Habari za leo ndugu msomaji? Naamini unaendelea vizuri na harakati za kuboresha maisha yako. Hata kama huendelei vizuri, muda sio mzrefu mambo yako yatakuwa vizuri. Badili mtazamo wako na acha kujiona mwenye hatia. Wewe ni mshindi, ulizaliwa kuwa mshindi. Usikubali tena kuendelea kuwa mtumwa wa mawazo ya watu wengine.

Karibu tena kwenye kujenga tabia za mafanikio. Mwezi huu tunazungumzia tabia ya kupenda kujisomea na jinsi inavyoweza kukunufaisha. Najua tayari umeshajua ni jinsi gani tabia hii inaweza kukunufaisha. Wiki iliyopita tulijadili ni kwa nini watu wengi hawapendi kujisomea na tuliona ni kwa sababu ya mtazamo tuliojengewa na kujijengea tokea tukiwa watoto wadogo. Hivyo kama unataka kujijengea tabia hii huna budi kuvunja kabisa mitazamo hii.

Wiki iliyopita nilitoa kitabu kwa ajili ya kujisomea, sijajua ni wangapi waliosoma, ila nina uhakika wewe hujamaliza kukisoma. Kama umemaliza kukisoma kuna biashara tatu ambazo mwandishi alizipendekeza mtu afanye kama kweli anataka kuwa na uhuru wa kifedha na maisha. Mbili kati ya biashara hizo zinaweza kufanyika hapa Tanzania na mtu ukawa na mafanikio makubwa sana, ndio hata mimi nazifanya. Kama ulisoma na kuona biashara hizo niambie kisha nitakupa mpango mzuri sana kuhusiana na biashara hizo mbili na kama utazifanya baada ya muda mfupi utakuwa na uhuru wa kifedha na maisha. Niandikie email kwenda amakirita@gmail.com kunieleza biashara hizo alizozungumzia mwandishi kisha nikupe fursa zaidi ya kuweza kunufaika nazo. Kama hukusoma ndio fursa inakupita hivi hivi, nataka kuwaonesha ni jinsi gani kusoma kunaweza kukutengenezea fursa ambazo ulikuwa huzijui au kuzifikiria. Karibu sana kwa wale ambao wamesoma na wanataka kutumia fursa hizo.

Wiki hii tutajadili jinsi ya kupata muda wa kusoma na jinsi ya kupata vitabu vya kujisomea.

Unapata wapi muda wa kujisomea?

Najua niliposema wale waliosoma kitabu nilichotoa wiki iliyopita wanitafute niwape fursa umeanza kunilaumu japo kimoyomoyo. Kwamba huyu ndugu anatutenga kama hatujasoma hajui wengine hatuna muda kabisa wa kujisomea, tuko bize sana na maisha na kazi halafu bado haelewi hilo. Asante sana ndugu yangu, mimi naelewa uko bize na kazi na maisha pia, ila kabla sijakubaliana na wewe kwamba uko bize na maisha yako naomba unihakikishie kwamba hufanyi mambo yafuatayo.

1. Huangalii TV siku nzima na kila siku kwenye maisha yako.

2. Husomi magazeti au kufuatilia habari nyingine kwa njia nyingine.

3. Haupo facebook, twitter, g+, linkedin, wasap, na hata instagram.

4. Hulali zaidi ya masaa nane kwa siku.

5. Hukai baa na marafiki hata siku moja kwenye wiki.

6. Hujawahi kukaa kwenye foleni ya magari au kusubiri huduma nyingine.

7. Husomi na kujibu emails kila siku.

8. Hutumii simu.

Na kama hufanyi hata moja kati ya hayo hapo juu HUNA MAISHA.

Kitu nataka kukuambia hapa ni kwamba kwa maisha yoyote unayoishi kuna sehemu unapoteza muda, amini hilo. Unaweza kujiona wewe uko bize sana lakini tukikaa na tukaangalia siku yako kiundani kuna karibu masaa mawili unayapoteza kila siku.

Muda huu unaopoteza ndio muda mzuri kwako kuutumia kujisomea. Punguza sana muda unaotumia kuangalia tv, au kufuatilia habari nyingine. Sehemu kubwa ya habari unazolishwa kila siku ni za uongo na zimeongezwa chumvi ili kukukamata uendelee kufuatilia au kuzinunua(magazeti), ukiweza kupunguza muda unaotumia kwenye habari hizi itakusaidia sana kwenye maisha yako.

Punguza muda unaotumia kwenye simu yako. Tafiti zinaonesha watu wanaomiliki smartphones wanaziangalia simu zao zaidi ya mara 50 kwa siku. Sasa kama na wewe unaiangalia simu yako zaidi ya mara 50 kwa siku na hutengenezi fedha yoyote katika kuiangalia ni vyema ukarekebisha matumizi yako ya simu.

Yote hayo na mengine ambayo tulijifunza kwenye TABIA YA MUDA ni muhimu sana kuyaweka vizuri ili kuweza kupata muda wa kujisomea. Unahitaji nusu saa au saa moja tu kwa siku kwa ajili ya kujisomea na baada ya hapo unaweza kufanya mambo yako mengine. Nakusisitiza sana ujisomee kwa sababu najua asilimia 90 ya vikwazo vyako vya maendeleo inaweza kutatuliwa kwa kujisomea.

Unapata wapi vitabu vya kujisomea?

Wiki iliyopita nilizungumzia kwa kifupi aina au mifumo ya vitabu unavyoweza kujisomea. Tuliona vitabu vilivyochapwa, vitabu vilivyosomwa na vitabu vya kusomea kwenye kompyuta au simu. Hapa tutaangalia ni jinsi gani ya kupata vitabu vizuri kwa aili ya kujisomea.

1. Vitabu vilivyochapwa.

Kupata vitabu hivi nenda kwenye duka la vitabu na uangalie vitabu vinavyohusiana na mada unayopendelea kisha ununue. Kwa wale wanaokaa dar, kuna wauzaji vitabu wanaokaa barabarani maeneo ya ubungo, kariakoo, posta na hata mnazi mmoja. Wauzaji hawa wanavitabu vizuri sana na bei zao ni nzuri. Unaweza kuwa unaweka utaratibu wa kununua kitabu kila wiki au hata kila mwezi kutoka kwa watu hawa. Kwa wauzaji wa barabarani vitabu vinakwenda kati ya tsh elfu tano na tsh elfu kumi. Kwenye maduka ya vitabu bei huwa inakuwa juu kidogo ila bado sio mbaya kulingana na kitu utakachokipata kutoka kwenye kitabu.

2. Vitabu vya kusoma kwenye kompyuta au simu(softcopy, pdf).

Vitabu hivi ni rahisi sana kuvipata kwenye mtandao wa intanet. Kuna ambavyo unaweza kupata bure, kuna vingine itakubidi uvinunue kupitia mtandao wa intaneti. Kupata vitabu vya bure nenda kwenye google kisha andika jina la kitabu na mwishoni malizia na neno PDF DOWNLOAD. Kwa mfano tuseme unataka kudownload kitabu THINK AND GROW RICH, nenda kwenye google kisha andika THINK AND GROW RICH PDF DOWNLOAD, ukisearch yatakuja machaguo mengi sana ila wewe bonyeza yale ambayo yatakuwa yameanza na neno PDF mwanzoni. Kwa kubonyeza hapo kitabu kinaanza kudownload moja kwa moja. Angalia picha hapa chini kama hujaelewa vizuri; Kwa mfano kwenye hii picha nimebonyeza link ya kwanza kabisa na nikapata kitabu.

download

Unaweza kutumia mbinu hii kupata vitabu vingi sana unavyotaka. Kama hakipatikani bure watakuletea link ya AMAZON ambapo utatakiwa kulipia ili kupata kitabu hiko.

Sehemu nyingine unazoweza kupata na kudownload vitabu ni 4shared.com, 2shared.com na sehemu nyingine nyingi zinazotoa vitabu.

Njia rahisi ya kupata vitabu ni kwa kusikia kitabu kizuri kisha wewe ukaenda kukitafuta. Nakushirikisha yote haya lakini hakuna mtu amewahi kunifundisha hata kitu kimoja, ni njaa yangu ya kujifunza imenipatia yote haya.

Kuwa mwangalifu na vitabu vya kusomea kwenye kompyuta au simu mara nyingi utajikuta unafanya mambo mengine badala ya kusoma. Hivyo nizamu ni muhimu sana linapokuja swala la kujsomea.

Vitabu vingine vya mfumo huu unaweza kununua kwenye AMKA MTANZANIA kuna vitabu kama KWA NINI MPAKA SASA WEWE SIO TAJIRI na JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG kama utahitaji kupata vitabu hivi wasiliana nami.

3. Vitabu vilivyosomwa.(AUDIO BOOKS)

Hii ndio aina bora sana ya vitabu kwangu kwani unaweza kusikiliza na kupata mambo mazuri ukiwa unatembea, ukiwa kwenye foleni, ukiwa unafanya jambo ambalo halihitaji kufikiri na hata ukiwa umepumzika. Vitabu hivi unaweza kusikiliza kwenye simu, redio, tv, na kifaa chochote kinachopiga muziki. Kuna vitabu vingi sana vizuri viko kwenye mfumo huu. Na uzuri wake ni kwamba kwa mfumo huu unaweza kumaliza kusikiliza kitabu kizima ndani ya siku moja, vipi ukisikiliza mwezi mzima? Vitabu 30, utakuwa na maarifa mara 30 ya uliyonayo sasa. Kama utataka kupata vitabu hivi bonyeza maandishi haya na ujue list ya vitabu ninavyoweza kukupatia kisha uniambie nikutumie. Natoa nafasi ya upendeleo kwa WANAKISIMA kwa sababu nilishaacha kutoa vitabu hivi.

Jiwekee lengo la kusoma angalau kitabu kimoja kwa wiki. Tenga angalau nusu saa kwa siku ya kusoma, na mwisho wa wiki pale unaposhawishika kuangalia TV au muvi chukua kitabu na usome, utafaidika mara 100 ya utakavyofaidika kwenye muvi.

ZOEZI LA WIKI.

Wiki hii tutajisomea kitabu kinachoitwa 100 SIMPLE SECRETS OF SUCCESSFUL PEOPLE. Hapa utajifunza siri 100 zilizofanyiwa utafiti na kudhibitishwa kisayansi za watu waliofanikiwa. Kwa kuwa wewe unatengeneza tabia za kuwa na mafanikio makubwa kwenye maisha yako basi hiki sio kitabu cha kuacha kusoma. Kupata kitabu hiki bonyeza maandishi ya kitabu hapo juu(jina la kitabu)

Ni kitabu kizuri sana kitakachokupa mwanga wa vitu gani ufanye na vitu gani uache kufanya ili uweze kufanikiwa. Kitabu kina siri 100, una siku saba za kukisoma hivyo kila siku soma siri 15 ili kukimaliza ndani ya siku hizi saba. Baada ya hapo utakuja urudie tena kukisoma huku ukijenga tabia husikw kwako ili uweze kufanikiwa.

Kumbuka ni muhimu tukawa tunashirikishana yale tunayosoma ili kuweza kuelewa zaidi. Tushirikishane kwenye FORUM-MAJADILIANO 

Nakutakia kila la kheri katika mafanikio yako, TAYARI WEWE NI MSHINDI, unatakiwa kuchukua ushindi wako.

TUKO PAMOJA.