3140; Chukua picha nyingi zaidi.

Rafiki yangu mpendwa,
Siku moja ya tarehe 10 Disemba mwaka 1914, Thomas Edison akiwa nyumbani kwake alipata taarifa kwamba maabara yake kubwa ilikuwa inaungua moto.
Aliongozana na kijana wake kwenda kuangalia hilo na kukuta kweli maabara ikiteketea kwa moto.
Baada ya kuona kinachoendelea, Edison aligeuka na kumwambia kijana wake; “Nenda kamwite mama yako na marafiki zake wote, hawatakuja kuona moto mkubwa kama huu tena.”

Kuna mengi sana ya kujifunza kupitia namna Edison alivyokabiliana na taarifa hiyo mbaya.
Lakini moja muhimu sana ambalo nataka wote tuondoke nalo hapo ni umuhimu wa kuweka kumbukumbu kwa hali zote ngumu tunazopitia, kwa sababu hazitakuja kujirudia tena.

Kuna hatua nyingi ngumu ambazo tunakuwa tunapitia kwenye hii safari yetu ya mafanikio.
Hatua ambazo nyingi hatutakuja kuzirudia tena.
Lakini pia ambazo zitatengeneza hadithi nzuri sana ya kule tulikotoka mpaka tulikofika.

Njia nzuri kwa hizi zama zetu ya kuweka kumbukumbu za hatua zote tunazopitia ni kuchukua picha za kila hatua tunayopitia.
Simu zetu za mkononi ni kifaa kinachoweza kuchukua picha nzuri sana.
Na pia tuna mitandao ambapo tunaweza kutunza picha zetu zisipotee, hata pale tunapopoteza simu zetu au vifaa vingine vyenye hizo picha.

Hivyo basi, wajibu wetu ni kuchukua picha nyingi zaidi za hali zote tunazopitia.
Chukua picha ya biashara yako tangu ikiwa ndogo na kadiri inavyoendelea kukua.
Chukua picha na watu unaoshirikiana nao tangu hatua za chini kabisa, washirika, wafanyakazi, wateja n.k.
Chukua picha za eneo unaloishi na kufanyia kazi zako.
Chukua picha ya salio lako la benki na uwekezaji kama wa UTT kwa hatua zote tangu unapoanzia chini na unavyoendelea kwenda.
Kwa kifupi, chukua picha za kila kitu unachopitia sasa na unachoendelea kupitia kwenye safari yako ya kujenga mafanikio makubwa.

Zoezi la kuchukua picha kama sehemu ya kumbukumbu za maisha siyo geni, lilikuwepo sana tangu zamani.
Lakini zama hizi za simu janja na mitandao tunalichukulia poa, wakati ndiyo tungepaswa kulipa uzito zaidi.
Kwani kwa zama hizi unaweza kuchukua na kutunza picha nyingi zaidi na kwa gharama ndogo zaidi.
Lakini pia unaweza kuchukua na kutunza sauti pamoja na video za kila hatua unazopita.

Unachukua na kutunza hayo kwa kumbukumbu zako binafsi na vizazi vyako.
Lakini muhimu zaidi ni kuna watu watakuja kuongea ujinga sana siku za mbeleni huko utakapokuwa umefanikiwa.
Watasema una bahati au kuna namna ulipita njia za mkato.
Wajinga kama hao huhitaji kubishana nao kwa maneno, bali kwa kuonyesha ushahidi wa picha ulizochukua kwenye kila hatua.
Japo siyo lengo, lakini ni hadithi nzuri na yenye nguvu.

Lakini pia sisi binadamu huwa tuna tabia ya kusahau mambo haraka.
Tunaweza kutokea chini kabisa, tukapambana na kufika juu, halafu tukajisahau, kitu kinachotupa anguko kubwa.
Kwa kuwa na kumbukumbu halisi za kule tulikotoka, ambazo tunaziangalia mara kwa mara, tunakuwa wanyenyekevu na kuendelea kuweka juhudi bila kuruhusu mazoea.

Na kama kuna picha zako za nyuma ambazo ulipiga na zikachapwa kwa nakala ngumu, zigeuze kuwa nakala laini na tunza kwenye maeneo uliyochagua ya kutunza picha zako ili zisipotee.

Kitu kimoja tunachokijua bila ya shaka yoyote ni kwamba tutapiga hatua kubwa sana zaidi ya pale tulipo sasa.
Ni muhimu sana tuweke kumbukumbu zetu sawa kwa kila hatua tunayopiga kwa ajili ya matumizi mazuri ya baadaye.
Kwa sababu ni hatua ambazo hatutakuja kuziona tena na wale tunaokuja kukutana nao huko mbele pia hawatakuwa wameziona.

Haijalishi umefanikiwa kiasi gani, hakikisha una kumbukumbu zote za hatua ulizopitia kufikia mafanikio hayo.
Hilo litakusaidia kuendelea kuwa mnyenyekevu na hata kuwaonyesha wengine ambao hawakuwepo wakati unapiga hatua hizo.
Hivyo chukua picha nyingi zaidi kwa kila hatua unayopiga kwenye maisha yako, ni muhimu sana kwa maendeleo yako.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe