Naomba nianze kwa kuwashukuru sana wasomaji wote wa AMKA MTANZANIA kwa ushirikiano mkubwa mnaoendelea kuonesha. Watu wengi mmekuwa mkiniandikia kunieleza ni jinsi gani mtandao huu umekuwa na manufaa kwenu. Pia wengi wenu mmemkuwa mkiwashirikisha marafiki zenu ili nao wapate mambo haya mazuri. Nasema asanteni sana kwa sababu hili ndio lengo kubwa la AMKA MTANZANIA, kuweza kuwafikia watanzania wengi zaidi tunategemea nguvu zetu za kuwashirikisha wengine.

Kutokana na ushirikiano wako mzuri sasa baadhi ya makala za AMKA MTANZANIA zitakuwa zinachapwa kwenye gazeti la MTANZANIA siku za jumanne kwenye kona ya mjasiriamali. Hivyo wale ambao hawawezi kufikia mtandao wanaweza kupata baadhi ya vitu vizuri tunavyojadili hapa kupitia gazeti hilo kwa siku za jumanne. Ni hatua kubwa sana ambayo tumepiga na hii yote imetokana na wewe msomaji.

MTANZANIA

Leo naomba tujadili kuhusu swala la kusubiri uchaguliwe au kujichagua mwenyewe.

Kama kweli unataka kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako usisubiri mtu yeyote akuchague ndio uweze kufanya mambo makubwa, jichague mwenyewe. Wewe mwenyewe amua kufanya mambo makubwa zaidi ya unayofanya sasa, sio kwa sababu kuna mtu amekuambia ufanye ila kwa sababu ndio uwezo wako ulivyo na unataka kuufikia.

Kipindi cha zamani watu wengi walikuwa wanakaa wakisubiri watu wawaambie unaweza kufanya hiki au huwezi kufanya kile, lakini ulimwengu wa sasa unaweza kufanya chochote unachowaza kufanya kama utajichagua mwenyewe.

Nilipoanza kuandika na kuendesha blog, hakuna mtu aliyeniambia, Amani sasa hivi anza kuandika, na wala hakuna mtu yeyote aliyewahi kunielekeza jinsi ya kuandika au kuendesha blog yenye mafanikio. Na hata nilipokuwa naandika sikupata wasomaji wengi kwa mara moja, na hata wengi hawakuamini kama kuna kitu cha tofauti nafanya. Hata marafiki zangu wa karibu walijua hii ni blog nyingine ambayo itakuwa kama blog zilizopo. Nilikuwa na kila sababu ya kuacha ila kwa sababu nilikuwa na picha kubwa kwenye kichwa changu sikusikiliza neno hata moja la kukatisha tamaa.

Sasa blog hii inawafikia watu wengi na watu wengi wanakiri maisha yao kubadilika kutokana na yale wanayojifunza hapa.

Haya ni mafanikio kidogo sana ukilinganisha na picha kubwa niliyoko nayo kichwani mwangu, lakini ni mafanikio yenye maana kubwa kwangu na kwa wasomaji wote. Kama ningesubiri mtu anichague au anihalalishe kwamba wewe unaweza kuandika, au huwezi leo hii usingejua kitu kinaitwa AMKA MTANZANIA.

Nakutia moyo sana kwamba unaweza kufanya kitu cha tofauti popote pale ulipo, iwe huna ajira, umeajiriwa au umejiajiri mwenyewe. Jambo la kwanza unalotakiwa kufanya ni kujichagua wewe kwanza, kuamini unaweza na kufunga masikio kwa wakatishaji tamaa.

1. Kama hujaajiriwa na kila siku unazunguka na bahasha ina maana hapo bado unatafuta mtu wa kukuchagua. Kwa nini usiachane na mtazamo huo na kuamua kujichagua mwenyewe, ukachagua kitu kimoja unachotaka kufanya, ukaweka nguvu zako? Kama ukijitoa kweli kwenye kitu ulichochagua nakuhakikishia utapata mafanikio makubwa sana. Nikikuambia uache kusubiria kuajiriwa na ujiajiri au ufanye biashara utasema huna mtaji, hii ndio njia rahisi uliyotumia kuhalalisha subira yako ya kuchaguliwa. Yaani ni kama unasubiri mtu aje na fedha zake akuambie sasa John chukua hizi milioni nenda kafanye biashara maana umesubiri sana bila ya ajira! Hizi ni ndoto za mchana unaota rafiki yangu. Kuna biashara nyingi sana unaweza kuanzisha bila ya kuwa na mtaji au hata kwa mtaji kidogo sana. Pia kuna njia nyingi unaweza kuzitumia kukusanya mtaji ili kuweza kuanza biashara yako. Kwa ushauri zaidi juu ya hili nitumie email kwenye amakirita@gmail.com

2. Kama umeajiriwa usisubiri mtu akuchague kwamba unaweza kufanya majukumu ya ziada au kuongeza ufanisi wako kazini. Hiki ni kitu ambacho kinatakiwa kutoka ndani yako na kama ukifanya vyema kwenye hili utapata mafanikio makubwa sana kwenye kazi yako hiyo. Ni jambo la kushangaza sana watu wanatumia muda mwingi kutafuta kazi halafu wakishaipata hawafanyi kazi ya maana. Watu wapo wapo kwenye kazi, wanachelewa kuanza kazi na wanawahi kufunga kazi. Kati kati ya kazi ni klutafuta sababu za hapa na pale za kuwafanya wazunguke zunguke badala ya kufanya kazi na kupoteza muda mwingi kwenye mitandao kuangalia vitu ambavyo havina msaada wowote kwenye maisha yao. Wakimuona mwenzao ameamua kujichagua na kufanya majukumu ya ziada, wanaleta majungu, na kumkatisha tamaa. Ikifika wakati mwenzao akapandishwa cheo au kupewa zawadi wanaleta tena majungu na kuona amependelewa. Kama na wewe upo kwenye kundi hili la wafanyakazi naweza kukuhakikishia jambo moja tu, HUTOWEZA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KWENYE KAZI HIYO.

Acha kusubiri mtu akuchague, jichague mwenyewe na jua ya kwamba unaweza kufanya mambo makubwa, usilalamike bali chukua hatua na baada ya muda mfupi utaona mabadiliko makubwa kwako na kazi yako.

3. Kama umejiajiri, unafanya biashara au ndio una mpango wa kuingia kwenye njia hii usisubiri hata kidogo mtu akuambie ni kitu gani unaweza na kitu gani huwezi. Amua wewe ni kitu gani unataka kufanya, weka nguvu zako na akili yako yote kwenye kitu hicho, ng’ang’ania na baadae utaona mafanikio makubwa. Kosa kubwa la watu wanaoingia kwenye biashara ni pale wanapoangalia ni biashara gani inalipa na wao kuiga wakiamini ndio njia ya mafanikio. Mafanikio yapo kwenye jambo lolote ambalo unalifanya kwa juhudi na maarifa na unafurahia kulifanya.

Ni wakati wa wewe kuamua, unasubiri wakuchague na wakuambie wewe unaweza kuimba, kuchora, kuandika au kufundisha? Au utajichagua mwenyewe na kuweka juhudi na maarifa katika uimbaji wako, usanii wako, uandishi wako na hata uzalishaji wako kwenye kazi? Hili ni jibu ambalo unaweza kulijibu wewe mwenyewe.

Kama umeamua kujichagua mwenyewe nakupa hongera kubwa kwa sababu umeshafika hatua ya kwanza ya kuelekea kwenye mafanikio. Kufuata hatua nyingine za mafanikio ikiwemo kujenga tabia za mafanikio nakusihi sana ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA ili uweze kupata maarifa muhimu ya wewe kufikia mafanikio makubwa kwenye jambo lolote unalofanya. Kupata taarifa zaidi kuhusu kisima bonyeza hayo maandishi ya herufi kubwa.

Ombi muhimu.

Kwa kuwa lengo letu kubwa ni kuwafikia watanzania wengi zaidi naomba tushirikiane kusambaza ujumbe huu ili watanzania wengi zaidi waweze kuupata. Njia moja ninayopendekeza pamoja na nyingine tunazofanya ni kualika marafiki zetu kulike ukurasa wetu wa facebook.

Nenda kwenye ukurasa wa facebook wa AMKA MTANZANIA(bonyeza hayo maandishi), kama hujalike bonyeza like na kisha kuna sehemu imeandikwa INVITE FRIENDS bonyeza pale kuwaalika marafiki zako nao waulike. Kama tayari umeshalike bonyeza maandishi hayo na ukifika kwenye ukurasa waalike marafiki zako walike ukurasa huu.

Napendekeza kwa mwezi huu wa sita tufikishe watu elfu kumi wanaolike ukurasa huu. Sasa hivi wamelike watu elfu moja na mia saba hivi, kwa kuwa makala hii itasomwa na zaidi ya wasomaji elfu moja mapendekeza kila mmoja aalike marafiki ishirini kati ya hao ishirini kumu wataitikia na kulike hivyo tutafikia watu elfu kumi ndani ya siku moja.

Nategemea sana ushirikiano wako katika hili, fanya jambo hili dogo na utakuwa sehemu ya mageuzi ya kifikra katika taifa letu la Tanzania.

Asante san kwa kuendelea kuwa msomaji wa AMKA MTANZANIA,

TUKO PAMOJA.