Tafiti mbalimbali za kiuchumi zinaonesha kwamba ndani ya miaka kumi ijayo (2015 – 2025) Tanzania itakuwa ni moja ya nchi ambazo uchumu wake utakua kwa kasi kubwa sana. Zipo sababu nyingi zitakazosababisha hili, ila moja ambayo ni kubwa sana ni ugunduzi wa kiasi kikubwa sana cha gesi asilia.

Ugunduzi huu wa gesi utavutia wawekezaji wengi sana kuja kuwekeza hapa nchini. Hivyo katika kipindi hiki ambacho uchumi utakua kwa kasi kubwa sana, kuna watu wengi sana watakuwa matajiri. Swali ni je wewe utakuwa mmoja wa watu hao? Je wewe utanufaika na ukuaji huu wa kasi wa uchumi?

Kwa sehemu kubwa sana ya watanzania jibu ni hapana, hawatanufaika na ukuaji huu wa uchumi. Yaani tutakuwa na uchumi ambao unakua kwa kasi sana na ukuaji huo utatengeneza matajiri wengi ila kwa bahati mbaya sana wengi watakuwa sio watanzania.

GESI

Watanzania wengi hawatanufaika na ukuaji huu wa uchumi kwa sababu hawajaandaliwa na hawajajiandaa pia. Huna haja ya kwenda darasani kulisoma hili, mana tumeliona wazi wazi kwenye rasilimali ya madini. Tumeshuhudia wawekezaji wakichimba madini mpaka yanaisha huku jamii inayozunguka machimbo hayo ikiwa haina hata huduma za msingi za maisha na watu wakiwa na maisha magumu sana. Haya ndio yanakwenda kutokea tena kwenye gesi kama tutaendelea kama tulivyo.

Tukiangalia nchi nyingi zenye rasilimali kubwa hasa za Afrika zote zina hadithi inayofanana. Wageni wananufaika na rasilimali huku wazawa wakiwa na maisha magumu au wakiwa ‘bize’ kupigana. Angalia mfano wa Nigeria, Sudan na Congo kote utaona utajiri mkubwa sana wa rasilimali ambao haumnufaishi mwananchi wa hali ya chini.

Ufanye nini ili uweze kunufaika na ukuaji huu wa uchumi?

Kuna mambo mengi sana unayoweza kufanya wewe kama mwananchi yatakayokuwezesha kunufaika na sehemu hii ya picha kubwa.

Moja ya mambo hayo ni kuishinikiza serikali kuweka sera nzuri ya uwekezaji kwenye rasilimali hii kubwa ili iweze kumnufaisha kila mwananchi. Sera nzuri itapelekea kuwa na mikataba mizuri ambayo itatunifaisha kama taifa. Njia hii ya kwanza tumeona ikipigiwa kelele sana na baadhi ya wanasiasa na wafanyabiashara wakubwa. Mfano watu wa Mtwara walijaribu kushinikiza gesi iwanufaishe kwanza wao kabla ya kupelekwa kwingine.

Jambo la pili kubwa unaloweza kufanya na unalotakiw akufanya wewe kama mtanzania ni kuingia kwenye uwekezaji katika uchumi huu unaokua kwa kasi.

Kwa kuwa sisi hapa AMKA MTANZANIA hatuishii kulalamika au kulaumu tu na kwa kuwa tunaamua kuchukua hatua juu ya maisha yetu wenyewe, huu ndio wakati mzuri wa kuchukua hatua hiyo

Huu ndio wakati wa kuchukua hatua ya kuwekeza kwenye uchumi huu unaokua kwa kasi sana ili na sisi tuweze kunufaika kwa kiasi kikubwa.

Utawekezaje kwenye gesi wakati huna hata hela ya kuanzisha biashara ndogo? Ninaposema tuwekeze kwenye uchumi huu unaokua sio lazima na wewe ununue kitalu cha gesi na uanze kuchimba au sio mpaka uingie kwenye mfumo wa usambazaji wa gesi, japo unaweza kufanya hayo kama upo kwneye biashara au unapanga kuingia kwenye biashara.

Kuna aina nyingine nyingi za uwekezaji ambazo zitamwezesha kila mtanzania kunufaika na uchumi huu. Katika kipindi hiki ambacho uchumi utakua kwa kasi sana, makampuni mengi yatakuja kuwekeza Tanzania na makampuni haya yatakuwa ya umma kwa maana kwamba yatauza hisa zake kwa wananchi. Huu ndio wakati wa wewe mtanzania kununua hisa za makampuni mbalimbali na hatimaye kunufaika kwa hisa zako kadiri uchumi unavyokua.

Najua watanzania wengi hatuna elimu hizi za uwekezaji hasa kwenye hisa ndio maana nimeandika hili leo ili kukumbushana tufanye nini. Watanzania hatuna elimu hizi na wala hatutaki kuzitafuta kwa sababu tumeshazoea kufanya mambo kwa mazoea. Kama wewe ni mfanyakazi umezoea kufanya tu kazi na kusubiri mshahara wako. Kama wewe ni mjasiriamali umezoea tu kufanya ujasiriamali wako au biashara. Kwa ufupi watanzania wengi tunafanya mambo ambayo wanaotuzunguka wanayafanya, hatujifunzi mambo mapya na hivyo kukosa nafasi nzuri ya kunufaika.

Leo jifunze kuhusu uwekezaji kwenye soko la hisa ili ujue unaweza kuanzia wapi. Sio kitu kigumu na wala haihitaji uwe na mamilioni ya fedha ndio uweze kuingia kwenye uwekezaji huu. Unachohitaji ni kuwa na taarifa sahihi kwenye muda sahihi.

Unaweza kujifunza zaidi kuhusiana na uwekezaji kwenye hisa na jinsi ya kunufaika nao kwa kubonyeza maandishi haya, UWEKEZAJI TANZANIA.

Anza sasa kuchukua hatua juu ya maisha yako kwa kuingia kwenye uwekezaji wa uchumi huu unaokua kwa kasi sana. Usisubiri kwamba mambo yatakuwa mazuri yenyewe, ni nafasi yako sasa kuyafanya yawe mazuri.

Nakutakia kila la kheri katika uwekezaji na mafanikio.

TUPO PAMOJA.

kitabu-kava-tangazo4323