Kuna watu wamekuwa wanachagua wao wenyewe kufa, kwa kukikaribisha kifo kabla hata ya muda wake.
Na hawafanyi chochote ambacho ni hatari ili kujiua, bali wanafanya kila ambacho wanategemewa kufanya na matokeo yake kuwa kifo cha mapema.
Njia ambayo imekuwa inatumiwa na wengi kuchagua kufa bila ya kujua ni kustaafu. Pale mtu anapochagua kupumzika na asifanye tena kazi, mwili wake unajua hauna tena mahitaji na hapo unakaribisha kifo.
Tafiti nyingi zimekuwa zinaonesha watu wengi hufa ndani ya miaka mitano tangu kustaafu kazi zao. Pamoja na sababu nyingine zinazoweza kuchangia, lakini kubwa zaidi ni mwili kuona hauna tena kazi.
Unapokuwa unafanya kazi, roho yako inajua bado unahitajika na hivyo inausukuma mwili ili uendelee kuwa imara kupambana na kazi. Unapostaafu kazi, roho inajua kazi imeisha na hivyo haiusukumi mwili, kitu kinachopelekea mwili kudhoofu, inakuwa rahisi kukaribisha magonjwa na hauwezi kupambana nayo.
Hivyo moja ya njia za kuepuka kufa haraka ni kuhakikisha hustaafu kazi au biashara unayoifanya, kuendelea kuifanya maisha yako yote.
Lakini siyo kila aina ya kazi au biashara itakupa nafasi ya kuishi muda mrefu, bali ile ambayo unapenda kuifanya ambayo inatokana na kusudi la maisha yako.
Kama kazi au biashara unayoifanya huipendi na inakupa msongo, kuendelea kuifanya ni kuchagua kuyafupisha maisha yako. Lakini kama ni kitu unachopenda kufanya, ambacho upo tayari kukifanya kwa muda mrefu bila kuchoka, basi unapaswa kuendelea kukifanya kila siku unapokuwa hai.
Ndiyo maana ni muhimu sana ujue kusudi la maisha yako na uchague kitu cha kufanya kukamilisha kusudi hilo, ambacho utakifanya maisha yako yote.
Wengi hupuuza hili, hasa wanapokuwa na kazi au biashara zinazowalipa sana japo hawazipendi. Wakijiambia wanafanya kazi au biashara hizo kwa muda tu, wapate uhuru wa kifedha kisha wastaafu na kupumzika. Wanafanya kweli, wanazipata fedha, ila wanapostaafu na kupumzika, maisha yao nayo yanaporomoka haraka.
Hata kama utaazimika kustaafu kazi au biashara unayoifanya, kwa sababu zozote zile, hakikisha una kitu chako unachoweza kuendelea kukifanya siku zote za maisha yako, ambacho hakuna namna utalazimika kustaafu, mpaka uchague mwenyewe.
Kama bado hujawa na kitu cha aina hii, anza kukifanyia kazi mapema. Anza kujiangalia mwenyewe, jisikilize nini kinatoka ndani yako, jaribu vitu mbalimbali na utakutana na kile kinachokuvutia zaidi na unachokitumia kutoa mchango kwa wengine, kisha kitengeneze kwa namna utaweza kukifanya kila siku. Na ukiwa na njia ya kulipwa kukifanya, basi inakuwa bora zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante sana kocha kwa ukurasa huu hongera pia kwa kuweza kuandika na kufika ukurasa 2100 si mchezo na bado utaandika
Kitu nimejifunza kwa wafanyakazi wengi ni wamekosa maana ya kazi tupo kwenye kazi tu kwa sababu tuna wategemezi wanaotutegemea na hatufanyi kwa ile maana toka moyoni …kazi za wengi hawazipendi ni kama kifungo maisha yaendelee…
Jiulize mtu anakwambia nikipata million kumi tuu hii kazi naacha hapo ndipo nilijua huyo mtu haipendi kazi yake…
Kabla ya kuangalia kipato ndo uchague kazi utakosa maana na huwezi kuendelea kufurahia kudumu kwenye kazi hiyo milele
Changamoto hazikomi kwenye maisha na kazi hivyo kazi zetu ukiipa maana bila kujali malipo na kuipenda inatakiwa iwe ni kama unavyopumua kuingiza hewa na kutoa hewa yahani ni sehemu ya maisha milele.
LikeLike
Asante Hendry,
Ni kweli kama usemavyo, kazi zimekuwa vifungo kwa wengi na ndiyo maana maisha ya wengi yana msongo.
Ndiyo maana sisi tunaopata maarifa haya hatupaswi kuruhusu hilo litokee kwetu.
LikeLike