“Crimes often return to their teacher.”
—SENECA, THYESTES, 311

Kupata nafasi hii nzuri ya kuiona siku ya leo ni bahati ya kipekee sana kwetu.
Siyo kwa sababu tunastahili sana au kwa sababu ya juhudi zetu, bali ni bahati tu.
Kazi yetu hapa duniani bado haijakamilika, hivyo leo tuna nafasi nyingine ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.

Asubuhi ya leo tutafakari UNACHOWAFUNDISHA WENGINE, KITARUDI KWAKO…
Chochote kibaya unachowafundisha wengine kufanya, kuna siku kitarudi kwako, kuna siku watakufanyia ubaya huo na wewe pia.
Kama una biashara na unawafundisha wafanyakazi wako jinsi ya kuwaibia wateja, kuna na uhakika kuna siku wafanyakazi hao hao watakuibia na wewe pia.
Kama ni watoto wako umewafundisha jinsi ya kudanganya ili kukwepa majukumu kuna siku watakudanganya wewe na kuyakimbia majukumu yao kwako.
Kama utawafundisha wengine jinsi ya kuwa waonevu, kuna siku watakuonea na wewe pia.

Ubaya na uovu wowote unaowafundisha watu wengine kufanya, kuna siku watakufanyia uovu huo wewe pia.
Ni kanuni ya asili, ndivyo dunia inavyokwenda.
Wapo wanaosema malipo ya kila kitu yako hapa hapa duniani,
Na wengine wanasema unachowafanyia wengine ndiyo utakachofanyiwa.
Vyovyote unavyoamini, lakini kuwa na uhakika, hakuna utakachofanya na ukaondoka bila kupata malipo yake.
Fanya wema na utalipwa wema, fanya ubaya na utalipwa ubaya.
Unapoona unafululiza kulipwa ubaya, kabla hujaanza kulaumu watu, hebu angalia ni vitu gani ulifanya huko nyuma.
Utaona jinsi ambavyo wewe mwenyewe uliwatengeneza wale wanaokufanyia ubaya sasa.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuepuka kufanya ubaya au kuwafundisha wengine kufanya ubaya kwa sababu mwisho wa siku ubaya huo utarudi kwako mwenyewe.
#UnavunaUlichopanda #MalipoNiHapaHapa #AsiliHaikopwi

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1