3299; Uhakika wa kushinda au kushindwa.

Rafiki yangu mpendwa,

Kwenye maisha, kushinda au kushindwa ni vitu ambavyo mtu anachagua mwenyewe.
Hayo huwa siyo matokeo ya nje kama wengi wanavyodhani.
Bali ni maamuzi ya ndani ya mtu mwenyewe.

Mtu anakuwa na uhakika wa kushindwa pale;
1. Anaposema anajaribu kufanya kitu. Kujaribu kufanya kitu ni kukubali kushindwa. Maana majaribio yanapokea kushindwa kama sehemu ya matokeo.
Kuondokana na hilo acha kuwa mtu wa kujaribu na fanya. Mara zote fanya kwa uhakika na utaweza kufanya kwa ushindi.

2. Unapokuwa na machaguo mengi mbadala. Pale unapokuwa na machaguo mengi mbadala ya vitu vya kufanya pale kile unachoanza nacho kinashindwa, ni kukubali kushindwa. Huwezi kupambania kitu hasa kama una machaguo mengi mbadala. Unapokutana na magumu na changamoto, unakimbilia kwenye chaguo jingine na siyo kukomaa na kile unachofanya.
Kuondokana na hilo futa machaguo yote mbadala uliyonayo na komaa na kitu kimoka pekee. Kitu hicho kimoja kipe kila kinachopaswa kutolewa ili kupata matokeo ya uhakika.

3. Unapokataa kulipa gharama halisi ya mafanikio unayotaka. Kila kitu kwenye maisha kina gharama, hakuna chochote kinachopatikana bure. Kadiri mtu anavyotaka mafanikio makubwa, ndivyo pia gharama ya kulipa inavyokuwa kubwa.
Kwenye mafanikio, gharama kubwa ya kulipa ni kutoa kafara. Hapo ni kuachaba na vitu vizuri na unavyopenda lakini ni kikwazo kwako kupata mafanikio makubwa unayoyataka.
Kuondokana na hilo kuwa tayari kulipa kila aina ya gharama unayopaswa kulipa ili kupata unachotaka. Toa kafara ya kila kitu ili upate mafanikio makubwa unayoyataka.

Ni pale unapokitaka kitu hasa, huku ukiwa huna namna nyingine ndiyo unakuwa umejitoa hasa kufikia mafanikio makubwa.
Kingine chochote nje ya hapo ni kukubali kushindwa kwa uhakika.
Wewe ikatae kabisa hiyo njia ya kushindwa ili uweze kupata ushindi wa uhakika kwenye maisha yako.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe