3395; Unachofikiria wakati huna cha kufikiri.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Watu wanaweza kusema mambo mengi juu ya yale wanayofanya au kutaka.
Lakini wengi huwa siyo wakweli kwenye yale wanayosema.

Wanaweza kusema wanayataka sana mafanikio makubwa.
Wanaweza kuonyesha kwamba wanaweka juhudi kubwa ili kuyapata mafanikio hayo.
Pia wanaweza kulalamika kwamba licha ya kuweka juhudi, bado hawapati matokeo mazuri.

Kuujua ukweli wa watu siyo rahisi kwa sababu mambo mengi yapo ndani yao.
Lakini kuna njia moja ya karibu inayoweza kutuonyesha kama mtu ni mkweli.
Njia hiyo ni kulinganisha matokeo ambayo mtu anapata na yale anayosema kwamba anafanya.

Kama matokeo yanaendana na yale anayosema, basi mtu huyo ni mkweli.
Lakini kama matokeo ni tofauti kabisa na yale anayofanya, siyo mkweli kwenye hayo anayosema.

Huwa wanasema kimtokacho mtu ndiyo kilichomjaa.
Matokeo ambayo mtu anayapata, ni zao la fikra anazokuwa nazo muda mrefu.
Hivyo mtu anaweza kusema mengi atakavyo, lakini matokeo yatamsaliti.
Matokeo yataonyesha ni vitu gani mtu huyo amekuwa anavifikiria muda mwingi zaidi.

Matokeo ambayo watu wanayapata yanatokana na vitu wanavyokuwa wanavifikiria muda wote.
Yaani hapo ni yale ambayo watu huwa wanayafikiria pale wanapokuwa hawana cha kufikiria.
Pale wanapokuwa huru na mawazo yao, mawazo hayo makuu bado yanakuwa hayawezi kuwaacha.

Watu pekee wanaokifikiria kitu kwa muda mrefu ni wale wanaokipenda kitu hicho kuliko vitu vingine vyote.
Wale ambao wanakuwa na mapenzi ya dhati kwenye kitu kiasi kwamba hakiwezi kutoka kwenye fikra zao.
Hao ndiyo wanaoyapata mafanikio makubwa sana, bila ya kujali wanaanzia wapi.

Hilo ndiyo linalopelekea watu wanaokuwa wanafanya kitu kimoja, kwa namna inayofanana kupata matokeo yanayotofautiana kabisa.
Tofauti ya matokeo inaanzia kwenye kufikiri.
Wale wanaofanikiwa sana wanakuwa wanafikiria kuhusu kitu muda wote, hata muda ambao wanakuwa hawakifanyi.
Lakini wale wasiofanikiwa huwa wanafikiria kitu wakati wa kukifanya tu. Wakati ambao hawakifanyi, huwa hawakifikirii kabisa.

Kuwa na mipaka kwenye kukifikiria kitu kunakupa matokeo yenye ukomo.
Kwa sababu akili haipati nafasi ya kukielewa kitu kwa undani kama mawazo yanakatishwa kila mara.

Kutokuwa na mipaka kwenye kufikiri kitu kunakupa matokeo yasiyo na ukomo.
Akili inapofikiria kuhusu kitu muda wote, inakuwezesha kuziona fursa za tofauti zenye mchango kwenye kitu hicho.

Rafiki, swali kwako ni je huwa unafikiria nini kwenye nyakati ambazo huna cha kufikiri?
Ukishtuka kutoka usingizini usiku wa manane, ni fikra gani zinazokuwa zimetawala akili yako?

Kama kuna kingine unachokipa nafasi kuliko mafanikio makubwa unayoyataka, jua hilo litakuwa kikwazo kuyapata mafanikio hayo.

Hakikisha wakati wote unatawaliwa na fikra za mafanikio makubwa sana unayoyataka.
Kuwa na taswira ya mafanikio yako ambayo unaipitisha kwenye fikra zako mara kwa mara.
Kuwa na mazingira yanayokukumbusha kuhusu mafanikio yako makubwa mara zote.
Weka alamu kwenye simu yako ili mara kwa mara ukumbushwe kuhusu mafanikio yako makubwa.

Ukiweza kudhibiti akili yako ifikirie kuhusu mafanikio makubwa unayoyataka muda wote, ufapata msukumo mkubwa sana wa kuyafikia.
Hili lipo ndani ya uwezo wa kila mmoja wetu, wajibu wetu ni kulifanyia kazi ili kunufaika nalo.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda sana,
Kocha Dr. Makirita Amani.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe