2526; Mtego wa mateso.

Haya maisha huwa yana mitego ya mateso ambayo usipoijua utaishi maisha ya kuteseka sana.

Mitego hii haijaanza sasa, wanafalsafa wa kale waliielewa sana na wakawa na mafunzo ya kuwatahadharisha watu.

Kuna mifano mikubwa miwili ya mafunzo ya kale yanayoonyesha mitego hii.

Wa kwanza ni Promethus ambaye aliiba moto kwa miungu na kuuleta kwa wanadamu.
Miungu ikakasirika na kumpa adhabu ya kufungiwa kwenye jiwe, kisha mwewe kula ini lake akiwa hai.
Usiku ini hilo linaota tena na mchana linaliwa tena na mwewe.

Wa pili ni Sisyphus ambaye aliikaidi miungu naye akapewa adhabu ya kusukuma jiwe kubwa kupanda kwenye kilima, likifika juu linarudu tena chini na anarudia zoezi hilo. Muda wote anakuwa anasukuma jiwe bila kupumzika.

Mifano hii ina funzo kubwa kuhusu baadhi ya vitu tunavyofanya kila siku, tukiona kama ni sehemu ya maisha, kumbe ni mtego tumenasa.

Angalia kitu kama ulevi, wakati mtu anaanza inaweza kuwa kama burudani, lakini kadiri anavyokwenda inakuwa adhabu kubwa. Asipotumia hajisikii vizuri na hata akitumia pia hajisikii vizuri.

Angalia pia mitandao ya kijamii, wakati mtu anaanza kuitumia anaona ni kitu kizuri, baadaye inageuka kuwa kitu kinachopoteza muda. Lakini pia hawezi kuacha kutumia, maana anaona atapitwa na mengi kama hataingia kwenye mitandao hiyo.

Kuna mengi watu wanahangaika nayo kila siku, ambayo hayana tija yoyote kwao, huo ndiyo mtego wa mateso.

Hatua ya kuchukua;
Tafakari ni vitu gani umekuwa unavifanya kila siku bila kukosa lakini havina mchango wowote kwenye mafanikio yako. Chagua sasa kuteseka kwa kutokuvifanya, badala ya kuvifanya ili kuepuka mateso halafu uishie kuteseka zaidi.

Tafakari;
Mwanzo wa kitu chochote kile huwa ni raha, mwendelezo huwa ni karaha. Kama kitu hakina manufaa, ni bora hata usianze kukifanya. Maana kinga ni bora na rahisi kuliko tiba.

Kocha.