3226; Biashara ambayo upo.

Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye harakati zetu za kupata mafanikio tunayoyataka, huwa tunahangaika na mambo mengi sana.

Kwa sababu tunakuwa tunayataka sana matokeo na kwa haraka, huwa tunaona kama tumechelewa sana.
Hivyo tunakazana kuharakisha kwa kuhangaika na mambo mengi.

Kila fursa ambayo tunaiona au kuisikia tunaiendea kwa kuona hiyo ndiyo yenye matokeo tunayokuwa tunayataka sana.

Kwa haraka tunayokuwa nayo ya kupata matokeo, tunaishia kupoteza muda na nguvu na kuishia kuchelewa.

Tunahangaika na mambo mengi kwa lengo la kuharakisha safari, lakini matokeo yake ni kuchelewa zaidi.

Dawa ya hili ni moja tu, fokasi.
Kuweka umakini wako wote kwenye kile ambacho unakifanya mpaka kikupe kile hasa unachotaka.

Kuna kauli huwa inasema jali biashara yako (mind your business).
Kauli hii ina maana kubwa sana kama itafanyiwa kazi.
Unaifanyia kazi kauli hiyo kwa kujua biashara ambayo upo kisha kuipa hiyo umakini wako wote.
Mengine yote unayapuuza na kupambania hilo moja pekee.

Unakaa kwenye kile ambacho unajua ndiyo unachofanya.
Kila unachofanya, kinakuwa kinahusisha hicho kikuu moja kwa moja na siyo nje ya hapo.
Huhangaiki na kila kinachokuja mbele yako, hata kama ni rahisi kiasi gani.

Nguvu na umakini utakaoutawanya kwenye mambo mengi, ukikusanya kwenye biashara yako kuu moja, utazalisha matokeo makubwa na ya tofauti kabisa.

Unazo fursa za kufanya kwa mitindo tofauti.
Unaanza na wingi, ambapo unaongeza kiwango chako cha ufanyaji. Kwa mfano kufanya mara kumi ya ulivyozoea kufanya.
Kisha unaenda kwenye kufanya kwa ubora, ambapo unaboresha zaidi vile unavyofanya.
Na mwisho ndiyo kufanya kwa upya.

Wengi huwa wanakimbilia kuboresha kabla ya kufanya kwa wingi.
Wanaishia kushindwa na kukosa kujifunza pia.
Kwa sababu wanakuwa hawajui nini kimepelekea washindwe, kiwango chs ufanyaji au ubora.

Kabla hujafanya kitu chochote tofauti au kipya, hebu fanya hicho hicho kwa ukubwa zaidi.
Fanya angalau mara 10 ya unavyofanya sasa kwa muda mrefu.
Kisha angalia matokeo unayopata.

Jua biashara ambayo upo na itendee kwanza haki kabla hujahangaika na mambo mengine.
Kuna hazina kubwa unayoiacha hapo ulipo sasa na kukimbilia vitu vipya.
Achana na hilo kwa sasa na kaa kwenye biashara ambayo upo kwanza.

Kila wakati jikumbushe kujali biashara yako na kufanya yale unayofanya kwa wingi kwanza kabla ya kubadili chochote.
Mara nyingi unakwama kutokana na kufanya kwa udogo kile ambacho tayari unakifanya.
Ukiongeza tu wingi, unajiweka kwenye nafasi ya kupata matokeo makubwa na bora.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe