Mpendwa rafiki yangu,

Kwanza katika zama hizi hutakiwi kumtegemea mtu bali unatakiwa kujitegemea wewe mwenyewe. unatakiwa kusimama na miguu yako mwenyewe na siyo kwa miguu ya watu wengine. kuwategemea watu ni utumwa mbaya utakaokufanya usione maana ya maisha hapa duniani.

Watu wengi wamezaliwa na dhana ya utegemezi, wanajua kabisa maisha yao ni jukumu la watu wengine, kiongozi au mtu fulani ndiyo atawajibika kurekebisha maisha yao kama vile wanavyotaka. Huwa tunajidangaya sisi wenyewe kwa matarajio hewa kila siku, unakuja kushtuka umri umeenda, nguvu huna tena ya kufanya kazi, muda ambao ulikuwa una nguvu ulikuwa unazielekeza sehemu ambayo siyo sahihi.

Ili usije kujutia baadaye, tafadhali tumia muda na nguvu zako vizuri, ukiwa mzee unaweza kuwa na muda wa kufanya kile unachotaka lakini utashindwa kwa sababu ya kukosa nguvu. Hata uwe na muda vipi kama umekosa nguvu ni sawa na bure. Gari haliwezi kwenda mbila nishati yaani mafuta hivyo mafuta ya binadamu ni nguvu.

Sababu kuu moja kwanini usimtegemee kiongozi yoyote katika maisha yako ni kwamba, jukumu la maisha yako ni lako mwenyewe na siyo la mtu mwingine. Unatakiwa kuwajibika na maisha yako kama vile unavyowajibika na mwili wako. Huwajawahi kumwachia mtu mwili wako kuubeba kwa sababu umechoka bali kokote unakokwenda lazima utakwenda nao uwe mzima au unaumwa hivyo mwili wako ndiyo mahali au nyumba unayoishi na maisha yako ni jukumu lako unatakiwa kuwajibika kwa kila kitu.

SOMA; Sifa Bora Ya Uongozi Ambayo Kila Kiongozi Anapaswa Kuwa Nayo

Uchungu wa maisha unakuja pale unapoona kuwa jukumu la maisha yako siyo lako bali ni la mtu mwingine. Utataka watu wabadili maisha yako wakati nao wana kazi ya kubadili maisha yao.

Hakuna mtu ambaye anakosa usingizi kwa sababu ya maisha yako. kila mtu ana yake muhimu yanayomsumbua hivyo simama kwa miguu yako. chukua hatamu ya maisha yako. hakuna ushujaa mkubwa kama kujiambia jukumu la maisha yangu ni langu mwenyewe. hivi pale unapotaka kuvamiwa na wezi au majambazi utakaa na kusubiri na kusema jukumu la ulinzi siyo lako ni la polisi? Lazima utapambana kuhakikisha unakuwa salama kwa sababu ni maisha yako.

Uongozi

Pale unapokuwa unasikia njaa au umebanwa na haja huwezi kumwambia mtu naomba unisaidie kwenda msalani nimebanwa na haja bali utakwenda mwenyewe ndivyo maisha yalivyo unatakiwa kuwajibika na maisha kama unavyowajibika na mwili wako kila siku.

Ondoa dhana ya utegemezi na kutegemea viongozi waje kubadilisha maisha yako. kiongozi mkuu wa maisha yako ni wewe mwenyewe na siyo mtu mwingine.

Mkurugenzi wa maisha yako ni wewe mwenyewe, hivyo pambana kuhakikisha maisha yako yanakuwa bora, usilalamike kwa lolote, maisha yako ni jukumu lako ingia kwenye vita pambana mpaka upate ushindi. Utakula kile unachokitafuta kila siku, huwezi kila siku kula kwa jasho la wengine.

Tunaweza kuifanya dunia kuwa salama kwa kila mmoja kama kila mtu akiyabeba maisha yake. Kila mtu akichukua jukumu la maisha yake na kusema kuwa jukumu la maisha yake ni lake mwenywe na siyo mtu mwingine.

Hatua ya kuchukua leo; jukumu la maisha yako ni lako mwenyewe. hivyo wajibika ili uishi. Hakuna mtu anayekosa kufanya yake au kukosa usingizi usiku kwa sababu ya maisha yako. usimtegemee kiongozi yoyote isipokuwa wewe mwenyewe ambaye ndiyo jemedari mkuu wa maisha yako mwenyewe.

Kwahiyo,mafanikio ni haki yako. mafaninikio ni wajibu wako hivyo pambana ili uweze kupata kile unachotaka. Tafuta dunia nzima hakuna aliyefanikiwa kwa kulalamika bali kuchukua hatua juu ya maisha yako.

Makala hii imeandikwa na

Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali. Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa www.mtaalamu.net/kessydeo, vitabu na kwenye klabu yake ya MIMI NI MSHINDI.  Karibu sana.

Ukawe na siku bora sana rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,

Mwl, Deogratius kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com // kessydeo@mtaalamu.net

Asante sana