Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Mafanikio ni kitu kinachopendwa na wengi, lakini wachache sana ndiyo wanaoyapata. Na siyo kwa sababu mafanikio yametengwa kwa ajili ya watu hao wachache, bali kwa sababu kinachohitajika kufanyika ili mafanikio yapatikane ni tofauti kabisa na wengi wanavyofikiri.
Watu wengi wanataka wapate mafanikio makubwa, lakini pia waendelee kuwa na maisha ambayo tayari wanayo. Hawataki chochote kibadilike kwenye maisha yao, ila wanataka mafanikio yaongezeke. Hilo halijawahi kutokea na wala halitakuja kutokea.
Ukiacha kazi kubwa ambayo mtu unapaswa kufanya ili upate mafanikio makubwa, kazi ambayo itakutesa, unahitaji pia kugombana na watu sana ndiyo uweze kufanikiwa.
Mafanikio makubwa yanakutaka uvunje sheria nyingi ambazo umekuwa unazifuata kwa adabu kubwa. Na kufuata sheria hizo, japo kunakufanya uonekane mtu muungwana, kumekuwa kunakukwamisha kupata mafanikio makubwa unayoyataka.
Kabla hujakimbilia kwenda kuvunja kila aina ya sheria, soma kwa kina hii #BaruaYaKocha ili uweze kuielewa dhana ya kuvunja sheria zote ili ufanikiwe.

1. Uongo Uliojengewa Kwenye Malezi Na Elimu.
Sehemu kubwa ya malezi na elimu tuliyopata, kwa kipindi chote cha ukuaji wetu ilikuwa ni kutufanya tufuate sheria na taratibu mbalimbali. Na tuliaminishwa kabisa kwamba kama tutafuata kila utaratibu ambao umewekwa, tutapata kile ambacho tunastahili kupata.
Malezi hayo yamekuwa na nia njema, ya kujenga jamii iliyostaarabika na yenye watu wanaoshirikiana kwa manufaa ya watu wote. Lakini utekelezaji wake umetengeneza watu ambao wanashindwa kujisimamia wenyewe na kufanya makubwa ambayo wanaweza.
Ni kama malezi na elimu hizo zimefunga ile nguvu kubwa tuliyozaliwa nayo na kutufanya tusubiri kupewa maelekezo ya nini cha kufanya na kufanya hivyo. Kadiri elimu na malezi hayo yalivyosisitizwa, ndivyo madhara yake yamekuwa makubwa kwa watu, kwa kuwazuia wasifanikiwe.
Tungedhani baada ya kutoka kwenye mfumo wa elimu na chini ya wazazi/walezi, mtu anapokuwa na maisha ya kujitegemea basi angeweza kuwa huru kuyaishi maisha yake. Lakini badala yake anarudi kufuata maelekezo na taratibu anazopewa na serikali, dini na jamii inayomzunguka.
Huo utii, ambao unapendwa na wenye mamlaka mbalimbali, unazirahisishia mamlaka hizo kupata watu wanaotekeleza matakwa yao. Lakini pia utii huo unaondoa ule moto wa mafanikio makubwa unaokuwa ndani ya mtu na kumsukuma kufanikiwa.
Mfumo wote huo wa utii na unyenyekevu umekuwa uongo mkubwa ambao umekukwamisha sana kufanya makubwa kwenye maisha yako. Umeaminishwa ukifuata taratibu zote utapata matokeo mazuri, lakini kila siku unawaona wanaopata matokeo ni wale ambao hawafuati utaratibu kama wewe.
Na hiyo ni kwa sababu watu hao walipata bahati ya kujua mapema kitu utakachoenda kukijua leo. Na kama utakifanyia kazi, basi utatoka chini ya ukandamizi ambao umewekwa na kuwa huru kujenga mafanikio makubwa.
2. Asilimia 90 Ya Sheria Ni Mazoea.
Kuna sheria na taratibu nyingi ambazo unazifuata, ukiamini ndiyo mambo yalivyo na huna cha kufanya. Lakini ukweli ni huo, asilimia 90 ya sheria na taratibu unazofuata ni mazoea tu. Yaani hazina ushahidi wowote wa kwa nini ziko hivyo.
Kuna vitu vidogo vidogo ambavyo mimi huwa naamuaga tu kukataa kwenye maisha yangu, halafu watu wananiuliza haipaswi kuwa hivyo. Na mimi huwa nawauliza swali moja tu, nionyeshe sheria gani na ushahidi gani kwamba haipaswi kuwa hivyo?
Hapa nitaweka mifano michache, lakini ipo mingi. Tuna mtoto wetu, ambaye tangu amezaliwa hatujawahi kumnyoa nywele. Ilipofika ile miezi ambayo kwa utaratibu ndiyo watoto wanatakiwa kunyolewa nywele, niliwauliza waliotaka hilo lifanyike wanipe sababu, hakuna hata mmoja aliyeweza kunipa sababu ya msingi. Wengi waliishia kusema nywele za kuzaliwa nazo lazima zinyolewe ndiyo ziote nywele halisi, kitu ambacho hakuna ushahidi ulioweza kutolewa. Basi ukawa ni mjadala wa kila mara na kila aliyeuliza, hatukumnyoa na hiyo habari iliisha.
Kuna mambo mengi sana ambayo umekuwa unahangaishwa nayo kwenye maisha yako ya kila siku na unakazana kuyafuata na hayana mchango wowote kwenye maisha yako.
Na ubaya ni kwamba, mambo hayo yanayokuhangaisha, yanakukwamisha wewe kupeleka nguvu kubwa kwenye kupambania mafanikio yako. Unapoteza muda na nguvu kwenye mambo yasiyokuwa na tija kabisa.
Anza kwa kuhoji kwa nini unafanya kila ambacho unaambiwa na wengine ufanye. Tafuta ushahidi wa kwa nini ni lazima vitu hivyo vifanyike na jua madhara ya kutokufanya.
Kitu kimoja kitakachokushtua ni kwamba karibu kila kitu unachoweza kuamua kufanya, unaweza pia kuamua kutokufanya bila ya madhara yoyote kwako. Kinachofanya mpaka sasa uwe unafanya ni mazoea ambayo umekuwa nayo kwenye kufanya vitu hivyo.
Safari yako ya mafanikio makubwa inaanzia kwenye kupunguza mambo yasiyo na tija ambayo yanachukua muda wako, nguvu zako na umakini wako. Usikubali kuendelea kufanya mambo kwa mazoea, hoji na achana na yote ambayo hayana ushahidi wa ulazima wake kufanyika.
Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK116; Kufanikiwa, Vunja Sheria Zote