3268; Adui yako mkuu.

Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye mafunzo mengi ya maendeleo binafsi, watu wamekuwa wanaambiwa wakitaka kumjua adui yao mkuu basi wasimame mbele ya kioo.
Mtu anaposimama mbele ya kioo, anajiona yeye mwenyewe.
Dhana kuu hapo ni kwamba adui mkuu wa mtu ni mtu mwenyewe.

Ni kweli adui wa kwanza kwa mtu kufika kule anakotaka kufika ni mtu mwenyewe. Lakini kwa kuishia hapo, wengi hawaelewi na hivyo hawachukui hatua sahihi za kumshinda adui huyo ili waweze kufanya makubwa.

Leo nakwenda kukuonyesha ni jinsi gani umekuwa adui yako mwenyewe kwa mambo ambayo umekuwa unayafanya na jinsi ya kujishinda wewe mwenyewe ili uweze kufanya makubwa.

Ukweli ni kwamba, kila mmoja wetu anao uwezo wa kufanya makubwa sana ndani yake. Uwezo ambao ni mkubwa sana ila umekuwa hautumiki kwa usahihi.
Na hapo ndipo uadui wa mtu kwake mwenyewe unapoanzia, kwa yeye mwenyewe kujizuia kutumia uwezo mkubwa ambao tayari upo ndani yake.

Watu wengi wamekuwa wanaendesha maisha yao kwa mazoea na kuwaiga watu wengine. Kwa njia hii wamekuwa wanajizuia kutumia uwezo wao mkubwa kuzalisha matokeo ya tofauti.

Kuna sifa tatu ambazo ndiyo zimekuwa zinawafanya watu kuwa maadui kwao wenyewe. Hizi ni sifa ambazo watu wanazo kwa mazoea ila ni kikwazo kikubwa kwao. Unapaswa kuzijua na kuzivunja ili zisiwe kikwazo kwako.

Sifa ya kwanza ni kutokujiamini. Kwenye haya maisha, kama hujiamini, hakuna chochote kikubwa utakachoweza kufanya. Hiyo ni kwa sababu kuna hali kubwa ya kukatishwa tamaa inayokuwa inaendelea kwenye kila ambacho mtu anafanya. Ni kupitia kujiamini, tena kwa kupitiliza ndiyo mtu anaweza kuvuka vikwazo mbalimbali na kufanya makubwa.

Hatua ya kuchukua hapa ni kuhakikisha unajiamini sana wewe mwenyewe. Kwa chochote kikubwa unachotaka, amini bila ya shaka yoyote kwamba utakipata. Usijali ni magumu kiasi gani unapitia, weka imani yako imara kwenye kile unachotaka na uwezo mkubwa ulio ndani yako na utaweza kukipata.

Sifa ya pili ni kukata tamaa haraka. Pale watu wanapochukua hatua kwenye kile wanachotaka, lakini wakakutana na magumu na changamoto, huwa wanaona hawawezi kuendelea. Hapo ndipo wanakata tamaa na safari kufika tamati. Wanachagua kurudi kwenye mazoea yao na kuiga wengine. Kukata tamaa haraka imeua ndoto kubwa ambazo wengi wamekuwa nazo.

Hatua ya kuchukua hapa ni kutokukata tamaa kamwe, bila ya kujali unapitia nini. Ukishachagua kile unachotaka kupata na kule unakotaka kufika, hupaswi kuishia njiani. Bali unapaswa kupambana kwa kila namna mpaka kupata kile unachotaka. Unapokutana na magumu hupaswi kuacha, bali unapaswa kuyavuka ili upate unachotaka. Mambo makubwa hayajawahi kuwa rahisi, hivyo ni muhimu sana uwe tayari kuukabili ugumu bila ya kuyumbishwa na kukata tamaa.

Sifa ya tatu ni kutokuweka juhudi za kutosha. Hapa ndipo watu wengi huwa wanashangaza sana. Watu wanakuwa na malengo makubwa, lakini wanafanya kazi sawasawa na wale ambao hawana malengo makubwa. Wanaanza kazi kwenye muda wa kawaida na kumaliza kwenye muda wa kawaida. Wamasisitiza kuwa na usawa wa kazi na maisha. Huwezi kutaka kupata makubwa halafu ukaweka juhudi sawa na wale wanaofanya kawaida. Unapotaka kufanya makubwa, kipaumbele chako pekee kinakuwa ni kazi na muda wako wote unapokuwa hujalala unautumia kufanya kazi. Kunakuwa hakuna kingine chochote kinachokusumbua isipokuwa kazi yako kuu uliyochagua.

Hatua ya kuchukua hapa ni kuweka juhudi kubwa sana kwenye kile ulichochagua kufanya. Kifanye kuwa kipaumbele pekee kwenye maisha yako na puuza mengine yote ambayo hayana mchango kwenye lengo lako kubwa unalokuwa nalo.

Ukiweza kuyavuka hayo matatu ambayo yamekuwa yanakukwamisha sana, utaacha kuwa adui yako mwenyewe na kuweza kufanya makubwa.
Uzuri ni hayo yote yapo ndani ya uwezo wako hivyo ukiwa tayari kuyafanyia kazi utaweza kufanya mabadiliko makubwa kwenye maisha yako.

Haijalishi unaanzia wapi, unaweza kufanya makubwa sana kama utaweza kufikia na kutumia uwezo mkubwa ulio ndani yako. Chukua hatua sasa ili uache kuwa adui yako wewe mwenyewe.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe