Kuna aina za mashindano ambapo kushinda ni kushindwa.

Yaani unashindana au kubishana na wewe na kufikia mwisho wewe unaibuka mshindi, lakini kwa uhalisia unakuwa umepoteza.

Yule unayekuwa umemshinda, inakuwa ni kwa hoja, lakini bado anaamini alichokuwa anaamini, na ushindi wako unamfanya azidi kutofautiana na wewe.

Japokuwa hatakuwa na hoja za kukueleza, lakini ndani ya nafsi yake anakuwa amekuweka kwenye upande wa mtu asiye sahihi.

Mashindano au mabishano yoyote ambayo yanahusisha hisia, ndiyo yanayotengeneza hali ya aina hii. Na kadiri hisia zinavyokuwa kali, ndivyo ushindi wako unakupoteza zaidi.

Tuchukue mfano mdogo tu, ni nani ambaye amewahi kubadili dini yake baada ya kuwa na ubishani mkali na wengine ambao walimpa hoja kwa nini dini yake siyo sahihi. Watu hao wanaweza kushinda kwa hoja, lakini hilo litamfanya mtu ashikilie dini yake zaidi.

Kadhalika kwenye michezo, hakuna anayebadili timu anayoipenda kwa sababu watu wamemwonesha jinsi isivyo sahihi.

Tukirudi kwenye maisha yetu ya kawaida, hasa ya mahusiano yetu na watu wa karibu kwetu, kuna vitu vingi ambavyo tunaweza kubishana na watu hao, na kuwapa hoja kweli, tukaona tumeshinda, lakini tukawa ndiyo tumepoteza.

Ili kuepuka ushindi huu hewa, zingatia yafuatayo;

  1. Epuka mashindano au ubishani unaohusisha imani au itikadi za watu. Hakuna namna unaweza kushinda katika maeneo hayo, kadiri unavyokuwa sahihi ndivyo upande wa pili unavyozidi kuupoteza.
  2. Angalia thamani ya ushindi kabla hujashiriki kushindana. Chukulia mfano uko na mwenza wako mnaangalia tv, wewe unataka kuangalia chanel fulani na yeye anataka kuangalia nyingine. Hakuna anayekubaliana na mwingine, hivyo mnaanza ubishani, kila mtu anatoa hoja kwa nini chanel anayotaka kuangalia yeye ni muhimu. Unaweza kutoa hoja nzuri, ukashinda na kupewa nafasi ya kuangalia chanel hiyo, lakini mwenzako hataridhika na hilo, hata kama hatakuambia. Katika hali kama hiyo, ni vyema kupima thamani ya ushindi, unanufaikaje kushinda kuangalia chanel ya tv, huku mwenza wako akiwa na kinyongo? Kwa vitu vidogo vidogo kama hivyo, mpe mtu nafasi ya kufanya kile anachopendelea kufanya.

Kwa kuzingatia hayo mawili, utajiepusha na mashindano au mabishano yasiyo na tija kwako na hilo litakupelekea kuboresha mahusiano yako na wengine.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha