2467; Mlango wa sita wa hisia.
Tumefundishwa sana kuhusu milango mitano ya hisia.
Macho yanayoona.
Pua inayonusa.
Ulimi unaoonja.
Masikio yanayosikia.
Ngozi inayohisi.
Hiyo ni milango inayoeleweka kirahisi na ndiyo maana inafundishwa bila tatizo.
Kuna mlango wa sita wa hisia ambao umekuwa haueleweki kirahisi jinsi unavyofanya kazi, ndiyo maana umekuwa haufundishwi.
Lakini ni mlango ambao upo na unafanya kazi kwa kila mtu.
Mlango huo ni machale ambayo mtu huwa unakuwa nayo.
Machale hayo huwa yanakujia, huwezi kuyaelezea jinsi yanavyokuja na wala yanamaanisha nini, ila huwa yanakuwa sahihi.
Unakutana na mtu na kitu ndani yako kinakuambia mtu huyo siyo sahihi. Lakini wewe unakipuuza na kwenda na mtu huyo. Baadaye unakuja kugundua kweli siyo sahihi.
Nafsi zetu zina kumbukumbu kubwa ya yale yote ambayo tumeshapitia tangu tukiwa watoto. Kumbukumbu ambazo akili zetu zimeshasahau kabisa.
Ndiyo maana nafsi inapoona kitu, inakuletea machale fulani, maana ina kumbukumbu ya jinsi kitu cha aina hiyo kilienda huko nyuma.
Kwa bahati mbaya watu hushindwa kutofautisha machale na hisia. Hisia huwa ni mhemko tu wa muda, ambao huwa unapita. Lakini machale ni kitu cha ndani, uzoefu ambao unao lakini huwezi kuuelezea, na machale huwa siyo ya kupita.
Machale yanahitaji mtu uwe umejijengea uzoefu mkubwa kwenye kitu husika. Mfano kama ndiyo unaanza biashara, hujawa na uzoefu wa kutosha kuwa na machale ambayo ni mazuri. Lakini mtu aliyefanya biashara kwa miaka kumi, ana machale yenye manufaa. Kuna uzoefu mwingi ameshakuwa nao ambao hata ameshasahau, lakini nafsi yake haisahau.
Kadhalika mtu huyo huyo ambaye ana uzoefu wa miaka 10 kwenye biashara fulani, machale yake hayawezi kuwa na msaada kwenye biashara nyingine tofauti na hiyo, kwa sababu bado hajajenga uzoefu wa kutosha kwenye biashara hiyo nyingine.
Kumekuwa na ushauri mwingi wa watu kuamini nafsi (machale) yao. Lakini ambacho watu wamekuwa hawaambiwi ni machale sahihi yanahitaji uzoefu uliojengeka. Na pia unapaswa kutofautisha machale na hisia.
Hatua ya kuchukua;
Kwa kila maamuzi unayofanya kwenye maisha yako, kuna sauti ya ndani inakuambia kama ni sahihi au siyo sahihi. Ichunguze sauti hiyo ya ndani kwa kuangalia msukumo wake na uzoefu wako kwenye jambo unalofanyia maamuzi hayo. Ondoa kila tamaa za kunufaika unazokuwa nazo na ona kama bado sauti hiyo inabaki, hayo yanakuwa machale na siyo hisia. Na kama ni eneo ambalo tayari una uzoefu nalo basi ni machale sahihi. Yasikilize na chukua hatua sahihi, utaepuka mengi yasiyo sahihi.
Tafakari;
Ni vizuri kusikiliza nafsi (machale) yako, lakini hakikisha siyo hisia tu zinakusukuma na pia kuwa na uzoefu kwenye eneo hilo.
Kocha.
Asante Sana kocha.
LikeLike
Nashukuru sana hapa nimenifunza kitu kikubwa sana hii ni elimu ya kiroho kabisa
LikeLike
Karibu sana.
LikeLike