Kwenye maisha yetu tuna machaguo makuu matatu; ZAIDI, KIDOGO, NA SAWASAWA.

ZAIDI.

Kwenye maisha yako kuna vitu ambavyo unapaswa kuvifanya zaidi, hivi ni vile vitu vizuri vinavyokupeleka kwenye mafanikio makubwa. Kadiri unavyofanya zaidi vitu vizuri, ndivyo unavyojiweka kwenye nafasi ya kufanikiwa zaidi.

KIDOGO.

Kwenye maisha yako kuna vitu ambavyo unapaswa kupunguza kufanya, hivi ni vitu ambavyo havina mchango wa wewe kufika kwenye mafanikio makubwa. Ni vitu ambavyo siyo muhimu sana kwako na ukiacha kuvifanya hakuna unachokosa kwenye maisha yako. Vitu hivi huwa vinakula muda wako mwingi na unashindwa kuutumia kwenye vitu vya msingi.

SAWASAWA.

Kwenye maisha yako, kuna vitu ambavyo unapaswa kuendelea kuvifanya kama unavyovifanya sasa. Hupaswi kupunguza wala kuongeza, unapaswa kuendelea kuvifanya kama unavyofanya sasa. Hivi ni vile vitu ambavyo vinakuletea matokeo bora na kukuwezesha kufikia mafanikio makubwa zaidi.

Rafiki, hayo ndiyo maamuzi matatu muhimu ya kufanya kwenye maisha yako, na ni maamuzi yanayohusisha kila eneo la maisha yako, hata kwa watu wanaokuzunguka. Kuna watu unapaswa kuwaongeza, kuwapunguza na ambao unapaswa kuendelea nao. Kadhalika kuna maeneo unapaswa kuongeza muda na nguvu zako, mengine kupunguza na mengine kuendelea nayo kama unavyokwenda sasa.

Kila siku jikumbushe maamuzi haya matatu na ona wapi pa kufanyia kazi ili uweze kufikia mafanikio makubwa zaidi kwenye maisha yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha