Kila mtu kuna mahali amekwama kwenye maisha yake,
Haijalishi amepiga hatua kubwa kiasi gani, bado kuna hatua kubwa zaidi anazoweza kupiga.
Lakini wengi wamekuwa hawapigi hatua hizo zaidi.
Kwa sababu kunakuwa na vikwazo ambavyo vimewakwamisha.
Ni rahisi kuangalia nje na kuona vikwazo vya nje ambavyo vinamkwamisha mtu. Labda mazingira, hali ya uchumi, washindani, watu wa karibu na kadhalika.
Lakini ukweli ni kwamba, sehemu kubwa ya vikwazo vinavyomzuia mtu kupiga hatua, vinaanzia ndani yake.
Kwa hakika, asilimia 80 ya vikwazo vinavyokuzuia wewe usipige hatua, vinaanzia ndani yako mwenyewe.
Vikwazo hivi vinaanzia kwenye imani zako, fikra ulizonazo, tabia ulizojijengea, mtazamo ulionao, uwezo uliopo ndani yako na ujuzi ulionao au usiokuwa nao.
Ukianza kufanyia kazi maeneo hayo, kwa kuamini kwenye kile unachotaka na kwamba unaweza kukipata, kuwa na mtazamo chanya mara zote, kufikiria kuhusu kule unakotaka kwenda na kuepuka fikra za kukatisha tamaa. Kisha ukajijengea tabia bora unazoziishi kila siku, ukatumia vizuri uwezo uliopo ndani yako na kujijengea ujuzi mpya utakaokufikisha kule unakotaka kufika, hakuna kinachoweza kukukwamisha.
Kila wakati utakuwa unapiga hatua zaidi licha ya wengine kuwa wamekwama na kulalamika mambo ni magumu.
Mambo ni magumu kama wewe mwenyewe utakubali kuwa mgumu na kubaki kama ulivyo. Lakini unapokuwa tayari kubadilika wewe mwenyewe, una fursa kubwa ya kuyafanya mambo kuwa bora zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,