Kuna wakati unafanya maamuzi bila ya kujua kwa nini unayafanya na yanaishia kuwa maamuzi sahihi. Hapo unajiambia kwamba machale yamekucheza na ukaona kitu ambacho huwezi kukielezea lakini ni sahihi.

Lakini pia kuwa wakati machale hayo hayo yanakupoteza, yanapelekea ufanye maamuzi ambayo siyo sahihi na yanayokugharimu.

Machale ni zile hisia unazozipata kuhusu kitu, ambazo huwezi kuzielezea lakini ndani yako unapata msukumo wa kipi sahihi au siyo sahihi.

Kwa kuwa zoezi la kufanya maamuzi siyo rahisi, na kwa kuwa hisia nyingi huwa zinaingilia zoezi hilo, ni vizuri kujua wakati gani wa kuyatumia machale yako na wakati gani wa kutokuyatumia.

Kuna vigezo vikubwa vitatu vya kuzingatia kabla hujayaamini machale yako na kuyatumia kufanya maamuzi.

Kigezo cha kwanza ni ukawaida wa jambo. Kwa jambo ambalo huwa linatokea kwa kujirudia rudia unaweza kuyatumia machale yako kufanya maamuzi. Kwa kuwa machale ni uzoefu wa kitu uliojijengea kwa muda mrefu, kama kitu kimekuwa kinajirudia rudia bila kubadilika, basi machale yako yanakuwa sahihi. Mfano mzuri ni kuendesha gari kuelekea eneo fulani unalopita kila siku, baada ya muda unajikuta umefika bila hata kufikiria wakati unaendesha. Lakini maamuzi mengi magumu huwa ni mapya kwetu na hata kama yanajirudia ni kwa namna ya tofauti, hivyo tunapaswa kuwa makini na machale.

Kigezo cha pili ni uzoefu ulionao kwenye kufanya maamuzi kwenye eneo husika. Hata kama jambo linajirudia rudia, uzoefu wako kwenye kufanya maamuzi na matokeo ambayo umekuwa unayapata unahitajika. Kila unapofanya maamuzi, matokeo unayoyapata yanajenga uzoefu fulani ndani yako. Hivyo unapojikuta kwenye hali kama ile ile, machale yako yanakukumbusha matokeo ambayo umewahi kupata huko nyuma na hivyo kujua hatua sahihi za kuchukua. Epuka kuamini machale pale ambapo huna uzoefu kwenye eneo husika.

Kigezo cha tatu ni mrejesho ambao mtu umekuwa unaupata kwenye eneo husika. Kwa yale matokeo ambayo unayozalisha, mrejesho unaoupata kutoka kwa wengine au kwa wewe mwenyewe kujifanyia tathmini unasaidia sana kujenga uzoefu mkubwa ndani yako. Hilo litafanya wakati mwingine ujue hatua sahihi za kuchukua kwa kuwa mrejesho uliokuwa unapata umekujenga zaidi. Hivyo hata kama una uzoefu wa kufanya kitu, kama hupati mrejesho sahihi unaweza kutumia uzoefu mbaya kama machale na ukafanya maamuzi yasiyo sahihi.

Zingatia vigezo hivyo vitatu kila unapojikuta kwenye hatua ya kufanya maamuzi makubwa na machale yako yanakuonesha hatua sahihi ya kuchukua. Tumia machale hayo kama vigezo hivyo vitatu vipo, kama havipo basi jipe muda wa kufikiri kwa kina ili uweze kufikia maamuzi sahihi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha