Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Tunaishi kwenye dunia inayokwenda kwa kasi kubwa sana. Maendeleo makubwa ya teknolojia yamerahisisha sana mambo yote ambayo binadamu tunayafanya.
Mtu aliyefariki karne ya 19 na hata ya 20, akifufuka leo na kuona hatua ambazo zimepigwa, atadhani maisha ya watu yako vizuri sana. Lakini atakapopata nafasi ya kuangalia maisha halisi ya watu, ataona bado hayana tofauti kubwa na yale waliyoishi wao.
Ujio wa Akili Unde (AI) umemwezesha kila mtu kuweza kufanya kitu chochote anachotaka. Hata kama mtu hana uwezo na ujuzi mkubwa, kwa kuweza kuielekeza vizuri AI, anaweza kupata matokeo asingeweza kuyapata yeye mwenyewe.
Lakini pamoja na fursa hiyo kubwa ya kila mtu kuweza kufanya chochote anachotaka, bado swala la mafanikio limekuwa mtihani mgumu. Bado watu wanaofanikiwa wanabaki kuwa wachache, huku wengi wakiyatamani mafanikio, lakini wanashindwa kuyapata.
Kila mtu sasa ana zana za kumwezesha kufanya chochote kitakachompa mafanikio anayoyataka. Lakini wengi wanashindwa kutumia zana hizo, kwa kutokujua kitu muhimu kuhusu mafanikio.
Kitu hicho ni mafanikio kutaka sana uzito, wakati dunia inahadaa na wepesi. Hapo ndipo penye mtihani mkubwa. Wakati tuna zana nyingi za kurahisisha mambo, tunaishia kuyafanya kwa wepesi. Wakati huo, mafanikio bado yanataka uzito, ambao tunaweza kuupata kwa zana tulizonazo, ila siyo kwa urahisi kama tunavyotaka.
Kwenye hii #BaruaYaKocha naenda kukukumbusha umuhimu wa uzito kwenye mafanikio na kukuongoza kutengeneza uzito ambao utakupa mafanikio makubwa. Na kwa zana nzuri zilizopo sasa, ukishauelewa uzito, inakuwa swala la muda tu kwako kupata mafanikio makubwa unayoyataka.

1. Mafanikio Yanayodumu Ni Yenye Uzito
Mwembe na mninga ni mimea. Ukiipanda kwa wakati mmoja, mwembe utakua haraka na kuanza kutoa matunda. Mninga utachukua muda mrefu zaidi mpaka uwe mti mkubwa. Miti hii ikikomaa na ukachana mbao, kisha ukatumia mbao hizo kutengeneza samani, zinazotengenezwa kwa mninga zitakuwa na uzito zaidi kuliko zinazotengenezwa kwa mbao za mwembe. Na zaidi, samani iliyotengenezwa kwa mbao ya mninga itadumu muda mrefu kuliko iliyotengenezwa kwa mbao ya mwembe.
Huo ni mfano mmoja rahisi kueleweka, lakini maisha yetu yanajengwa na mifano mingi ya aina hiyo. Kitu chochote kinachodumu ni kile ambacho kina uzito na ili uzito huo upatikane, lazima kazi kubwa ifanyike kwa muda mrefu.
Hivyo ndivyo ilivyo kwenye kila kitu kwenye maisha yetu. Vitu ambavyo gharama yake ni ndogo na vinapatikana kwa urahisi huwa ni vyepesi, na vinaisha au kuharibika haraka. Na vitu ambavyo ni imara na vinavyodumu muda mrefu huwa ni vizito na vina gharama kubwa.
Ieleweke tunapozungumzia uzito siyo tu kwa kilo, bali kwa ubora na uimara wa kitu. Kama ambavyo ukiulizwa kilo moja ya pamba na kilo moja ya chuma ipi nzito zaidi, kwa haraka unaweza kusema chuma. Lakini kumbuka zote ni kilo moja, kwa sababu ni kipimo sawa. Ila unapoangalia, utaona kilo moja ya chuma inachukua ujazo mdogo kuliko kilo moja ya pamba. Hiyo ndiyo maana ya uzito tunaozungumzia kimafanikio.
2. Dunia Ina Mitego Mingi Ya Vitu Vyepesi
Uzito, unaotokana na uimara na ubora ndiyo kanuni ya asili ya kudumu kwa vitu. Lakini dunia imekuwa inatuhadaa na vitu vyepesi. Kwa sababu watu wanataka matokeo ya haraka, basi wanajikuta wananasa kwenye vitu vyepesi, ambavyo vinaweza kupatikana haraka. Na kama ilivyo kanuni, kadiri vitu vinavyopatikana haraka, ndivyo pia vinavyopotea haraka.
Kila mtu anakimbizana na vitu vya haraka, mafanikio ya haraka, utajiri wa haraka, vyakula vya haraka, umaarufu wa haraka na mengine. Na wote tunaona jinsi ambavyo vitu hivyo vinavyopatikana kwa haraka vinavyopotea haraka pia. Vitu ambavyo havina uzito haviwezi kuhimili misukosuko ambayo vinakutana nayo.
Kanuni ya kujenga maisha yenye mafanikio ni kujenga tabia na nidhamu sahihi, kitu kinachochukua muda kutokea. Lakini dunia inakuhadaa na njia za mkato za kuchukua ili upate matokeo, ambayo hata ukiyapata yanapotea, kwa sababu tabia zako zinakuwa hazijabadilika.
Kanuni ya kujenga utajiri unaodumu ni kipato kuzidi matumizi, kuweka akiba na kuwekeza kwa muda mrefu bila kuacha. Lakini dunia inakuhadaa na njia za mkato kama kucheza kamari na bahati nasibu, kusubiri mirathi au kuchukua mikopo mikubwa. Hata pale mtu anapopata fedha kwa njia hizo, huwa hazidumu.
Kanuni ya kujenga biashara inayodumu bila kukutegemea mwanzilishi ni kuwa na mifumo bora ya kuendesha biashara na kuajiri watu wazuri ambao wanapata mafunzo na usimamizi mzuri. Lakini dunia inakuhadaa kwa njia za mkato za kufanya kila kitu mwenyewe ili usisumbuke na watu.
Chochote ambacho dunia inakuonyesha ni njia rahisi na ya haraka ya kupata mafanikio, jua ni kitu ambacho hakina uzito. Na matokeo yoyote utakayoyapata kwa kutumia njia hiyo, jua hayawezi kudumu.
Unaweza kudhani wewe ni mjanja sana na unaweza kuzuia hilo. Lakini kama ambavyo huwezi kuifanya mbao ya mwembe ikadumu kuliko ya mninga, ndivyo ambavyo huwezi kufanya mafanikio ya haraka yakadumu kwa muda mrefu. Ni kanuni za asili hizo, hakuna namna unaweza kuzibadili.
Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK089; Mafanikio Yanataka Uzito, Lakini Dunia Inakuhadaa Na Wepesi