Kwenye maisha yako, jihusishe na watu ambao tayari wana furaha kwa hali yoyote wanayopitia kwa wakati walionao. Na siyo watu wasiokuwa na furaha, kwa kuamini kwamba utaweza kuwapa furaha.

Huwezi kumbadili mtu asiye na furaha akawa na furaha, kwa sababu kinachowakosesha furaha siyo kitu cha nje, bali kitu kilichopo ndani yao.

Watu wasio na furaha wamechagua kutokuwa na furaha na hakuna chochote unachoweza kufanya kikabadili hali hiyo waliyochagua.

Kuna tabia ambazo watu wanakuwa wamechagua kwenye maisha yao, ambazo zinachangia wasiwe na furaha, hakuna unachoweza kufanya ukabadili hali hiyo.

Hivyo usipoteze muda na nguvu zako kutaka kuwafanya wengine wawe na furaha, chagua kuyaishi maisha yako na kushirikiana na wale ambao tayari wana furaha.

Na kama wewe ndiye mtu usiyekuwa na furaha na unayetegemea kupata furaha kutoka kwa wengine, ni wakati sasa wa kuacha kupoteza muda kutafuta kitu ambacho hujapoteza. Badala yake kaa na angalia ndani yako, na ona ni wapi unapojikwamisha usiwe na furaha.

Kama unaona maisha yako hayafai, maisha hayako sawa kwako na dunia inakutenga, chukua nafasi na tembelea hospitali yenye wagonjwa mahututi au tembelea gereza na ongea na watu waliofungwa kwa muda mrefu, ukitoka hapo, utaona jinsi ambavyo una kila cha kushukuru na kufurahia kwa kutokuwa mgonjwa au mfungwa.

Na hata kama una ugonjwa sugu au umefungwa, fikiria wale ambao wameshafariki, tena kwenye mazingira magumu, lakini wewe bado unaivuta pumzi, ni jambo la kushukuru na kufurahia sana.

Nimalizie  kwa kukuambia, watu wasiokuwa na furaha wana kisirani chao wenyewe, kaa nao mbali, maana watakuambukiza kisirani hicho.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha