Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Eneo la maarifa na hamasa ya mafanikio kwa sasa lipo vizuri sana. Kila mtu anayetaka mafanikio kwenye jambo lolote lile, ana fursa nyingi za kujifunza na kuhamasika ili kufanikiwa.
Siri zote za mafanikio kwa sasa zipo bayana. Hakuna tena kilichofichwa kuhusu mafanikio. Mtu yeyote anayetaka mafanikio, anaweza kujua chochote anachotaka kuhusu mafanikio hayo. Hakuna tena taarifa zinazohodhiwa na watu wachache.
Hadithi za watu waliofanikiwa ni nyingi na za kuhamasisha na kusisimua. Kwa yeyote anatetaka mafanikio, zipo hadithi zinazoendana na yeye kabisa. Hadithi za watu walioanzia chini kuliko hata yeye, wakapitia magumu sana, lakini wakapambana na kufanikiwa.
Pamoja na mambo hayo yote kuwa rahisi, bado wanaofanikiwa wanabaki kuwa wachache, huku wengi wakibaki kwenye hali za chini au wakijitahidi sana kuwa kawaida.
Hii ni hali ambayo watu wengi wanaipitia, wanapambana sana kujiboresha, wanasoma kila kitabu wanachoambiwa, wanahudhuria semina na mafunzo mbalimbali. Wanachukua hatua kwenye yale wanayojifunza, lakini bado maisha yao hayabadiliki.
Ni jambo ambalo linawaacha wengi wakiwa wamekwama, wasijue nini cha kufanya ili waweze kutoka kwenye mkwamo huu.
Kwenye hii #BaruaYaKocha unaenda kujifunza sababu zinazokukwamisha kufanikiwa licha ya juhudi kubwa unazoweka kwenye kujiboresha. Kwa kujua sababu hizo na kuzifanyia kazi, juhudi zako zitaweza kuleta mabadiliko unayotaka.

1. Almasi Ndani Ya Tope Bado Ni Sehemu Ya Tope.
Almasi ni moja ya madini yenye thamani kubwa sana duniani. Madini haya huwa yanapatikana chini ardhini, yakiwa ndani ya miamba na matope mengi. Ili almasi hiyo iwe na thamani, inaondolewa kwenye hilo tope, inasafishwa vizuri na kupelekwa mahali safi ambapo thamani inaonekana.
Kama almasi itatolewa kwenye tope, ikasafishwa vizuri kabisa na kisha ikarudishwa kwenye tope, bado inabaki kuwa sehemu ya tope. Pamoja na uwezo mkubwa wa thamani unaokuwa ndani ya almasi hiyo, kwa kuwa ipo kwenye tope, inaonekana kama tope tu.
Hicho ndiyo kimekuwa kinaendelea kwenye maisha yako kwa harakati zako za kuyaboresha. Umetambua maisha yako yana thamani kubwa. Kupitia kujifunza na hamasa, umeboresha thamani hiyo zaidi na zaidi. Lakini tatizo ni moja tu, bado umebaki kwenye tope.
Tope ambalo umebaki ni mazingira na mifumo ambayo umekuwa ndani yake kwa kipindi chote cha maisha yako. Mazingira na mifumo hiyo imekuwa inafifisha thamani yako, lakini wewe hutambui hilo. Unaendelea kukazana sana kujiboresha, lakini matokeo yako ni yale yale.
Ni wakati sasa wa kutambua tope linaloshusha thamani kubwa unayoitengeneza kupitia harakati zako za kujiboresha. Ni kwa namna gani unaendelea kujizuia kupata matokeo ya tofauti licha ya kuweka juhudi kubwa sana? Hapo ndipo pa kuanza kutafakari ili uweze kuyabadili maisha yako kwa uhakika.
2. Unajiboresha Sana, Lakini Umenasa Hapo Hapo.
Umejifunza siri nyingi za mafanikio na kuzifanyia kazi, lakini bado huoni mabadiliko makubwa kwenye maisha yako.
Umefuatilia tabia za watu wenye mafanikio makubwa na kujijengea tabia hizo, lakini huoni zikileta matokeo ya tofauti.
Umehangaika na mengi, kuamka mapema, kusoma vitabu, kufikiri na kujinenea chanya, kujituma kwenye kazi, kujenga mahusiano mazuri na mengine mengi. Lakini bado matokeo unayopata ni yale ambayo umekuwa unapata mara zote.
Tatizo siyo kwamba mambo hayo hayafanyi kazi, yanafanya sana, ndiyo maana umejifunza kwa wengine ambao wanayafanya na wanapata matokeo.
Wewe hupati matokeo kwa sababu ya hapo uliponasa. Thamani yote unayojitengenezea kwa hayo unayofanya haiwezi kuonekana kwenye mazingira ambayo upo.
Ndiyo maana umekuwa unahangaika sana, na mpaka watu wanakushangaa, lakini bado hakuna kinachobadilika. Hata wewe mwenyewe uwe bora kiasi gani, kuna vitu vya nje yako vinavyoathiri matokeo yako ambavyo huwezi kuvibadili kwa juhudi zako.
Vitu hivyo ni vya kuachana navyo, kuondokana navyo kabisa ili thamani uliyojenga iweze kuonekana. Vitu hivyo ni kama magugu yanayozuia mazao yasipate rutuba na kuzalisha vizuri. Unahitaji kuondoka kabisa kwenye magugu hayo kama unataka kupata matokeo ya tofauti.
Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK088; Hii Ndiyo Sababu Ya Maisha Yako Kutokubadilika Licha Ya Kupambana Sana Kujiboresha