Ni watoto.
Malezi ni kazi kama zilivyo kazi nyingine. Usidharau kazi ya malezi, ifanye kazi ya malezi kwa moyo. Ulikubali mwenyewe kuwa baba au mama basi wajibika kuwaongoza vema watoto uliopewa.
Watoto wanahitaji kuoneshwa njia ili waweze kufika. Uko hapo ulipo sasa kwa sababu kuna mtu alikuonesha njia ya kupita. Na wewe ni jukumu lako kufanya hivyo.
Ukinunua simu au kifaa cha kieletroniki huwa unapewa na kijitabu cha namna ya kutumia kifaa hiko. Lakini kwenye binadamu pale anapopata mtoto inakuwa tofauti kabisa. Kwani hujapewa kijitabu cha namna ya kumlea mtoto wako unatakiwa kujifunza.
Usikubali mzazi au mlezi mtoto au watoto unaowalea wabaki kuwa kama walivyo siku zote. Huo utakua ujinga kama alivyowahi kusema Zig Ziglar kwamba, ujinga ni kufanya kitu kile kile kwa mtindo ule ule huku ukitegemea kupata matokeo tofauti. Usiwe mjinga kwenye malezi ya mtoto, jifunze namna ya kulea vizuri. Soma vitabu mbalimbali, viko vitabu vya kiimani kama vile Biblia na Kuruani. Mtume Mohammed na Yesu wanayo mafundisho mazuri sana ambayo ukiyatumia yatakusaidia kuwafanya watoto wako kuwa vizuri.
Watoto wanashindwa kuwa bora sana kwenye maeneo mbalimbali ya vipaji vyao kwa sababu ya wazazi wao kushindwa kuwajibika vema.
Wewe kama mzazi huwezi kuwa mzazi ambaye hujui kitu kabisa. Hata kama huna cha kumfundisha basi mpende kweli yule unayemlea hata siku aje kukumbuka kuwa ulimpenda.
Watoto wengi hawajui kusali. Shida inaanzia kwa wazazi. Huwa tunaalikwa kusali kwa pamoja sala za nyumbani lakini wanaofanya hivyo ni wachache sana. Tunawategemea walimu wa kiroho kuwafundisha bila kujua huo ni wajibu wa mzazi. Mtoto akipotea utakuja kudaiwa , ulikuwa wapi mpaka mtoto amepotea kwenye eneo fulani la maisha yake.
Mtoto akiharibika hasara siyo tu kwa mzazi bali ni kwa jamii nzima.
Watoto wanaweza endapo wakipewa msingi mzuri. Wakijengewa imani ya kuaminishwa kuwa wanaweza. Wazazi wanapotoa maneno mabaya kwa watoto yanawaharibu hivyo mwisho wa siku yale maneno yako mabaya unayomwambia yanakwenda kujengeka katika akili yake.
Kila siku unapotoka nyumbani hakikisha unamwambia mtoto wako neno moja chanya.
Ikiwezekana andika maneno hayo mazuri na mbandikie kwenye chumba chake akiwa anaingia na kutoka akikutana na neno “Mimi ni mtoto mwenyewe akili sana, mwenye bahati sana nk. Hawezi kubaki kama alivyo.
Hatua ya kuchukua leo; Fanya mapinduzi kwenye malezi ya watoto wako. Wafuatilie vizuri kwenye kila eneo la maisha yao.
Kama una watoto wadogo pata muda hata wa kuwakata kucha zao, unapofanya hivyo, mtoto anakuwa anapata kitu cha upendo kutoka kwako.
Wazazi wanaposhindwa kuwafuatilia watoto wao dunia itakusaidia lakini kwa maumivu makubwa. Utalipa gharama hiyo kwa riba kubwa. Jua kila kinachoendelea kwa mtoto wako awe mkubwa au mdogo bado mzazi anayo nafasi ya kurekebisha pale ambapo hapako sawa.
Makala hii imeandikwa na
Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali.
Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa
http://kessydeo.home.blog ,vitabu nakwenye klabu yake ya MIMI NI MSHINDI. Karibu sana.
Ukawe na siku bora sana rafiki.
Rafiki na mwalimu wako,
Mwl, Deogratius kessy
0717101505//0767101504
deokessy.dk@gmail.com //
Asante sana