikutakie maandalizi mema ya juma tunalokwenda kuanza, na maandalizi mema ya kushiriki SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018, nina imani kubwa tutakuwa pamoja juma lijalo, tukijifunza na kuweka mikakati ya kufanyia kazi kwa mwaka mzima ili kufanikiwa zaidi.

Hakikisha unakamilisha malipo yako ya ada ya semina mapema ili usikose nafasi hii ya kipekee. Pia usisahau kuepuka makosa yale 25 ya kisaikolojia ambayo tunayafanya mara kwa mara na yanapelekea kufanya maamuzi mabovu.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu