Rafiki yangu mpendwa,

Kila siku mpya unayoipata ni nafasi nyingine ya kwenda kuwa bora kuliko siku iliyopita.

Nimekuwa nakushauri kwamba kama kuna mtu unayepaswa kushindana naye basi ni wewe mwenyewe. Wewe wa leo, unapaswa kushindana na wewe wa jana, kwa kuhakikisha leo unakuwa bora kuliko ulivyokuwa jana.

Lakini ubora ni kitu ambacho kwa sasa kimesahaulika, ni kama vile kuna mashindano ya kuwa kawaida, yaani kuwa hovyo.

Utaona kwenye kila eneo la maisha, kuanzia kwenye ajira ambapo kila mtu anajaribu kufanya kazi kidogo awezavyo, huku akikimbia majukumu yake na kuwaachia wengine.

Kwenye biashara ambapo tulitegemea watu kujisukuma zaidi, mambo ndiyo yanazidi kuwa mabaya, katika kuhangaika kushindana na wafanyabiashara wengine, wengi wameharibu zaidi biashara zao, kwa kukazana kuuza kwa bei ndogo kuliko wengine na hivyo kushindwa kutoa huduma bora na biashara kuwa hovyo.

Kwenye maisha binafsi na hata mahusiano pia hili limeingia, watu wanaishi leo kama walivyoishi jana, na hawana msukumo wowote wa kuwa bora zaidi leo kuliko walivyokuwa jana. Na hili limepelekea wengi kujikuta wakikutana na changamoto zinazowashinda kila mara.

elimu fedha 2

Katika kuhakikisha kwamba unapata msukumo wa kuwa bora zaidi kila siku, hapa nimekushirikisha kauli tano ambazo nimejifunza maeneo mbalimbali na kwa njia mbalimbali. Ukizielewa na kuzitumia kauli hizi, kila siku kwako itakusa siku ya kuwa bora kuliko iliyopita.

Moja; Fanya vizuri au usifanye kabisa.

Kwa chochote unachoamua kufanya, una maamuzi ya aina mbili, kukifanya vizuri kabisa kadiri ya uwezo wako au kutokukifanya kabisa. Hupaswi kuwa na maamuzi mengine nje ya hayo mawili. Usifanye kawaida, usifanye kama wanavyofanya wengine, bali fanya kwa ubora wa hali ya juu au usifanye kabisa.

Zile kauli kwamba unafanya fanya tu au unajaribu hapa hazina nafasi, maisha siyo majaribio, maisha yana hali mbili, unaishi au umekufa, hivyo usipoteze nafasi nzuri unayoipata kwa kujaribu chochote. Fanya. Fanya kwa ubora. Na kama huwezi kufanya vizuri na kwa ubora, basi achana na kitu hicho kabisa.

Hujisaidii wewe na wala humsaidii yeyote kwa kufanya kitu nusu nusu, kwa kufanya kitu kwa ukawaida, unaishia kupoteza muda wako na wa kila mtu.

Mbili; Ingia mzima mzima.

Huenda lengo lako la baadaye ni kumiliki kiwanda, lakini kwa sasa huwezi kuanza na lengo hilo. Badala yake inabidi uanze na kitu kingine huku ukijiandaa kwenda kwenye lengo lako kuu. Hivyo unaweza kuanzia kwenye ajira au ukawa na biashara nyingine, lengo ni kujifunza na kukusanya mtaji wa kwenda kwenye lengo kuu.

Sasa wengi wamekuwa na tabia ya kufanya kawaida na kuona kile siyo wanachotaka kufanya bali wanapita tu. Hili ni kosa ambalo linawazuia wasiwe bora. Chochote unachochagua kufanya, ingia mzima mzima, yaani kifanye kama ndiyo kitu pekee utakachofanya hapa duniani.

Na hivyo ndivyo ilivyo, huenda ndiyo kitu pekee utakachofanya hapa duniani, maana wengi huwa na malengo tofauti lakini wanapoanza kufanya kitu tofauti malengo yao yanabadilika pia.

Ingia mzima mzima, chochote unachochagua kufanya, kifanye kama ndiyo kitu pekee utakachofanya kwenye maisha yako, hata kama ni kwa leo tu. Mtazamo huo utakusukuma uwe bora zaidi.

SOMA; 1627; Kweli Tatu Ambazo Dunia Haitaki Uzijue, Zijue Hapa Ili Maisha Yako Yaweze Kuwa Bora…

Tatu; Jinsi unavyofanya kitu kimoja ndivyo unavyofanya kila kitu.

Unaweza kumdanganya kila mtu kwenye maisha lako, lakini kuna mtu mmoja ambaye huwezi kumdanganya, mtu huyo ni wewe mwenyewe. Unaweza kuchagua kuwa na maisha ya aina mbili, kuwahadaa wengine, lakini wewe unajua na hilo litakusumbua.

Jinsi unavyofanya kitu kimoja, ndivyo unavyofanya kila kitu kwenye maisha yako. Usijidanganye kwamba usipokuwa mwaminifu kwenye mahusiano yako basi utaweza kuwa mwaminifu kwenye kazi au biashara yako. Kila unachofanya, hata kama ni kwa kificho kiasi gani, kinaathiri kila eneo la maisha yako.

Hivyo kama kuna kitu ambacho siyo sahihi kufanya, usifanye, hata kama ni mara moja, hata kama ni kwa kificho na hata kama unajiambia hakihusiki na kazi au biashara yako, kila unachofanya kwenye maisha yako kinaathiri kila eneo la maisha yako. Fanya kilicho sahihi, fanya kwa ubora na hilo litakupa msukumo wa kuwa bora kwenye kila eneo la maisha yako.

Nne; Kila unachofanya kinabeba jina lako.

Watu wanakuona, kukujua na kukuhukumu kwa kila unachofanya. Kila unachokifanya kinabeba jina lako, na dunia nzima inakuona kupitia matokeo unayozalisha.

Hivyo usikubali chochote unachogusa kiwe kawaida au hovyo, hakikisha kinakuwa bora na yeyote atakayekutana nacho, aseme hapa kuna mtu alifanya kitu.

Hata kama unachofanya ni kufagia barabara, ifagie kwa namna ambayo kila atakayepita kwenye barabara hiyo atasema hii barabara imefagiliwa vizuri.

Kwa kujua hili, jisukume kufanya kila kitu kwa ubora, kuacha alama nzuri kwenye kila unachogusa, watu wakikutana na kazi yako, waikubali na kuipenda.

Hili ni jambo ambalo lipo ndani ya uwezo wa kila mmoja wetu, unachohitaji ni kuweka roho na utu wako kwenye kila unachofanya. Usikifanye kama wengine, bali kifanye kama wewe, utu wako unaweka tofauti kubwa sana kwenye kile unachofanya.

Tano; Una nafasi moja ya kuonekana, itumie vizuri.

Huwa tunasema usihukumu kitabu kwa ganda la nje, lakini hivi ndivyo kila mtu anavyofanya. Mtu anafanya maamuzi kuhusu wewe kwa dakika chache sana na ndivyo atakavyokuchukulia maisha yake yote.

Una nafasi moja tu ya kuonekana, hivyo itumie vizuri. Jinsi watu wanavyokuona mara ya kwanza, ndivyo wanavyokuhukumu na kuanzia hapo ndivyo watakavyokuchukulia, hata kama walivyokuona sivyo ulivyo.

Hili linapaswa kukusukuma kuwa vizuri kila wakati, kufanya kila unachofanya kwa usahihi na ubora wa hali ya juu, kiasi kwamba yeyote unayekutana naye, anaona thamani kubwa iliyopo ndani yako.

Unapoitumia nafasi yako moja vizuri usifanye kwa maigizo, badala yake ifanye kwa uhalisia wako. Wengi wamekuwa wanafanya maigizo ambayo baadaye yanawagharimu, fanya kile kilicho sahihi kwa sababu ni sahihi kufanya na siyo kwa sababu unataka kuonekana na wengine. Kwa kufanya hivyo kila wakati, utaonekana hata pale ambapo hudhamirii kuonekana.

Rafiki, ziandike kauli hizi tano na kila siku jikumbushe na kuziishi, ni kauli rahisi kueleweka na hata kuziishi, lakini matokeo yake yatakuwa mazuri sana kwako.

Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania