Rafiki yangu mpendwa,

Kitu kinachojenga au kubomoa maisha yetu, kinachofanya tufanikiwe au kushindwa, ni maamuzi ambayo tunayafanya kwenye maisha yetu.

Kila siku tunafanya au kuepuka kufanya maamuzi fulani, na hayo ndiyo yametufikisha pale tulipo sasa. Hapo ulipo leo ni matokeo ya maamuzi ambayo ulifanya au kutokufanya siku zilizopita.

Kwa mfano kama hapo ulipo una kipato kidogo, ni kiashiria kwamba kuna maamuzi muhimu ambayo hukuyafanya siku zilizopita. Na kama utaendelea unavyoendelea, bila ya kufanya maamuzi bora yanayoweza kukupeleka kwenye kipato kikubwa zaidi, utaendelea kuwa na kipato cha chini.

Rafiki, leo nakwenda kukushirikisha jinsi ya kutumia majuto kama kipimo cha kufanya maamuzi bora kwetu. Huwa tunayapa majuto sura mbaya, tunaona kujuta ni kama kitu kibaya kwenye maisha yetu, na hii ndiyo sababu tunapaswa kuyatumia kupiga hatua zaidi.

regrets-dying_mirror2

Bronnie Ware alikuwa muuguzi kwenye kituo kinachotoa huduma kwa wagonjwa ambao wanasubiria kufa. Hawa ni wagonjwa ambao walikuwa na magonjwa sugu na yasiyoponyeka, hivyo walikuwa wanasubiria kifo. Bronnie alipata nafasi ya kukaa na wagonjwa wa aina hiyo kwa zile siku za mwisho kabisa za maisha yao, na wagonjwa hao wakijua wamefika tamati ya maisha yao. Bronnie alichukua nafasi ya kumuuliza kila mgonjwa ni kitu gani anajutia zaidi kwenye maisha yake, na hapo alipata majibu mengi, lakini matano yalijirudia kwa wengi zaidi. Matano yaliyojirudia sana ni, natamani ningeyaishi maisha yangu, natamani nisingefanya kazi sana, natamani ningeweza kueleza hisia zangu, natamani ningekuwa karibu na marafiki zangu na natamani ningejiruhusu kuwa na furaha.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; When Breath Becomes Air (Safari Ya Mtu Mmoja Katika Kujua Maana Ya Maisha Na Kifo).

Lengo la makala ya leo siyo kuangalia majuto hayo matano, lakini kujifunza kwamba kila mtu huwa anakuwa na majuto fulani anapofikia tamati ya maisha yake. Na wengine majuto haya huanza mapema kabla hata maisha hayajaenda sana.

Hivyo basi, kama tukiweza kuyatumia majuto vizuri, tunaweza kufanya maamuzi bora ambayo yatatuzuia kuwa na majuto baadaye.

Je unawezaje kutumia majuto kuweza kufanya maamuzi bora kabisa kwenye maisha yako?

Pale unapojikuta njia panda, kwamba ufanye au usifanye kitu fulani, jiulize swali moja, je siku zijazo nitajuta kwa kufanya au kutokufanya kitu hiki? Fikiria miaka kumi imepita na umefanya au hujafanya maamuzi hayo, je utajutia kutokuchukua hatua kipindi hiki?

Kama jibu ni ndiyo kwamba utakuwa na majuto, kama utajutia kutokuchukua hatua fulani leo hii, basi chukua hatua sasa. Lakini kama ni kitu ambacho hutajutia, kama ni kitu ambacho utakisahau kabisa, basi unaweza kuachana nacho.

Hata pale unapotaka kuahirisha kitu kwa ajili ya kesho au siku zinazo, jiulize je utakuwa na majuto kwa kutokufanya kitu hicho leo, na kama jibu ni ndiyo, basi kifanye. Kwa sababu huwezi kujua kesho inakujaje na hutaki kuanza kesho ukiwa na majuto.

Majuto ni kipimo kizuri sana kwetu kufanya maamuzi, kwa sababu inatuonesha kipi ambacho kitaendelea kutusumbua zaidi kwenye maisha yetu.

Na ili kuepuka kutumia majuto kama uzembe wa kutokufanya, ili kuepuka kujidanganya kwamba unaacha kuchukua hatua fulani kwa sababu hata hivyo hutaijutia, wewe jiangalie.

Kwa mfano kama umejiambia leo hutajutia kwa kutokuchukua maamuzi uliyopanga kuchukua, lakini kesho ukakutana na mtu anayechukua maamuzi na ukajisikia vibaya, basi jua baadaye utakuja kujuta sana. Usiendelee kujidanganya, chukua maamuzi.

Kama kwa muda mrefu kuba biashara umekuwa unataka kuifanya, kama kwa muda kuna kipaji ndani yako umekuwa unataka kukiendeleza, lakini umejidanganya huna haja ya kufanya hivyo kwa sababu tayari una kazi na upo bize, lakini unapokutana na watu wanaofanya biashara uliyopenda au wenye kipaji ulichonacho unajisikia vibaya kwa kutokuwa kama wao, rafiki yangu chukua hatua sasa. Siku utakayokuwa unavuta pumzi yako ya mwisho, utajutia sana na hutajisamehe kwa zawadi hiyo uliyoikosa ya kuyaishi maisha yako, ya kujiruhusu kuishi kwa furaha.

Rafiki, unaweza kumdanganya kila mtu hapa duniani, isipokuwa mtu mmoja tu, ambaye ni wewe mwenyewe. Hivyo kwa kutumia majuto, chagua kuyaishi maisha ambayo hata ukifa kesho, hutakuwa na cha kujutia, kwa sababu utakuwa umepata unachotaka, au utakuwa kwenye njia ya kufanyia kazi kukipata.

SOMA; USHAURI; Ujumbe Muhimu Sana Kwa Wenye Miaka 20, 30, 40 Mpaka 50. Kama Unajiona Muda Umekutupa Mkono, Soma Hapa.

Usikubali kuianza siku ukifikiria ungeweza kuwa unafanya kitu kingine bora na muhimu zaidi kwako kuliko unachofanya kwa wakati huo. Tunaishi kwenye dunia ambayo kila mtu anaweza kufanya chochote anachotaka kufanya. Tumia nafasi hii kuchukua hatua sasa, ili siku zijazo usiwe na majuto yoyote, uende safari yako hapa duniani na kuimaliza ukiwa na furaha kwa kuchagua kuyaishi maisha yako na kufanya yale ambayo ni muhimu zaidi kwako.

Nihitimishe makala hii kwa kukusisitiza hili rafiki yangu, tumia majuto kama kipimo cha kufanya maamuzi muhimu kwako, kama kitu utakijutia baadaye, basi chukua hatua. Badala ya kufanya maamuzi yako kwa kutumia kufanikiwa au kushindwa, au furaha au maumivu, fanya maamuzi yako kwa kutumia majuto na hutakuwa na majuto kwa maisha yako yote.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge