Kukutana na changamoto na vikwazo kwenye maisha hilo ni jambo ambalo lazima litokee. Hata uwe umejipanga vipi, una utajiri kiasi gani kuna vitu havitakwenda kama wewe ulivyopanga kwenda.
  Pamoja na kujua hilo lakini bado unapokutana na vikwazo ambavyo ni vikubwa sana vinakuyumbisha kwa kiasi kikubwa sana. Unajua kabisa kwamba imeshatokea ila bado huwezi kujipa moyo na kuendelea na mipango mingine.
  Hii inasababishwa na wewe kufikiri kwamba hilo tatizo ulilopata litaadhiri sana maisha yako ya baadae. Unaogopa kufanya jambo fulani ambalo lingekusaidia, kwa sababu kama ukikosea utaharibu maisha yako ya baadae. Tunajenga picha kwamba kama tukikutana na vikwazo vikubwa ama changamoto kubwa sana basi hapo ndio MWISHO WA DUNIA na maisha yetu ya mbele yamefutika kabisa.
        
sio mwisho wa dunia 2
  Hii ni picha ya kutisha na ya uongo kabisa uliyoibeba kwenye akili yako. Na picha hii imekuzuia sana kufanya mambo makubwa kwenye maisha yako ambayo yangeyabadili maisha yako kwa kiasi kikubwa. Leo ondoa picha hiyo kwa kujua kwamba kwa lolote litakalotokea kwenye maisha yako kama bado uko hai basi jua huo sio mwisho wa dunia. Maisha yataendelea na ni uamuzi wako kama utataka yawe maisha mazuri au yawe maisha mabaya.
  Kama umeweza kufika hapo ulipo sasa hakuna sababu yoyote inayoweza kukuzuia kufika mbali siku zijazo. Unajiogopesha kwa kuona kama ukipoteza ulichonacho sasa basi hutaweza kupata kingine kesho, uongo mkubwa sana na umekuwa unajidanganya kila siku.
  Maisha yapo na yataendelea kuwepo mpaka pale utakapokufa. Lolote linalotokea kwenye maisha yako wewe ndiye mwenye uamuzi wa kuboresha maisha yako zaidi ama kuyaharibu zaidi.
  Usiogope kufanya maamuzi kwa sababu unafikiri ukifanya maamuzi mabaya maisha yako ya baadae yataharibika sana. Kwa vyovyote vile kufanya maamuzi ni bora kuliko kutofanya maamuzi. Ukifanya maamuzi mazuri utafanikiwa, na ukifanya maamuzi mabaya utajifunza. Usipofanya maamuzi kabisa hutofanikiwa wala hutojifunza na utaendelea kuwa na hofu kubwa kuhusu maisha ya kesho.
  Usijiogopeshe na kushindwa kufurahia maisha kwa sababu tu unaogopa ukiharibu leo kesho imefutika. Kama unafanya jambo ambalo ni halali kiutu na kisheria basi huna haja ya kuogopa. Ila usisome hapa kisha ukafanye uhalifu kwa kuamini kwamba maisha yataendelea, kwa sababu baada ya hapo hutokuwa na amani kwenye maisha yako.
  Ujumbe muhimu kwako ni “kama umeweza kufika hapo ulipo basi hakuna kitakachokuzuia kufika mbali siku za mbeleni”