Hofu ni kitu ambacho kipo karibu kwa kila binadamu aliye chini ya jua. Hofu hizi huwa zipo za aina mbalimbali na huweza kutofatiana kati ya mtu mmoja na mwingine. Wapo ambao mara nyingi huwa wakihofia sana kifo, wengine huweza kuhofia kesho yao pia wapo ambao huweza kuhofia juu ya kuanza na kufanya jambo jipya katika maisha yao.
Hizo zote ni baadhi ya hofu ambazo huwa zinasababisha ama kutokana na mazingira tofauti tofauti kulingana kati ya mtu na mtu. Hofu hizi zinapozidi sana katika maisha yetu huwa ni hatari sana na zinakuwa kuzuizi cha kutufanya tushindwe kufikia kule tunakotaka kufika kimafanikio. Wakati mwingine hofu hizi huwa siyo za kweli kama wengi tunavyozichukulia.
Kwa kujua zaidi ukweli huu hebu jaribu kujiuliza ni mara ngapi mambo ambayo uliwahi kuyahofia katika maisha yako yalitokea kweli kama ulivyokuwa ukiyahofua? Kama yapo basi ni machache sana. Kama ni hivyo nini hasa kinachokufanya uwe na hofu sana katika maisha yako? Ni mambo gani ya kukumbukaa hasa pale unapokuwa na hofu ili yakusaidie kusonga mbele?
1. Acha kufikiria sana juu ya jambo linalokupa hofu.
Kama utakuwa unafikiria sana juu ya jambo linalokusumbua ni wazi kuwa hofu hiyo ndivyo ambavyo utazidi kuikuza na kuifanya iwe kubwa zaidi. Ili kuweza kuondokana na hali hiyo unalazimika kuachana na kutoendelea kufikiria sana juu ya jambo linalokupa hofu. Kwa kufanya hivyo utakuwa unaishinda hofu hiyo bila wewe kujua. Kutokufikiria sana juu ya jambo linalokupa hofu ni mbinu mojawapo muhimu ya kukumbuka wakati unapokuwa na hofu ya kitu chochote kile.
2. Hofu yako haiwezi kukusaidia kukufanikisha.
Hata uwe na hofu vipi juu ya jambo lolote lile, lakini ukweli utabaki wazi kuwa hofu yako hiyo haitaweza kukusaidia kufikia malengo yako hata iweje. Kama ni hivyo ni kipi hasa kinachokufanya uendelee kuogopa? Kama kuna jambo gumu liko mbele yako livae hivyohivyo.  Hofu uliyonayo inakuzuia kufanikiwa kwako kwa mambo mengi sana bila ya wewe kujijua. Ili kusonga mbele zaidi, kumbuka kuachana na hofu yako mara moja, vinginevyo utakuwa mtu wa kushindwa sana katika maisha yako.
3. Hofu hiyo uliyonayo haiko kwako tu.
Mara nyingi wengi unaowaona hawana kabisa hofu, pia nao huwa nazo ila tu wewe ndiyo hujui. Kama kila mtu ana hofu zake kwanini wewe ya kwako iwe kubwa sana kiasi kwamba inakuzuia mpaka kuweza kufikia ndoto zako? Hii ndiyo hofu ambayo hutakiwi kuwa nayo mpaka ikafikia hatua ikakutawala wewe. Najua kwa vyovyote vile hofu zipo katika maisha lakini zisiwe kubwa sana za kupita kiasi zitatupotezea mambo mengi ikiwemo malengo yetu.
4.  Unapokuwa na hofu ni rahisi sana kwako kushindwa.
Kwa kadri jinsi unavyozidi kuwa na hofu ndivyo ambavyo inakuwa ni rahisi kwako kushindwa. Kwa nini hii inakuwa hivi? Hii yote ni kwa sababu hofu inapozidi kukutawala unajikuta unakuwa hauna uwezo wa  kujiamini mwisho wa siku kila kitu unachofanya kinakuwa hakiko katika ubor a wake. Maisha yako yatakuwa ya maana ikiwa utaweza kuzifutilia mbali hofu zako zinazokusumbua.
Unachotakiwa kuelewa ni kuwa, hofu yoyote ile uliyonayo ni adui mkubwa wa mafanikio yako. Hutafika popote ikiwa utaendeleza kuwa na hofu hata zisizo na maana kwako. Ni wakati umefika wa wewe kuweza kukabiliana na hofu zako bila kuogopa kitu.
Kwa makala nyingine nzuri hakikisha unatembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa elimu na maarifa bora yatakayoboresha maisha yako.
Tunakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio, endelea kutembelea mtandao huu wa AMKA MTANZANIA kwa kujifunza kila siku.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048035,